Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuingia katika kikao hiki cha bajeti kwa awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja za Mawaziri wote wawili kwa asilimia mia moja. Nachukua pia nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu na team zao zote wanazofanya nazo kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango yangu itakuwa michache na nitajaribu kuitoa kwa ufupi sana. Nianzie na mpango wa MKURABITA. Nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Nimepita miradi mbalimbali ya MKURABITA na nimeona jinsi gani wananchi walivyohamasika na jinsi walivyokubaliana na shughuli ya MKURABITA na hivyo kuweza
kumiliki ardhi na kuwa na hati ambazo zinawezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali yangu kwa kuwa wananchi wameridhia ni vyema kabisa kwamba kwa sasa hivi shughuli hii iende moja kwa moja nchi nzima kwa kuangalia Majimbo ili kila Jimbo angalau tuwe na mfano mmojawapo wa kufanyia hii kazi. Nimeona
akinamama jinsi walivyopata hati za kumiliki ardhi pamoja na vijana, kwa hiyo, nashukuru na naiomba iendelee kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la TASAF, nimepita katika miradi mbalimbali nimeangalia, nimeona TASAF jinsi ilivyofanya kazi vizuri na kuwezesha watu wenye kipato kidogo kuweza kujenga nyumba, kupeleka watoto wao shule na kuwanunulia uniform, lakini pia na kubuni miradi mbalimbali ambayo imewawezesha kuongeza kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, kwa wale Watendaji wachache ambao hawakuwa wema, wakaamua kuvuruga utaratibu huu, nafahamu kwamba wamechukuliwa hatua, lakini ni vyema Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atuambie wale watendaji ambao kwa
makusudi wameamua kuvuruga utaratibu huu wamechukuliwa hatua gani? Badala ya kuwalazimisha wananchi walipe pesa ambazo hawakuziomba. Wale waliowajazia ndio walikuwa na matatizo. Kwa hiyo, tuwanusuru wale ambao wanalipishwa fedha ambazo hawana uwezo wa kulipa, tuwashughulikie wale waliowaandikisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika Mfuko wa Rais wa Uwezeshaji. Mfuko huu umefanya kazi vizuri sana, nampongeza Mheshimiwa Waziri na team yake yote, kwa sababu vikundi vya vijana ambavyo vimewezeshwa na Mfuko huu vimefanya kazi vizuri, lakini fedha zile zinazotolewa
zimekuwa chache. Ni vizuri tuangalie uwezekano wa kuwaongezea ili waweze kufanya kazi na kujiajiri wenyewe. Kwa sababu katika vikundi nilivyopitia, nimekuja kugundua kwamba siyo wote ambao elimu yao ni ndogo, wapo ambao wana elimu kubwa, wamejiunga na
wamewachukua wenye elimu ndogo na kufanya mradi wa pamoja hivyo kuweza kuajiriana wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nawapongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la TAKUKURU. TAKUKURU imefanya kazi nzuri, japo watu wanabeza. Kwa sasa hivi suala la rushwa limepungua, kwa kiasi kikubwa na kama Mheshimiwa Waziri alivyoelezea, wameweza kuokoa mamilioni kadhaa kutokana na mchakato uliofanywa katika kukagua na kutenda kazi zao. Ninachoshauri, fedha zile mmeeleza zimeenda Serikalini, lakini hatujaambiwa zimeenda kufanya nini? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie fedha hizo walizookoa zimeenda kufanya nini? Kwa sababu bado tuna matatizo kwa wananchi, fedha hizo zinaweza zikatumika kwa ajili ya kazi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la Usalama wa Taifa. Suala la Usalama wa Taifa ni suala nyeti na kama ni suala nyeti, naona kuna watu wanalifanyia uzembe uzembe tu. Mtu anaamka asubuhi, anatuma message, nimetekwa nyara. Hivi kutekwa nyara mchezo!
Mnatania suala la kutekwa nyara! Yaani mtu anatuma message, “nabadilisha nguo, naenda Polisi, nimetekwa nyara. Huko kutekwa nyara, mbona mnaifanyia utani taasisi hii!
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu ananyanyuka, anasema Wabunge 11 watatekwa nyara; yeye alikaa nao vikao akawajua hao Wabunge 11! Naomba Usalama wa Taifa kwanza wawanyanyue wale waliosema kuna Wabunge 11 humu watatekwa nyara, watutajie ni akina nani? Walikaa
wapi? Wanatekwa nyara kwa kosa gani? Kwa sababu Usalama wa Taifa, mimi nategemea mpaka tumekaa hapa, ni kwamba wako kazini na wanafanya kazi vizuri. Ni vizuri basi wakaongezewa fedha katika idara yao, wapate mbinu mpya za kufanya kazi, waongezewe vifaa tuweze kupata usalama zaidi. Mtu kutwa, anaamka asubuhi anatuma message kwa rafiki yake, “nimetekwa nyara.” Hebu waulizeni waliotekwa
nyara, hiyo simu unaipata wapi ya kutuma hiyo message? Kutekwa nyara mchezo! Hebu waulizeni wanaotekwa nyara, watakwambieni ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu mchezo wale wanaojifanya usalama fake, naomba Mheshimiwa Waziri unayehusika washughulikie. Kwa sababu sasa hivi mtu akishakata panki lake, akavaa kaunda suti yake, anatoa kitambulisho; mimi Usalama wa Taifa. Usalama wa Taifa
mchezo! Mtu amejizungusha zungusha tu huko, anawatisha watu mtaani, anasema Usalama wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wale ambao wanajifanya Usalama wa Taifa na kuwahenyesha watu mtaani, washughulikiwe. Wale wanaojifanya Usalama wa Taifa, kutoa data za uongo, washughulikiwe; sambamba na data za uongo za kwenye mitandao. Tumechoka! Nchi iko juu juu; watu tuko juu juu tunahangaika! Usalama wa Taifa wapo, mnawanyanyapaa; hebu fanyeni kweli; na tuanzie humu humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anasema hapa ushahidi ninao, usalama wa Taifa upo, hamjamchukua mpaka leo kuja kukwambieni Mbunge gani aliyetekwa nyara; mnamwacha tu, kwa nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie suala la utawala bora nikienda sambamba na maadili ya viongozi. Tumekaa muda mrefu tukizungumzia Ma-DC, Ma-RC tunajisahau sisi humu ndani. Maadili tuanze nayo sisi wenyewe na uongozi tuanze nao sisi wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukaa humu ndani miaka 30 au miaka mitano; kama toka mwanzo wamekuja na mpango wako wa kutukana, utafikiria utaratibu wa huku ni wa kutukana. Naomba semina hizi zianze pia na kwa Wabunge ili tuweze kuwasimamia wenzetu. Kama semina
hizi watu watapata, kila mtu atajua wajibu wake ni nini, mamlaka yake na madaraka yake yanaishia wapi? Hatutazozana na DC, RC na wala wao hawatazozana na Wabunge. Isipokuwa kwa sababu semina hizi hazipo, ndiyo maana kila mtu anajiona yeye kubwa kuliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Ma-RC, Ma- DC wazuri sana, wanafanya kazi vizuri sana; lakini wale baadhi ambao wanakosea ni sawasawa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walioko humu wanaofanya kusudi. Kuna wakati nilisema tupimwe akili, watu wakacheka, lakini
tunakoelekea itafika wakati watu watapimwa akili humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu yanayofanyika huku unajiuliza kweli huyu kiongozi, wanafikiria kujaza zile form za maadili ndiyo maana yake umemaliza maadili ya viongozi kumbe ni pamoja na matendo tunayoyafanya.
Taarifa....
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unitunzie muda wangu. Pili nataka kumwambia anayeongea, hiyo taarifa yake siipokei. Kwanza naona kazuka tu! Kwa sababu suala la Usalama wa Taifa, imeitwa Taifa; haijaambiwa wa chama wala wa idara fulani. Ina maana hapa tulipo wenyewe wapo na wanafanya hiyo mambo yake halafu asijadiliwe, ndiyo maana mnaitwa mnahojiwa. Ingekuwa hivi hivi, humu ndani kusingekuwa salama. Iko siku humu ndani mtu angetoka vichwa vingebaki humu; lakini kwa sababu watu wapo na wanatulinda, ndiyo maana mnaona amani ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba, suala la Usalama wa Taifa wasilichukulie mchezo, mchezo. Watu wana-support tu; wakisikia fulani katekwa nyara, hata kwa message wanakubali. Ninachosema ni kwamba, tunaomba amani iwepo na ninaendelea kusisitiza wale Wabunge waliosema wanawajua 11 wapo, watutaje; inawezekana labda na mimi nimo, nijue ni jinsi gani ninavyojilinda. Hawawezi kusema halafu wakaachwa na wamesema wanao ushahidi. Mmeona!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kabisa, asubuhi tunaingia hapa tunaomba dua, tunawaombea na viongozi wetu na Rais tunamwombea; baada ya dakika kumi, wanamtukana halafu wanasema hashauriki. Sasa hata ungekuwa wewe, huyo mtu anakudharau, anakutukana,
unamwita akushauri nini? Kwa sababu kinachotakiwa hapa Wabunge tumepewa nafasi ya kuishauri Serikali na kuisimamia. Muda tunaopewa kuishauri Serikali na kuisemea, hatufanyi hivyo, tunaikashifu na kuitukana, halafu mkihojiwa mnasema kuna kanuni. Kuna haja ya kuja kubadilisha hizi kanuni ili watu tuheshimiane vizuri humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwamba kama suala la kuheshimiana, tunavyoapa hapa, tunajaza form, tuendelee kuheshimiana na tumheshimu kila mtu kwa nafasi yake. Mheshimiwa Rais sio mtu wa kumtukana; asubuhi huwezi ukamwombea dua, mchana unamtukana, wajirekebishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema siku moja kwamba nyoka wa kijani huwa haumi, siku akiuma hana dawa. Sasa yule nyoka kaanza kufanya kazi; wakiitwa kuhojiwa wanasema wametekwa nyara. Hatuteki nyara mtu! Mnatakiwa mkatoe maelezo kwa nini mnatukana? Ujiulize,
kwa nini kila siku unahojiwa wewe? Jiulize, kwa nini kila siku unaitwa wewe Polisi? Ukishapata jibu utanyamaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba naungana na wenzangu wote wanaotetea Madiwani posho zao ziongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante.