Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuniwezesha na mimi kuweza kutoa mchango wangu kwenye hoja iliyo mbele yetu. Naomba nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, kwa mawasilisho yake mazuri sana aliyoyafanya kwenye hotuba yake. (Makofi)

Vilevile kuwasilisha hotuba nzuri ina maana hotuba hii ilitayarishwa na timu ya wataalam wenye weredi mkubwa sana, napenda nichukue nafasi hii, kumpongeza Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na wataalam wote kwenye Wizara hii kubwa ambao wamewezesha kutengeneza hotuba nzuri kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuipongeza na kuishukuru Serikali hii ya awamu ya tano ambayo kwa makusudi mazima imeamua kuwekeza karibuni asilimia 40 ya bajeti yetu kwenye miundombinu. Ukiwekeza kwenye miundombinu sawasawa na kuweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, kwa sababu miundombinu inachochea maendeleo na uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba nije kwenye barabara yangu ya Mbeya - Chunya - Makongorosi. Napenda nimfahamishe Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye anaifahamu sana hii barabara. Kwanza ninamsifu sana ametoka Mbeya mpaka Itigi anaikagua barabara. Hii barabara zamani ndiyo ilikuwa njia ya The Great North Road inayotoka Cape kwenda Cairo, ilipita Chunya, Itigi ikaja Manyoni kwenda Arusha - Nairobi mpaka Cairo. Serikali kwenye miaka ya 1960, 1961, 1962 ndio waliibadilisha route hiyo ya Great North Road kwa kutumia GN kwa kuifanya itoke Mbeya - Iringa - Dodoma - Babati kwenda Cairo, lakini originaly ilikuwa ni hiyo ya Chunya, Itigi, ndiyo hii The Great North Road kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakusifu sana umeikagua unaifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali imejenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Mbeya mpaka Chunya, kilometa 72 tunawashukuru sana wananchi wa Chunya, mmetupunguzia sana matatizo. Sasa hivi kutoka Mbeya kwenda Chunya ni shilingi 3,500 au 4,000 ambapo ilikuwa shilingi 10,000 au shilingi 12,000 sasa hivi mazao tunayolima Chunya yanafika haraka kwenye masoko, kwa hiyo mimi napenda kuishukuru sana Serikali kwa jambo hili kubwa ambalo wamelifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka huu Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 22 barabara hii kujengwa kwa lami kutoka Chunya kwenda Makongorosi hadi Mkola kilometa kama 42. Kwenye kitabu chake nimeiona na ninajua kwa sababu niko karibu sana na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, tender imetangazwa sasa hivi wako kwenye evaluation, najua ujenzi utaanza siku za karibuni, ninawawashukuru sana. Naomba barabara hii ambayo ni ya muhimu sana tuiendeleze mpaka ifike huko inakohitajika kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona vilevile kwenye kitabu kwamba, barabara hii hii kwa mwaka huu inaanza kujengwa kutoka Mkiwa kwenda Itigi ili mwaka ujao itoke Itigi kuja tukutane katikati na Mheshimiwa Massare, kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wa Chunya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niongelee barabara ndogo ambayo inatoka kijiji cha Kiwanja inakwenda kwenye kijiji cha Mjele kwenye Mkoa mpya wa Songwe, Wilaya mpya ya Songwe Barabara hii inashughulikiwa na Halmashauri ya Chunya, lakini kwa kuwa sasa hivi Mkoa wa Songwe ni Mkoa mpya na Chunya iko Mkoa wa Mbeya kwa hiyo hii barabara inaunganisha mikoa miwili, inaunganisha Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, naomba Serikali na Wizara muichukue barabara hii iweze kushughulikiwa na TANROADS badala ya kushughulikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kidogo kwenye hii hii barabara ya Mbeya - Chunya - Makongorosi. Barabara hii ina matatizo makubwa mawili, naleta kilio kwako Mheshimiwa Waziri. Tatizo la kwanza barabara hii baada ya kujengwa kilometa 72 ukipita sasa hivi kama ulivyoona ulivyopita kumeanza kuonekana matobo mawili, matatu, manne; kwa barabara ambayo haijamaliza hata miaka mitano siyo vizuri, haina afya hii. Kwa hiyo, naomba sasa hivi mnavyofanya evaluation kwa kuiendeleza barabara hii kutoka Chunya kwenda Makongorosi na Mkola, kandarasi ambaye alijenga huku nyuma ambaye hata miaka mitano haijapita mashimo yanaonekana asipewe kazi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili hili labda tungechukua mfano wa barabara ambayo inajengwa na Serikali kutoka Ruaha ambayo sasa hivi imefika mpaka Mafinga imekwenda Igawa, barabara imejengwa kwa kiwango cha juu sana. Labda wakandarasi wengine wa barabara hapa nchini wangekwenda kujifunza kwa mkandarasi huyu anayejenga barabara kutoka Ruaha kwenda mpaka Igawa kwenda mpaka Tunduma. Kwa hiyo hilo ni tatizo la kwanza, kwamba kumeanza kujitokeza mashimo madogo madogo, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri na viongozi wako mlielewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la pili, Chunya tunalima tumbaku, sasa wasafirishaji wa tumbaku wanaobeba tumbaku kutoka Chunya kuleta Morogoro kutoka Chunya kuja Mbeya wanapakia malori ya rumbesa kwa sababu wanajua kwamba kule sijui hakuna mizani; wanapakia malori ya rumbesa ili akifika Mbeya ndipo anagawa hilo lori yanakuwa malori mawili. Sasa hiyo rumbesa inaiumiza sana barabara ya lami ambayo mmetujengea inaumizwa vibaya sana. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri nipewe hata weighbridge moja au mbili hata mobile weighbridges ili tuweze kuilinda hii barabara, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongee kidogo kuhusu uwanja wa Songwe. Naishukuru Serikali kwa awamu zilizopita na awamu hii, mmejenga uwanja wa ndege wa Songwe ambao unainua sana uchumi wa Mikoa ya nyanda za juu Kusini; Mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Katavi, Rukwa, majirani wa Zambia wa Congo tunatumia uwanja wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona hapa karibuni wakati wa masika huu, ndege zinatoka Dar es Salaam kufika Songwe kama kuna ukungu zinashindwa kutua, kwa hiyo naomba katika hii bajeti tunayoimalizia mwaka huu, Serikali iweke taa kwenye uwanja huo ili madhumuni ya Serikali ambayo ilikuwa imepanga kwa ajili ya uwanja huu yaweze kutimia. Vilevile naomba Serikali imalizie jengo la abiria kwenye uwanja wa Songwe, naomba tafadhali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee reli ya TAZARA, reli ya Uhuru ambayo walijenga Waasisi wa Taifa hili. Serikali inafanya jambo jema sana kuwekeza kwenye miundombinu, kutengeneza bandari, kujenga reli ya kati kwa standard gauge, bandari za Mtwara, Dar es Salaam, Tanga Serikali inawekeza ili iweze kuvuna kwenye uchumi wa jiografia wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hatuwezi kukamilisha jambo hili kama tutaelekeza tu kwenye reli ya kati na bandari zile basi bila kuingalia reli ya uhuru. Reli ya uhuru yenyewe haihitaji kujengwa, reli ya uhuru inahitaji kukarabatiwa kidogo ifanye kazi, nadhani ni sheria ambazo zimeiweka reli ya uhuru. Naomba Serikali ishirikiane na Serikali ya Zambia tuangalie sheria hizo ni sheria gani ambazo zinaikwamisha reli hii bila sababu, ili bandari zikikamilika, reli ya kati ikikamilika na reli ya uhuru ikikamilika nchi iweze kuvuna kutumia uchumi wa jiografia ambao Mungu ametuwezesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye reli ya kati zimeanza block trains ambazo zinabeba mizigo inayokwenda Isaka au inayokwenda Burundi au Rwanda na reli ya TAZARA nayo ingeweza kufanya hivyo, tungeweza kufanya bandari kavu ikawa Mbeya au Makambako au Tunduma tukawa tunatoa block trains kwenda Dar es Salaam, Tunduma, Mbeya au Makambako. Naomba sana, tunapotaka kuboresha miundombinu ya kutumia uchumi wa Jiografia wa nchi hii basi tuiangalie na reli ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa barabara ya mchepuko (bypass), Mheshimiwa Mwanjelwa aliiongelea jana; ya kutoka Uyole kwenda Mbalizi. Sasa hivi congestion ni kubwa mno kutoka Uyole kwenda Mbeya Mjini na kuelekea Mbalizi. Barabara ni ndogo, ni ya siku nyingi, biashara ni kubwa mno, fursa ziko nyingi sana za biashara kwenye Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo, hii hadithi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina kila mwaka, naomba barabara hii ya bypass iweze kujengwa ili tuweze kuuokoa Mkoa wa Mbeya kwa uchumi ambao unaweza kudidimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja.