Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hotuba nzuri yenye kuonesha mwelekeo wa kujali maslahi ya nchi. Katika hotuba hii nitachangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mazingira, hali ya uharibifu wa mazingira kwa sasa nchini mwetu imekuwa mbaya sana. Jamii kwa ujumla suala la mazingira imelipa mgongo, maeneo ya vyanzo vya maji shughuli za kilimo ndiyo mahali pake. Ushauri wangu shughuli za mifugo na kilimo zisiendeshwe katika maeneo hayo ili kulinda vyanzo vya maji. Pia hata shughuli za makazi kwa maana ya ujenzi wa nyumba pia upigwe marufuku, Sera na Sheria zilizopo ni nzuri, tatizo ni usimamizi wa wenye dhamana ya kusimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa mazingira kukosa rasilimali fedha kwa ajili ya kupanda miti. Napongeza uanzishwaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Mazingira, ni imani yangu maeneo ambayo yatakuwa yameathirika na mazingira yatapatiwa fedha kutoka Mfuko huo. Tusipokuwa makini vyanzo vyote vya maji vitakauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuenea kwa hali ya jangwa, maeneo mengi nchini yameshuhudia ukataji wa miti kwa matumizi ya mkaa, mbao pamoja na kuanzisha mashamba kwa shughuli za kilimo. Kasi ya ukataji wa miti imesababisha maeneo mengi kukosa mvua nchini, hali hii nchini isipodhibitiwa nchi yetu itakuwa jangwa. Mfano mzuri katika Jimbo langu la Kilindi katika Kata za Negero, Msanja, Kilindi Asilia na Kimbe, zimeshuhudia kasi ya ukataji wa miti wa hovyo huku wahusika ambao ni Watumishi katika ngazi zote wakiacha hali hii kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Taarifa ya Wanazuoni wawili wa Chuo Kikuu cha SUA Morogoro, Profesa Dhahabu na Maliado, Wilaya ya Kilindi ni eneo ambalo limeathirika sana na ukataji hovyo wa miti. Taarifa yao ni ya mwaka 2003 hadi 2012 ilionyesha eneo la Kilindi lisipochukuliwa tahadhari Wilaya yake itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria zilizopo na Watendaji katika maeneo ya Vijiji hadi Wilaya bado tatizo hili linaendelea. Nimwombe Waziri mwenye dhamana ahakikishe Timu Maalum inakwenda hasa kwenye maeneo ya Kata za Negero, Msanja, Kimbe na Kilindi Asilia na vijiji vyote kwenye maeneo ya kujionea uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuchukua jitihada kubwa na kutenga fedha za kutosha kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi tutegemee athari kubwa zaidi. Bila msisitizo wa kusimamia sheria husika na kuwa na wataalam wa kutosha tatizo halitaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Baraza la Mazingira (NEMC), Baraza hili sehemu kubwa ya shughuli zake zinafanyika mijini. Niliombe sasa Baraza litanue shughuli zake vijijini kwa kuhakikisha wanakuwa na watumishi wa kutosha. Naamini kwa dhati, shughuli nyingi za ukataji miti na shughuli za kibinadamu pamoja na ufugaji zinafanyika vijijini. Baraza lipewe uwezo mkubwa wa kisheria katika kusimamia na kuratibu misitu na kuhakikisha maeneo yetu yanalindwa. Aidha, Baraza liongezwe bajeti yao waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.