Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya, nikasimama mbele ya Bunge hili Tukufu ili kuweza kuchangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati pamoja na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyosimamia, kuiendesha Serikali hii na kwa lengo la kuwapatia wananchi wote ustawi na maendeleo. Mheshimiwa Magufuli amefanya kazi nzuri na katika kazi yote hiyo iliyonifurahisha, moja inathibitisha kudumisha Muungano na inanifurahisha zaidi ni hii ya standard gauge nchini, Bombadia hewani, wabadhirifu, wafujaji na mafisadi kwapani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pongezi hizo za Dkt. Magufuli zinaenda pia kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa jinsi anavyoendeleza kazi zake, Mheshimwa Samia kwa kushirikiana na timu yake na vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yote nzima ya Mawaziri na Watendaji, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nasimama kifua mbele hapa kutoa tena pongezi nyingine kwamba watu kule Uyui katika Uchaguzi Mdogo tumewabandika matokeo Chama cha Mapinduzi, katika Vijiji 14 tumepata na CHADEMA moja, Vitongoji 51 na kwa CHADEMA saba, CCM mbele kwa mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa unaposema wewe wanakuwa wanaumia, wanakiherehere, lakini kila ukipigwa ngumi ndiyo unazidi kuwa imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua umuhimu wa Muungano na ndiyo maana leo mimi niko hapa bila ya Muungano nisingekuwa na sauti hii ya kusimama hapa kusema. Umuhimu wa Muungano unajulikana, una tija, unaleta mshikamano, unaleta udugu. Sisi wengine tuna watoto mwisho wa reli huko, kwa sababu ya Muungano, hivyo hatuwezi kukubali Muungano huu ukatawanyika na Muungano huu una faida nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru mpaka sasa hivi kwenye ripoti hii tumeambiwa kero nyingi sana zimemalizika, zimebaki kama kero tatu hilo ni jambo la kupigiwa mfano, hongereni sana Wizara ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea sana lazima niseme hapa maana yake mimi bila ya kuletwa na Zanzibar haiwi. Natoa pongezi za dhati kwa Dkt. Shein kuendelea kuishikilia na kuiongoza Serikali ya Chama cha Mapinduzi bila wasiwasi, maendeleo yanaonekana, kazi nzuri inafanyika na wale wanaongoja zamu yao wangojee mpaka hapo 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mazingira ambalo limeonekana kuwa ni tatizo kubwa sana. Mazingira yanaharibiwa vibaya sana, vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, ukataji mikoko ya baharini. Kwa mfano, kama sehemu za visiwa ile mikoko iko pale kwa kazi maalum ya biodiversity kulinda maji yasiingie zaidi, sasa inapokatwa maji yanasogea ardhi ambayo ingeweza kuwa ya kilimo inakuwa ya chumvi, kwa hivyo tija inapungua. Nafikiri iko haja ya kuendelea kuimarisha zaidi udhibiti wa maeneo haya au vilevile kutangaza maeneo ya hifadhi zaidi ya hayo yaliyopo ili kuzuia mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba kuna tabia ya watu kuchukua maji kutoka kwenye mito kupeleka kwenye sehemu zao wanazozitaka matokeo yake ni kuleta shida, kwa nini na sisi hatufanyi kama vile walivyotangaza wenzetu kule India ule Mto Ganges na mito yetu na sisi tukawa tunaiangalia kwamba mtu atakayechafua chafua
au atakayeharibu anakuwa sawa na ku-temper na uhai, kwa hivyo lazima kuwa na udhibiti muhimu, tuziimarishe hizo sheria zetu za kudhibiti kwa sababu tunajua mazingira yakiharibika ndiyo uhai unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka niligusie kwa haraka haraka ni suala la ajira. Tunajua kwamba yalikuwepo makubaliano ya tutapata asilimia ishirini na moja ya share ya ajira kwa Zanzibar kwa nafasi za kutoka kwenye Taasisi za Muungano, sasa nimeambiwa nafasi hizo zipo lakini nataka Waziri akija hapa atuambie katika nafasi hizo wamepata Wazanzibari wangapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba kwa nafasi ya Majeshi na Polisi huko hatuna tabu vijana wetu wengi wanapata ajira. Kwa hivyo, tunaomba tufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusu hizo nafasi kwa sababu katika kuzipata hizo nafasi kwa vijana wetu yako malalamiko ya kusuasua katika kupatikana nafasi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni hili la kuhusu makazi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais kule Zanzibar bado hayajawa katika hali nzuri sana yamechoka, nafikiri iko haja ya kufikiria kufanya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nataka nizungumzie ukiunganisha na hiyo kwamba bajeti inayotolewa kwa Ofisi hii naona haitoshelezi, iko haja ya kuongezwa. Kwa mfano, Ofisi binafsi ya Makamu wa Rais kupata 3.7 kwa mwaka mzima bado ni ndogo sana. Kwa mwaka jana Wizara hii ilipangiwa billioni nane lakini imeweza kupata millioni mia mbili, sasa inawakwaza watendaji wa Wizara hii, pamoja na Mawaziri ambao wanafanya kazi nzuri sana, lakini tusipowapatia pesa za kutosha inakuwa ni kikwazo. Tunawapa kazi lakini hatuwapi nyenzo za kufanyia kazi za kutosha, hivyo iko haja ya kufikiria ili kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kusema, ni muhimu kuhakikisha Muungano huu unadumu na
unaendelea kudumu kwa sababu ziko tija tunazozipata na usalama tunao na tunaona faida zake. Kwa hivyo siyo Muungano wa kufanyia masihara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuwa na maneno mengi, maneno yangu ni kwamba Muungano udumu na tunaona kazi inayofanywa na viongozi wetu kwa hivyo tuwape support. Wanawake kwa upande wetu tunashukuru viongozi wetu wametupa nafasi za kutosha, lakini tunataka zaidi lakini kila tukisema tunataka zaidi Mheshimiwa Rais anasikia na anatuongezea.