Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii asubuhi hii ya leo ili nichangie hoja iliyoko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa wasilisho lake zuri. Naelewa nyuma ya wasilisho hilo ni kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa Wizara hiyo pamoja na taasisi ambazo zipo chini ya Wizara hiyo. Hongereni sana kwa kazi nzuri, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, niungane tu na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wa hekima na busara lakini wa kijasiri sana kuhusiana na reli ya Kati. Uamuzi huu ni wa msingi sana katika kufungua fursa mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika,Naendelea kuiomba Serikali iendelee kuweka kipaumbele cha juu katika upatikanaji wa fedha za ujenzi wa reli hii kwa sababu wenzetu wa Northern Corridor wako mbali sana na shughuli hii. Kwa hiyo, nami naiomba sana Serikali twende nalo lakini naipongeza sana Serikali kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye mambo ya nyumbani, politics is always local. Nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 11- 12 Januari, alitembelea Mkoa wa Simiyu hususan Bariadi Makao Makuu ya Mkoa na Maswa. Akiwa Bariadi alifanya mambo makubwa sana na ndiyo maana wananchi wa Mkoa wa Simiyu tunaendelea kumshukuru sana. Moja, Mheshimiwa Rais alizindua barabara iliyokamilika ya kutoka Lamadi mpaka Bariadi yenye kilometa 71.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, akiwa pale pale alitoa tamko kuhusiana na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Simiyu. Tatu, alimaliza ngebe kuhusiana na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria, matenki makubwa yakae wapi. Nne, alitoa maelekezo kuhusu gharama za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwamba waziangalie kwa lengo za kuzipunguza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kwenda Maswa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba ujenzi wa barabara ya kutoka Bariadi kwenda Maswa kilometa 49.7 utangazwe; na kweli naona kwenye Bajeti hii Wizara imezingatia hilo. Tukiwa Maswa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara inayoendelea sasa hivi kutoka Mwigumbi kuja Maswa. Haya ni mambo makubwa sana katika kufungua Ukanda huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Simiyu ni Mkoa mpya, Makao Makuu yake yako Bariadi. Tunahitaji tuunganishwe sisi na Mikoa jirani ya Singida na Arusha. Ndiyo maana Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatamka, tufanye Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kutoka Bariadi kwenda Kisesa - Mwandoya - Mwanhuzi mpaka Sibiti. Njia tunayoona sisi ni kupitia Mkalama kuja Iguguno. Kwa hiyo, tungependa sana hili lionekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mimi nimekuwa Mwanasheria Mkuu nikiwa Mbunge. Hii barabara ya kutoka Odeani - Mang’ola - Matala, Sibiti kwenda Mwanhuzi – Lalago – Mhunze – Kolandoto, imekuwa inaongelewa story, story, story. Kwa mwaka huu nakubaliana na Serikali kwa hayo waliyosema kwamba wamekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mwaka kesho kama ikiendelea hivi mimi nitasema, maneno waache sasa waweke muziki. Hii barabara tunataka ijengwe. Kusema kweli ukishakamilisha usanifu huo, inakuwa sehemu ya kutoka Bariadi mpaka Mwanhuzi kwa sababu sehemu nyingine umeshamaliza. Kwa hiyo, waache maneno, waweke muziki. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukishafungua ukanda huo na kwa mapendekezo mengine ambayo tumeweka, barabara za kufunguliwa Ukanda wa Mkoa wa Simiyu, tutafungua maeneo hayo kiuchumi na kijamii. Sasa nilihangaikia sana hii Sheria ya Barabara kuweka vigezo vya namna ya kupandisha madaraja barabara hizi, basi tupate angalau maamuzi kwa nchi mzima. Vigezo vipo kwenye sheria hiyo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri waliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema ya nyumbani hayo, lakini nami kama Kiongozi wa Kitaifa niseme. Nchi hii ya Tanzania inafunguka kwa barabara. Angalia hizi barabara za kikanda, maeneo yote kuunganisha Tanzania na nchi jirani tumefanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi jirani sehemu ambayo naiona ni muhimu kwetu sana na nimeiona kwa mbali kwenye hotuba hii ni Kasulu – Kibondo – Manyovu na Burundi. Pia naiona kwa mbali Sumbawanga – Matai – Kisesya – Sanga Port ni muhimu sana. Naiona kwa mbali pia, Bagamoyo – Saadani – Tanga – Horohoro – Lungalunga – Mombasa – Nairobi – Isiyolo – Moyale – South Ethiopia. Haya ndiyo mawazo tumekuwa nayo, maana upande wa Uganda - Sudan ya Kusini Arua - kuja mpaka Kyaka tayari tunaendelea. Tukikamilisha kazi inayoendelea ya kutoka Nyakanazi – Kakonko – Kasulu mpaka Kigoma na tukashuka sasa kutoka Uvinza tukaelekea Mpanda - Stalike twende mpaka Kithi – Sumbawanga – Laela – Kikana – Tunduma unaiona nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimesafiri, namwelewa rafiki yangu Mheshimiwa Zuberi aliyoyasema, lakini nimeona humu, kutoka Masasi tukijenga barabara Masasi pale Nachingwea unaenda Nanganga, halafu Nanganga unaweza kushuka hivi kwenda Ruangwa. Haya ndiyo tunataka kuyaona humu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesafiri juzi pia, sikuamini, nimetoka Masasi nikaelekea Mtambaswala, Mangaka kule nikatoka pale nikarudi kutoka Mangaka nikaelekea Tunduru, barabara safi. Tukatoka pale tumekwenda mpaka Tunduru mpaka Namtumbo, Songea. Safi! Songea unakwenda mpaka Mbinga, sasa tunabaki sehemu ya Mbinga kwenda Mbamba Bay. Jamani, mambo yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo naitaka sana na nimeona kwa mbali, tukifungua Ukanda wa Kusini kwa chakula, angalieni ukitoka Kidatu uje Ifakara, piga hilo Lupilo uende mpaka Malinyi - Londo unakuja Lumecha, Songea, unafungua yote. Ni ukanda tajiri sana. Tukiyafanya hayo tutakuwa tumeisaidia sana nchi hii. Naiona Tanzania ikifunguka. Kwa sababu ya muda, siwezi kuyasemea yanayoendelea Ukanda wa juu wa kwetu kule, lakini yamo kwenye taarifa hii. Naishukuru sana Serikali kwa kazi hii wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa reli ya kati, kwa sababu tunatafuta mzigo utakaoweza kulipa reli hii, nadhani tuje tuiangalie kutoka Isaka kwenda Keza – Kigali - Msongoti. Pia Kaliua – Mpanda – Karema, maana mzigo wa DRC kwa Ziwa Tanganyika tungependa sana tuubebe huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sipendi kupigiwa kengele, Mheshimiwa Waziri akinisaidia; aah, nimalizie, sehemu moja ambayo nataka tuangalie pia, kutoka Mpemba pale kwenda Isongole upande wa Malawi tutakuwa tumekamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa hayo.