Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mchango wangu nitauelekeza moja kwa moja katika Shirika letu la Ndege la ATCL. Katika vipindi viwili vya 2016/2017 na mwaka 2017/2018, tumeona imetengwa karibu shilingi trioni moja kwa ajili ya ATCL ambapo kwa kila kipindi itakuwa shilingi bilioni
500. Uwekezaji huu ni mkubwa mno na unahitaji umakini wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili ATCL ipate faida, ni lazima twende sambamba na uwekezaji katika mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni uwekezaji wa ndege kama hivi tunavyofanya sasa hivi; jambo la pili ni kuwekeza katika uendeshaji wa ATCL, yaani mtaji wa kazi na rasilimali watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ndege, naomba nimpongeze sana Mhshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea ndege za kisasa na ametuhakikishia ni salama kabisa. Itakapofika mwaka 2020 kama siyo 2019 zitakuwa ndege saba. Nampongeza sana Rais wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi mkubwa unakuja kwenye uwekezaji katika uendeshaji wa ATCL. Tumezoea tukinunua tu ndege tunaacha, tunajua tayari tumeshanunua ndege bila kuwekeza. Tunategemea kupata faida, lakini hatuwezi kupata faida tu bila kuiwezesha ATCL iweze kuendesha biashara ya ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunajua kuwa ATCL ilibaki jina tu, haikuwa inafanya vizuri, ndege zake zilikuwa hazieleweki, lakini sasa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kaanza kuturudishia ATCL mpya. Vilevile haikuwa na rasilimali watu na mtaji; naongelea kwa upande wa kujiendesha. Kwa hiyo, lazima tuisaidie ATCL kujiendesha ili iwe kibiashara zaidi. Tunajua ATCL ilikuwa ni jina tu au Kampuni isiyokuwa na rasilimali watu wala chochote; tunajua kwa sasa hivi ATCL kitu ambacho inahitaji ni working capital na siyo startup cost. Ni wazi kwamba bila kuiwezesha ATCL haitaweza kujiendesha yewenye na haitaweza kujiendesha kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji uliofanywa na Serikali ni mkubwa mno, lazima uambatane na uwekezaji wa kuiendesha ATCL ili iweze kutoa huduma nzuri. Tumeanza kuona mabadiliko ya ATCL, tumeona safari hazikatishwi, tumeona inaenda vizuri sana. Vilevile naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea Mtendaji anayeweza hii nafasi, ana uzoefu. Ni muda mfupi sana naweza nikasema ametuonyesha wonders. Naomba sana tum-support Mtendaji huyu Ledislaus Matindi kwa kazi kubwa anayofanya, ana uzoefu na anajua changamoto za ATCL. Lazima tuunge juhudi za Serikali mkono na tuwe wazalendo kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Mheshimiwa Rais ameteua Bodi nzuri; lazima tuhakikishe Bodi na Menejimenti wamejikita zaidi kuisaidia ATCL ijiendeshwe kibiashara na siyo kukaa tu kusema kuwa ni Shirika la Serikali. Hatuna wasiwasi na matumizi ya fedha kwa sababu ya uongozi uliopo sasa hivi tunauamini, tunajua hata tukiwawezesha mapato yataenda vizuri, fedha zitatumika kama zilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze kwa wenzetu ambao waliweza kuendelea kama Shirika la Ndege la Ethiopia. Serikali yao iliwawezesha Ethiopia na waliendelea vizuri, ilivumilia na walijipanga vizuri. Walianza mambo yao ya ndege mwaka 1945, lakini walikuja kupata faida 1990 walikuwa wavumilivu, waliwekeza katika mishahara, matangazo na hadi sasa hivi inajiendesha kibiashara. Tusitegemee ATCL itaanza tu, tayari tupate faida asilimia 100, hapana. Lazima kama sisi Serikali kuiwezesha ili iweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio ya Ethiopia yalikuwa na uvumilivu, mkakati na nidhamu. Uvumilivu ulisaidia sana mpaka kufika 1990 ukiangalia ukiangalia kuanzia mwaka 1945, ni kipindi kirefu sana, kwa hiyo, kilihitaji uvumilivu. Nasi tukifanya hivyo, Serikali ikiwawezesha ATCL nina uhakika kabisa tutafika na tutaweza kuendelea vizuri na ATCL. Kwa hiyo, naomba Tanzania tui-support ATCL. Mpaka sasa hivi tumeona inaenda vizuri, ni muda mchache sana lakini imefanya vizuri na wote tumekubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuonyeshe uzalendo kwenye ndege zetu. Tumeona kuna ndege ndogo ambazo zinafanya safari kwenye miji mikubwa, kwenye barabara kuu ambazo zingeweza kufanya ndege zetu. Naomba pia Serikali iliangalie hili tumetumia kodi za wananchi. Ndege ndogo zinaweza kupewa trip nyingine kwenda sehemu ambazo hizi ndege zetu za ATCL haziwezi zikafika. Zenyewe zikaenda zikawaachia njia ATCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona kuna tabia moja kuwa ndege inapokuwa na nguvu kuna baadhi ya ndege zinakuja zinawakwamisha, zinaua kabisa. Tumeona ndege tayari ambazo tayari zilikuwa zinafanya vizuri zimekufa, lakini tusikubali hili kwa ndege zetu ambazo zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi. Tumeona ATCL inaweza ikaenda Mwanza labda kwa kiasi fulani lakini ndege nyingine ikaenda ikashusha kabisa. Hao ndio wauaji wakuu wa soko letu, Watanzania tusikubali, tuwe wazalendo wa nchi yetu. Mheshimiwa Waziri naomba uje unijibu wakati unajibu hili la ndege nyingine kuja kutuharibia biashara huku tukijua tunatumia kodi za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tusipokuwa makini tunaweza tukajikuta ATCL inakufa, tukaishia kwenye madeni yasiyolipika. Kwa hiyo, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais na nia yake nzuri ya kufufua Shirika letu la ndege ili lije kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie na uwanja wangu wa Ndege wa Arusha Airport. Kiwanja cha Ndege cha Arusha Airport, njia ya kurukia ni fupi, hali inayopelekea ndege za kati na kubwa kushindwa kutua, ikiwemo ATCL, inashindwa kuruka. Kwa hiyo, inabidi wakatize trip za kwenda Arusha. Ukizingatia Arusha ni Jiji lenye biashara, Jiji la utalii, ni kitovu cha utalii ambapo tungeweza kuiingizia Serikali mapato mengi sana kutokana na utalii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati ananijibu, naomba aniambie ana mpango gani na Kiwanja cha Ndege cha Kisongo cha Arusha ili nasi wana-Arusha tuweze kupata hizo ndege tuweze kuiingizia Serikali mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba Waziri aniambie ameandaa kiasi gani cha uwekezaji kama mtaji na rasilimali watu kuwekeza kwa ajili ya ATCL iweze kujiendesha yenyewe kibiashara? Siyo kuwekeza tu kwenye ndege tukasahau kuwa inahitaji na yenyewe kujiwekeza? Ahsante sana.