Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniingiza katika jengo hili, lakini pili, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.
Tatu, nimpongeze Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia, anawawakilisha wanawake wote hapa, mambo anayoyafanya mnayaona. Nne, nimpongeze Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Mwalimu Majaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika nichukue nafasi hii kuwapongeza TAMISEMI kupitia Waziri wake wa TAMISEMI kwa kazi wanayoifanya. Nimpongeze Naibu Waziri wake kamanda Mheshimiwa Jafo kwa ziara anazopiga. Katibu Mkuu Injinia Iyombe, mzee maarufu yuko pale TAMISEMI
inasonga mbele. Nirudi kwenye Utawala Bora, nimpongeze Mheshimiwa Angellah kwa kazi anazozifanya na Dkt. Ndumbaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina ajenda kubwa sana, ninayo mambo kama mawili au matatu. La kwanza kwa nini TAMISEMI inapongezwa. TAMISEMI ndiyo inashughulika na kila Mtanzania TAMISEMI kwa sababu ukienda kule kwenye Serikali ya Mtaa, Mtendaji wa Mtaa, Mtendaji wa Kata, Diwani na Mbunge ni wa TAMISEMI. Tunawapongezeni sana TAMISEMI na tuna haki ya kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa sababu TAMISEMI ndiyo imebeba mzigo wa Watanzania waliokuwa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namba mbili nihamie Utumishi. Utumishi kwenye kitabu chao wametuonyesha wameweza kugundua watumishi hewa zaidi ya 13,000. Si kazi ndogo, ni kazi ya Chama cha Mapinduzi kuelekeza lazima tuwaondoe mafisadi ndani ya Serikali yetu, tunakupongezeni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Utawala Bora kwenye eneo la TAKUKURU. Kwenye taarifa ya juzi ambayo TAKUKURU waliwasilisha kwa Mheshimiwa Rais imeonyesha wameokoa shilingi bilioni 53. Siyo kazi ndogo, ni kazi ya kusifia. Vilevile tayari tumeanzisha Mahakama ya Mafisadi tuwaombe TAKUKURU basi wale mnaookoa zile fedha waende kwenye Mahakama, msikae na mafaili pale
mezani ili impact ya kuokoa na watu wameenda kufanywa nini ionekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu sitasema sana, lakini mdogo wangu pale amesema, jana hapa kuna watu wanabeza elimu bure. Tumeenda pale kwenye semina ya TWAWEZA watu wanabeza elimu bure, sielewi, inawezekana hoja ya mpinzani ni kupinga. Kama ilikuwa shule watoto
wanaenda 200 leo darasa linaenda watoto 400 kwa sababu elimu ni bure kuna haja gani ya kutoipongeza Serikali hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliyoiuza kwa wananchi waliokuwa wengi na tukasema elimu itakuwa bure. Leo mwezi mmoja shilingi bilioni 18 zinaenda si kazi ndogo, ni kazi kubwa sana.
Taarifa....
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni taarifa ambayo imeletwa na wale wanaojifunza Chama cha Mapinduzi kinafanya nini. Kwa hiyo, ngoja tuwaunge mkono kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeisema na nashukuru imetoka kule, wao walikuwa na ajenda wanasema ufisadi, ufisadi lakini kwenye kutafuta kura wao wakakumbatia mafisadi. Nafikiri hiyo kumbukumbu wanayo vizuri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye kitabu cha msemaji wa jana wa Kambi ya Upinzani. Wakati anailaumu TAMISEMI kwa kupeleka maombi ya kutaka kujenga stand Moshi, sijui Halmashauri gani imetaka nini lakini mwisho akasema, TAMISEMI inakataa kuwaruhusu wasijenge stand kwa sababu wao ni wapinzani na akasema inaruhusiwa Morogoro na Tanga. Naomba nimjulishe vizuri ni Diwani mwenzangu huyo, ni mzoefu wa muda mrefu anaelewa taratibu za Local Government lakini ukisema Morogoro ni ya CCM, Tanga je? Umesahau una mtu wa hapa wa CUF ni Mbunge wa Tanga Mjini? Umesahau Halmashauri ya Tanga ni ya upinzani?
Taarifa...
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulikuwa Madiwani zamani hawa nao wakaja vijana, kwa hiyo, Diwani ukimsema lazima itafikia hatua hiyo.
Mimi nimesoma kilichoandikwa kwenye kitabu maelezo ya ziada ameyatoa kwenye mdomo wake saa hizi, kwa maana leo Tanga iko chini ya Upinzani na mradi unafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyongeza unavyoandika mradi kama Diwani katika Halmashauri yenu kwa nini TAMISEMI anapatikana? TAMISEMI ndiyo guarantor wa hiyo hela mnayotaka kukopa. Ni sawasawa na unapoandika mradi unaupeleka benki ni lazima Meneja
akubali huwezi kumlazimisha. Kwa hiyo, nashauri yale majiji yanayoandika miradi kuomba Serikali iwadhamini, andikeni miradi kwa kujifunza kwa wenzenu ambao wameshapata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahamia kwenye kitabu cha mama mmoja namheshimu sana. Huyu mama ni Mheshimiwa Mbunge, eeh ni mama kwa sababu hata nikimsema utajua ni mama.
Mheshimiwa mama, mama haifutiki. Huyu Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye Utawala Bora, Mheshimiwa Ruth Mollel, jana amesema hapa kauli nzito kidogo. Akasema Mheshimiwa Rais kwenye uteuzi wake wale wote waliogombea ndani ya CCM wakashindwa ndiyo wamekuwa Wakurugenzi, ma-DC na kadhalika. Swali langu dogo, Mama Mollel tangu amestaafu ni juzi, anataka kutushawishi kwamba aliingiaje CHADEMA, wale aliokuwa anaajiri alikuwa anaajiri Wakurugenzi kwa ajili ya maandalizi ya CHADEMA? Kwa sababu ni mtumishi ambaye amekuwa Serikalini mpaka amestaafu, anaheshima yake, anakula pensheni aliwezaje kutengeneza ajira ya wapinzani wengi
na leo siku tano anakuwa Mbunge anatokea ndani ya Chama cha Upinzani? Sasa nasema hivi Rais anayo mamlaka ya kuona nani anamfaa, nani amteue, nani amwakilishe katika Serikali yake anayoiongoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyongeza, heshima anayopewa huyu mama hebu aendelee kuiheshimu pamoja na kuwa yuko upinzani, ana siri nyingi za nchi yetu huyu. Ikiwa ataonekana huko alikotoka alikuwa anaandaa mazingira ya CHADEMA basi tutaangalia sheria zinasema nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba hoja zilizopo mbele yetu Tanzania ni moja.
Kuna mwenzangu jana wa Kigoma alikuwa anasema barabara yangu, eneo langu la wapinzani, sijui Mheshimiwa nini mwalimu lakini, nataka kuuliza mnaposema maeneo ya wapinzani hayahudumiwi elimu bora kuna mwanafunzi wa CCM na mwanafunzi wa CHADEMA? Mbona wote mnasoma elimu bure, mbona kule hamsemi hayo mazuri.
Ndugu zangu sisi ni Watanzania tukitoka hapo nje tunakunywa chai pamoja, tunapanda magari pamoja tusiitenganishe nchi yetu kwa itikadi zetu. Tutajenga mzizi ambao siku tukija kusema usifanyike gharama yake itakuwa kubwa sana. Tupingane kwa hoja, tushauriane kwa hoja na
siku ya mwisho tuwe wamoja kama Watanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.