Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nataka kuchangia kidogo kuhusiana na miundombinu katika Mkoa wa Katavi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Pia naunga mkono asilimia 100 hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nataka nijikite zaidi katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza kabla sijaenda mbali zaidi, ukisoma katika ukurasa wa 22 na 19, nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri; barabara ya kutoka Mpanda
- Stalike, barabara ile imekwisha, lakini ukisoma kwenye hotuba ya Waziri ametenga shilingi bilioni 4.1. Sasa pesa hizi ametenga kwa ajili ya ujenzi wa kitu gani? Ukisoma, mradi umekamilika. Nadhani atakapokuja kuhitimisha anieleze hii shilingi bilioni 4.1 ni ya nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna madaraja mengi katika Mkoa wa Katavi ambayo yamekuwa yanasuasua kwisha na watu wa Katavi wanaendelea kupata shida, hawana mawasiliano kutoka kwenye Wilaya moja kwenda kwenye Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna daraja la Iteka ambalo liko katika Halmashauri ya Nsimbo, daraja hili karibu kila mwaka limekuwa likiua watu, magari yanakwama, watu wanalala njiani, lakini katika bajeti hii sijaona popote daraja hili limetajwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Kibaoni – Mpanda; barabara hii imechukua muda mrefu sana. Watu wa Katavi wanahangaika, lakini muda mwingine wanasafiri zaidi ya masaa 12 kutoka Mpanda mpaka Sumbawanga, lakini katika bajeti hii sijaona kokote ambako Mheshimiwa Waziri ametenga bajeti kwa ajili ya kumaliza hizi barabara. Sasa sielewi ni nini mkakati wa Serikali; ni aidha kuendelea kuwatesa na kuwanyanyasa watu wa Katavi? Kwa sababu ukiangalia kwenye mikoa mingine, kwa mfano, Mkoa wa Bukoba pamoja na Pwani wametengewa zaidi ya
shilingi bilioni mbili kwa ajili ya matengenezo tu ya kawaida; lakini Mkoa wa Katavi leo hii tunaongea mnatutengea shilingi milioni 27! Za nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nijikite katika suala la mawasiliano. Wakazi wa Katavi ni watu ambao wanatangatanga, wanapata shida. Mawasiliano ni ya hovyo, barabara ni mbovu, sasa Mheshimiwa Waziri, kuna wakazi wa Kata ya Ilunde iko katika Jimbo la Mheshimiwa Engineer Waziri wa Maji; Kata ile watu wanasafiri kilometa 10 mpaka 15 kwenda kutafuta network ili awasiliane na mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Serikali gani hii ambayo mpaka leo mtu anasafiri, anatembea kilometa 10, anatembea kilometa 15 kwenda kutafuta network na network yenyewe inakuwa ni mbovu, mtu mpaka apande kwenye mti ndiyo awasiliane! Hatutakubali watu wa Katavi. Kwanza nashangaa kwa nini watu wa Katavi bado wanaendelea kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya kutoka Tabora - Sikonge kwenda mpaka Katavi. Barabara hii imechukua muda mrefu sana, mpaka sasa Wakandarasi haijulikani, kila siku wanaweka tu changarawe, wanarekebisha na ma-grader, ukipita, watu wanalala njiani lakini pia kuna Mto Koga ambao miaka mwili iliyopita kuna zaidi ya watu 30 walikufa katika mto ule, lakini ile barabara mnayotuletea ni marekebisho tu. Kimsingi, hamko serious na Mkoa wa Katavi. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini hawakutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa Mkoa wa Katavi? Wanayotuletea ni marekebisho tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kushangaza, ukisoma kwenye ukurasa wa 285 anasema; barabara hizi zitatumia kwa ajili ya marekebisho shilingi milioni 846 kwa kilometa 695.5. Ukigawanya shilingi milioni 846 kwa kilometa 695.5, katika hizi barabara zaidi ya saba zilizotengewa kwa ajili ya marekebisho, kila barabara yenye urefu wa kilometa 112, barabara ya kutoka Mamba – Kasansa; barabara ya kutoka Mpanda – Ugala; barabara ya kutoka Mnyamasu kwenda Ugala; zina zaidi ya kilometa 111; na nyingine, hii barabara ya kutoka Kagwira kwenda mpaka Karema ni kilometa 250.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu nadhani ni utani, unawezaje kufanya marekebisho kwa barabara yenye urefu wa kilometa 250 kwa shilingi milioni moja? Huu ni utani na hatuwezi kukubali kwa sababu kuna mikoa ambayo inapewa vipaumbele na Mkoa wa Katavi ukiendelea kuwekwa nyuma wakati ndiyo mkoa ambao unaoongoza kwa kuzalisha mazao ya chakula ambayo Waheshimiwa humu ndani wanatumia vyakula hivyo. Sasa hatuwezi kuendelea kukaa kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie pia kidogo kuhusiana na ujenzi wa uwanja wa ndege. Mwaka 2010, Serikali ilitenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege katika Mkoa wa Katavi, katika Manispaa ya Mpanda, lakini mpaka hivi tunavyoongea, wakazi wale hawajalipwa na wengine wakati wanalipwa zile pesa kwa jili ya kupisha ujenzi wa ule uwanja, watu walilipwa sh. 75,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ambaye alikuwa ana nyumba, ana kiwanja unaenda kumlipa sh. 75,000/=! Mpaka leo ninavyoongea kuna wananchi ambao wanalala kwenye mahema na wako mjini katika Kata ya Ilembo; pia kuna Kata ya Airtel ambayo wakazi wake wengi walitolewa kwenye lile eneo ambalo uwanja ulijengwa. Sasa watu hawa hawawezi kuendelea kusubiri huruma ya Serikali. Viwanja vilikuwa ni vya kwao na walikuwa wamejenga nyumba, sasa waliamua tu kupisha ujenzi huo.
MHeshimiwa Naibu Spika, pia wakazi wa Mpanda hawakuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya Uwanja wa Ndege, kwa sababu majority ya watu wa Katavi wanatumia usafiri wa reli ambapo usafiri wa reli wenyewe ni wa hovyo, barabara ni mbovu, mnaenda kuwapelekea Uwanja wa Ndege ambao mpaka sasa wanapanda watu wawili, watatu kwenye vindege vile vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kufahamu, hii TTCL ina faida gani? Sioni faida ya TTCL kwa sababu ukiangalia Hallotel wamekuja juzi tu, lakini leo wanafanya vizuri. Sasa labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, atueleze faida ya TTCL ni nini? Kuna haja gani ya kuendelea kuitengea bajeti TTCL?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu sasa, Wizara ina mkakati gani wa kuongeza pesa katika Mfuko wa Barabara kwa Mkoa wa Katavi? Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachoendelea hapa. Ukisoma kwenye ukurasa wa 287, hakuna bajeti yoyote iliyotengwa kwa ajili ya Mkoa wa Katavi. Sasa wakazi wa Katavi wataendelea kusubiri miradi ambayo haikamiliki kwa wakati, lakini ni miradi ambayo inawafanya watu wa Katavi waendelee kudanganywa kwamba mtaletewa barabara, mtatengenezewa standard gauge kwa ajili ya watu ambao wanasafiri kwa njia ya reli, hakuna chochote! Mtaendelea kuwadanganya mpaka lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitaji majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini sasa wakazi wa Mkoa wa Katavi wataacha kusafiri siku mbili mpaka tatu kulala njiani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kufahamu, ni kigezo gani ambacho kinatumika kwa ajili ya kuwapata wakandarasi… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.