Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii niongee machache kwa kutoa ufafanuzi kwenye hoja za msingi na nzuri ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Kwa kuwa huu ndiyo mwanzo wa mjadala wetu wa Bunge la Bajeti basi tutakuwa na fursa zaidi ya mara moja, ya kuendelea kueleza yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaleta na kwa sasa tu niwashukuru sana wale ambao wameongelea suala la utalii ambalo nitalitolea ufafanuzi kidogo katika mawasilisho yangu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge walioongelea juu ya sekta yetu wako kumi na wengi wao waliongea juu ya Utalii kama ambavyo nilisema. Jana Mheshimiwa Mbunge mmoja alitupa takwimu kidogo, ni kweli kwamba mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wetu ni mkubwa na unafikia asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na inachangia asimilia 25 au robo nzima ya mapato yote, hii inatokana na watalii 2,200,000 ambao wanakuja kwetu sasa. Hii ni takwimu ambayo ilifikiwa mwaka 2014 na ninategemea sasa hivi tunakokotoa tumefika karibu mwisho wa kukokotoa idadi ya watalii waliokuja mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe ufafanuzi kidogo kwamba mwaka 2010 ni kweli walikuja watalii 800,000 na wale waliohesabiwa mwaka 2014 walikuwa hao 1,200,000 na kwamba kulikuwa na ongezeko hapo karibu watalii 500,000 katika kipindi hicho. Siyo kwamba, katika miaka hiyo watalii waliokuja ni hao 500,000 gawanya kwa sita au 89,000 kama ilivyosemwa. Maana yake ni kwamba hao 89,000 ni wale wanaongezeka kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kutoka 500,000 mwaka 2006, wakafikia 800,000 mwaka 2010, laki tisa, milioni moja, milioni 1.2 ni ongezeko na hiyo 900,000 ni kwa mwaka. Tofauti kati ya milioni 1.2 na 800,000 ile ndiyo ongezeko lililotokea katika kipindi hicho, siyo kwamba katika mwaka mzima waliingia wale ambao wameongezeka tu, hata kidogo!
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba fursa zetu za utalii ni nyingi na kwamba watalii ambao wanakuja hao milioni 1.2 ni wachache sana. Lakini katika uchache wao ndiyo waliochangia robo ya mapato yetu yote ya kigeni hapa nchini. Kwa hiyo, tuna lengo la kuongeza mapato haya kutoka bilioni 2.3 ya sasa na kuyafikisha bilioni tano mwaka 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka huu tataanza mpango kabambe kabisa wa kutangaza kwenye masoko ya ndani na yale ambayo yanatuletea watalii wengi katika nchi yetu. Tutatangaza Marekani ndiyo nchi ya kwanza kutuletea watalii, mwaka 2014 ilileta watalii karibu 500,000, tutatangaza Uingereza, Jamhuri ya Muungano wa Kijerumani, (Federal Republic of Germany), Italia na nchi zile ambazo zinatuletea watalii wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tuna lengo la kushirikiana na United Arab Emirates ili watalii wale wanaofika Dubai milioni 27 kwa mwaka, angalau milioni tatu waweze kuja Tanzania kama sehemu ya safari yao kule Dubai. Kwa hiyo, kuongeza watalii wetu kwa idadi hiyo na tunaamini kabisa kwamba baada ya mipango hii kutekelezwa tutakuwa tumefikia mapato ya dola za Kimarekani bilioni tano kwa mwaka na kuongeza idadi ya Watanzania walioajiriwa katika utalii moja kwa moja 500,000 mpaka wafike milioni 1.2 na wale ambao wanaohudumia utalii kutoka milioni moja kufika milioni mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, sekta hii ni muhimu sana na sisi wenyewe tumejiandaa kwa kuyalinda haya mapori ambao ni nje ya TANAPA na nje ya Mamlaka ya Ngorongoro kwa kuanzisha mamlaka mpya inaitwa Tanzania Wildlife Authority. Italinda mapori tengefu, italinda game reserves na italinda na maeneo ambayo yako wazi ili kuhakikisha kwamba wanyama katika maeneo hayo wanatumika kwa faida ya Taifa.
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Waziri!
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana ndugu zangu baada ya hutuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kujadiliwa basi, tutaendelea kutoa ufafanuzi. Mimi naunga sana mkono hoja hii, ahsante sana!