Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kusimama leo hii mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya ya kizalendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. John Pombe Magufuli anafanya kazi nzuri ya kusimamia uwajibikaji na uadilifu katika Serikali yetu. Pamoja na kazi nzuri bado anaendelea kutumbua majipu ndiyo maana leo hii wenzetu wa upinzani wameamua kuweka mpira kwapani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waswahili wanasema mwenye wivu ajinyonge, tutaendelea kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli na tutaendelea kumuunga mkono kwa kazi anayoifanya katika nchi hii. Kwa namna ya kipekee naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri na kwa kazi nzuri anayoifanya kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mufindi Kaskazini kwa kunirudisha tena katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitaanza kwa kujielekeza katika ukuaji wa uchumi. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema mwaka 2015 uchumi ulikua kwa asilimia 7.1, mwaka 2014 uchumi ulikua kwa asilimia 7. Ni kweli uchumi unakua, lakini ninaomba Serikali inapozungumzia suala la ukuaji uchumi lazima waangalie na hali halisi ya maisha ya Mtanzania. Ukuaji wa uchumi unatakiwa uende sambamba na huduma za jamii kama afya, elimu pamoja na maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele ambavyo amevizungumzia Mheshimiwa Waziri Mkuu vya ukuaji wa uchumi amezungumzia suala la kilimo. Jana katika hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti alisema asilimia 79 ya Watanzania wameajiriwa katika eneo la kilimo, lakini ukuaji katika eneo hili unakua kwa asilimia 3.4 ambao ni ukuaji mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Waziri Mkuu amesema wakulima ni asilimia 66.3 ya Watanzania wote ambao wako kwenye eneo hili. Serikali ni kweli imeona kwamba, zaidi ya asilimia 79 ya Watanzania wameajiriwa katika sekta hii ya kilimo, lakini bado Serikali haijaamua kuwekeza kwenye eneo hili, katika eneo hili hakuna Mbunge ambaye haguswi. Tunaiomba Serikali iangalie kwa macho yote katika eneo hili haswa katika mfuko wa pembejeo, ule mfuko wa pembejeo umewekewa hela ndogo sana kulinganisha na pesa ambazo zinatakiwa ziwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutawekeza vizuri katika eneo hili la kilimo nina hakika kabisa hata eneo ambalo tumekusudia kwenda kwenye Mpango wa Pili wa viwanda tutakwenda vizuri, kwa sababu Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Waziri wa Viwanda ni watoto pacha, kama tutafanya vizuri kwenye kilimo automatically tutafanya vizuri kwenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba sana, kwenye eneo la pembejeo Serikali iongeze mfuko wa pembejeo ikilinganishwa na ilivyo sasa, kwa sababu unawagusa Watanzania karibu wote, aidha inagusa wananchi wa Chama cha Upinzani na wa Chama Tawala, kwa hiyo tunaiomba Serikali iwekeze sana kwenye eneo hili. Lakini la msingi zaidi tunatakiwa tuhakikishe zile pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati, zikiendelea kuchelewa zitaendelea kuwapa matatizo wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, eneo la kilimo ni eneo very sensitive, Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Kilimo, benki hii ya kilimo ilianza miaka mitatu iliyopita, na tulikubaliana kwamba, benki hii ianze kwa mtaji wa shilingi bilioni 100, lakini jambo la kusikitisha mpaka leo benki hii ya kilimo imepewa shilingi bilioni 60 wanashindwa kumudu na wanashindwa kuwasaidia wakulima.
Hivyo, tunaomba benki hii iongezewe mtaji na kama tulivyokubaliana kila mwaka benki hii ya kilimo iendelee kupata mtaji.
Mheshimwia Mwenyekiti, kwa kifupi bilioni 60 hazitoshi! Tunaomba benki hii isiwepo Dar es Salam tu, iende hadi kwenye site ambako wakulima wapo. Itakuwa bora kama benki hii ya kilimo itakuwepo kwenye mikoa haswa ya kilimo na iwafikie wananchi, utaratibu wa kupata mikopo uwekwe uwe wazi na wananchi wajue ni haki yao kupata mikopo ya riba nafuu. Tukifanya vizuri kwenye eneo hili kama nilivyosema awamu ya pili ya mpango tutakwenda tukiwa kifua mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuchangia kidogo ni kuhusu mfumuko wa bei. Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia sana mfumuko wa bei na jana Waziri wa fedha alizungumzia mfumuko wa bei. Lakini Waziri wa Fedha jana alizungumza jambo moja kwamba, tukidhibiti eneo la mafuta tutakuwa kwenye hali nzuri ya kuzui mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa mfumuko wa bei unasababishwa na mambo makubwa mawili, la kwanza Cost Push Inflation na la pili Demand Pull Inflation. Tunapozungumzia Cost Push Inflation ni kweli kwenye eneo la mafuta tunaweza tukawa kwenye eneo hili, lakini hatuwezi kuzungumzia eneo la mafuta peke yake bila kuzungumzia umeme, kama tuta- control bei ya umeme itakuwa iko chini na umeme utapatikana kwa wakati, automatically utapunguza cost of production.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuishii kwenye jambo hilo tu, vilevile nilitaka tuzungumzie suala la infrastructure kwa maana miundombinu kama tuna uhakika na miundombinu mizuri automatically tutakuwa tumefanya vizuri. Kwa namna ya kipekee naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwenye suala la Demand Pull Inflation Serikali iko vizuri na Watanzania tumekuwa tuna chakula kingi na hatuagizi nje ya nchi. Kwa hiyo katika jambo hili tuko vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo huwa tunalipigia sana kelele hapa suala la dollarization lakini Serikali imekuwa siyo sikivu haisikii kwenye jambo hili. Tunaomba hawa watu ambao wanaendeleza utaratibu wa dollarization kwa njia moja au nyingine ina-affect uchumi wa nchi hii, thamani ya shilingi automatically inapoteza mwelekeo kutokana na dollarization.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekisoma kitabu cha Waziri Mkuu, nimeona haikuzungumzia kabisa suala la uvuvi. Tunatakiwa tuwekeze kwenye eneo la uvuvi, eneo la uvuvi ni eneo muhimu ambalo tunawekeza mara moja na baada ya kuwekeza nina hakika tutakuwa tume-create ajira za kutosha, vijana wengi wanaweza kujiajiri katika eneo hili na tukapata mtaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tuwe waangalifu na tunatakiwa tuwe waangalifu na tuwekeze hasa kwenye bahari kuu ili kusudi tuweze kupata mitaji mikubwa. Kuna baadhi ya nchi hapa duniani kama Sychelles zinaishi kwa uvuvi na sisi hatuna sababu ya kutokupata mapato makubwa kwenye eneo la uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ninayotaka kuzungumzia ni kuhusu suala la maji. Maji ni muhimu sana kwa maisha ya Mtanzania na kwa masikitiko makubwa katika Jimbo langu ambalo lina Kata 11 maji ni tatizo, sina hata Kata moja ninayoweza kuzungumzia suala la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wetu ile senti 50 ambayo imeingizwa kwenye tozo ya mafuta ingeongezwa ikawa shilingi 100 badala ya shilingi 50 kusudi tuweze kupata maji katika Majimbo mengi na katika maeneo mengi. Tunaiomba Serikali inapoleta bajeti kwenye eneo la maji tuongeze hatuna sababu ya kutochangia kwenye eneo la mafuta badala ya shilingi 50 tuweke shilingi 100 ili mfuko wa maji uendelee kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la miundombinu. Ili tuone uchumi unakua vizuri ni vema tukahakikisha miundombinu yetu ni ya uhakika. Katika eneo langu lina matatizo katika barabara ya Mapanda, Usokami, Ihalimba na Kinyanambo, barabara ya Mtili, Ifwagi, Mdabulo na Ihanu. Tumewaandikia wenzetu wa TAMISEMI kwa vile hivi sasa barabara zile hazipitiki, tumewaandikia kwenye mfuko wa emergency watusaidie katika eneo hili. Wakitusaidia nina uhakika kabisa tunafanya vizuri katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la nishati. Tunazungumzia sana sasa hivi nishati ya gesi, tumesahau habari ya makaa ya mawe. Makaa ya mawe ni muhimu sana, ukiangalia wenzetu wa South Africa asilimia 57 ya umeme unatokana na makaa ya mawe. Sisi hatuna sababu ya kutokuwekeza kwenye makaa ya mawe, tulitakiwa tujenge transmission line kutoka Makambako kwenda Songea mpaka Mbinga ambayo gharama yake ilikuwa shilingi bilioni 60 na wenzetu wa SIDA walishakubali kutusaidia kwenye eneo hili. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba Serikali inasuasua kwenye eneo hili! Kuna uwezekano wa ku-produce megawati 120 kwenye kilowati 210.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivyo kwenye eneo hili tutakuwa tunawaonea watu wanaotoka kwenye maeneo hayo.