Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Joyce John Mukya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. JOYCE Y. MUKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo mbalimbali katika hotuba hii ya bajeti ya 2017/2018 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mazingira kwa mimi, ninavyofahamu au kutafsiri ni afya kwa maono ya kwamba mazingira yakiwa machafu yataathiri afya za binadamu, wanyama au viumbe hai chochote ikiwemo mimea. Kwa hiyo, naomba sana Wizara hii ipewe kipaumbele, kiuchumi kwani ndio Wizara inayolinda maisha na afya ya viumbe hai moja kwa moja na kama mazingira hayataangaliwa basi afya na viumbe hai zitakuwa hatarini wakati wowote. Matokeo yake ni kuhatarisha uhai wa viumbe hai kupitia magonjwa na upungufu wa virutubisho mbalimbali na hatimaye hata kuwasababishia vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyoelewa wanyama, mimea tunashirikiana katika mambo mbalimbali ili kuweza kuishi mfano katika hewa ya oxygen na carbondixide. Hivyo basi, ni dhahiri mazingira ni kitu muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimea vamizi, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana katika maeneo mbalimbali ndani na hasa katika maeneo ambayo kuna mifugo na wanyama ambao wamekuwa wakitegemea majani, kama chakula. Mfano katika eneo la Ngorongoro kumekuwa na mimea vamizi sana na ambayo inakuwa kwa kasi sana siku hadi siku na kusababisha wanyama kuyatenga maeneo hayo yenye mimea vamizi (invasive).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimea hii pia imekuwa ikiharibu uoto wa asili katika eneo la Ngorongoro na kuvuruga kabisa ekolojia. Ningeomba sana Serikali ichukue hatua za haraka katika kutokomeza mimea hii na kuendelea kuitunza mbuga ya Ngorongoro ili iweze kuiletea nchi yetu watalii na kuingiza fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la mimea vamizi limelikumba eneo la hifadhi ya Mlima Rungwe ambayo ni aina ya miti inayoitwa Mipaina ambayo imekuwa ni tishio kubwa katika Mlima Rungwe. Miti hii imekuwa ikisababisha upotevu wa baianowai ya Mlima Rungwe uliopo Mkoani Mbeya na kupoteza uoto wake wa asili. Kama nilivyoshauri
katika bajeti ya Waziri Mkuu wakati nimechangia kwa kuongea, naiomba tena Serikali iangalie tatizo hili kwa karibu kabisa ili kuweza kuidhibiti mimea hii vamizi na kunusuru maeneo haya yaliyovamiwa na kibaya kabisa mimea hii imekuwa ikikausua hadi vyanzo vya maji na kusababisha ukame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa ukuta wa Pangani, ujenzi wa ukuta huu uliopo katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Pangani unaelekea kutokumalizika kwa wakati kama ilivyopangwa kumalizika Novemba, 2017, kama Serikali haitapeleka fedha za ndani kiasi cha 10% walichokubali kukitoa wakati ujenzi huu unaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zingine za nje zimeshatolewa na ujenzi unaendelea vizuri katika upande wa mashariki wa ukuta huo kwani fedha za ujenzi zimetoka nje kwa wafadhili na wametoa fedha zote. Changamoto kubwa ipo katika eneo la Pangadeco na ndio eneo ambalo lina wakazi wengi ukilinganisha na eneo la mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Pangadeco ndiko wanategemea ile 10% ya fedha za ndani ambazo Machi, 2017 zilikuwa hazijatolewa hata shilingi moja. Naishauri sana Serikali ipeleke fedha hizo ambazo ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na kiasi kilichotolewa na wafadhili cha 90%, kama nilivyosema hapo mwanzo mazingira ni afya na kama hayatapewa kipaumbele yatahatarisha maisha na kusababisha vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.