Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nianze kwa kukushukuru wewe kwa nafasi hii, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote pamoja na taasisi chini ya Wizara kwa kweli kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Kuna msemo mmoja wa Kiswahili unasema ukiona adui yako anakupongeza kwa jambo lako, achana nalo; lakini ukiona adui yako kwa jambo lako anakupigia makofi, jitazame mara mbili. Kwa hiyo, wenzetu kila jambo jema linalofanywa wao hawakubali. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa yale mazuri ambayo mnayafanya na ni mengi tu, kazeni buti, endeleeni, wala msitishwe na hizo kelele ambazo zinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri, najua amevaa kiatu cha Mheshimiwa Rais kwa sababu Mheshimiwa Rais ndiye alikuwa Waziri wa Ujenzi; na kiatu hicho naona kinakufaa sana. Naomba, ipo barabara ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutoka Isandula - Magu inakwenda Bukwimba - Ngudu kwenda Hungumarwa. Ni ahadi! Mwaka 2016 mlisema kwamba mmetenga pesa kwa ajili ya usanifu, sasa leo sijaona humu, nami kama Senator hatupendi sana kupiga makelele na hasa ukizingatia kwamba Mheshimiwa Waziri wa Wizara ni mtu msikivu na mwelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne akiwa na Rais wa Awamu ya Tano, walikuja kufungua Daraja la Mto Simiyu, Maligisu. Vingunge wote wa Wizara walifika pale Maligisu na Mheshimiwa Rais aliahidi


kwamba ile approach ya mita 50 upande huu na mita 50 upande huu itajengwa kwa kiwango cha lami. Tena kama natania, ili na fisi nao waje wapite kwenye lami. Hiyo ilikuwa mwaka 2015. Mheshimiwa Waziri, maagizo ya Mheshimiwa Rais, mita hamsini hamsini, hebu tusimwangushe Mheshimiwa Rais. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa, Mheshimiwa Waziri, anazo taasisi zaidi ya 30 zilizo chini yake. Taasisi hizi ni kioo kwa nchi yetu na Taasisi hizi ni uchumi kwa nchi yetu. Nawaomba kwa sababu bahati nzuri ma-CEO wapo hapa, Wakurugenzi wapo kwa maana ya Wenyeviti. Kwa taasisi hizi, kila CEO, Mwenyekiti kwenye eneo lake kwa ajili ya kuisaidia Serikali na kwa sababu tunaomba pesa nyingi, pesa hizi tunazitegemea kutoka kwenye hizi taasisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana viongozi hawa, yale makubaliano ambayo inawezekana Mheshimiwa Waziri tutaweka na utaratibu mmoja mzuri, nafikiri wa kupimana, kwa sababu ile business as usual, tukienda na utaratibu huo kwa taasisi zetu hizi, tunaweza tukafika mahali tukashindwa kufikia yale malengo. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na viongozi wa taasisi zilizo chini yako, zifanye kazi ili kusudi matokeo makubwa tuyaone kwa kuisaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, namwomba Mheshimiwa Waziri upande wa Wakala kwa Mama Kijazi pale, TMA. Eneo hili ni eneo zuri sana kama watapatiwa vifaa na wataalam wa kutosha. TMA hii igawanyike kikanda; Kanda ya Ziwa, (mimi nazungumzia Kanda ya Ziwa, huku kwingine baadaye) ili kusudi waweze kutambua na kuwashauri wakulima, maana yake sasa hivi kuna ubashiri, lakini tutoke kwenye ubashiri tusogee kwenye uhalisia kwamba mvua zitanyesha kesho saa fulani. Jamani wale wavuvi kesho kutwa msiende ziwani kwa sababu kuna


upepo mkali. Sasa ili wafanye hivyo ni lazima wawe na vifaa vya kutosha vinavyoweza kuhimili badala ya kwenda kupiga ramli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, barabara ya Nyanguge - Musoma, Mwanza -Shinyanga Boarder tumekuwa tukizitengea pesa nyingi kila mwaka. Hivi hakuna utaratibu mzuri wa kuzifumua hizo barabara zikajengwa upya? Maana yake kila mwaka fedha inatengwa. Namshauri Mheshimiwa Waziri, hebu walitazame hili kusudi barabara zetu hizi ambazo kiuchumi na kijamii zina faida kubwa sana kwa Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nashukuru tunatengeneza hii reli ya kati. Sasa nasikia na namwomba CEO wa TRL, kama treni itatoka Dar es Salaam lakini inakuja Shinyanga, inafika Malampaka, halafu haisimami katikati hapa pote inakwenda kusimama Mwanza; nashauri treni hii isimame Bukwimba Stesheni, panajulikana! Panaeleweka! Kadogosa; siwezi kusema Kisukuma lakini nakuomba treni isimame Bukwimba Stesheni, miundombinu ipo ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu upoteaji wa makontena. Hebu wataalam wako wakae waangalie namna nzuri zaidi; hivi NASACO, Wakala wa Meli, nasema mkae mwangalie; Wakala wa Meli wa wakati ule NASACO, tulikosea wapi? Kwa nini tuliwaondoa? Kwa sababu haiwezekani mizigo ikawa inapotea, makontena hayajulikani, yanaingia makontena na taarifa hatuna. Naomba kama inawezekana NASACO iangaliwe upya ili kusudi tuweze kurejesha heshima ya nchi yetu hasa upande wa mizigo inayokwenda nje na ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena lakini naomba kusisitiza, taasisi hizi ni kioo cha nchi yetu; TPA ni kioo na uchumi, ATCL, TRL na mengine, ni kioo kwa uchumi wa nchi yetu. Toeni huduma, fanyeni biashara lakini kwa manufaa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja.