Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii, kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi, aidha nipende kuchangia katika Wizara hii ya Waziri Mkuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi, ninaipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa mipango mizuri ya kuinua uchumi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Waziri Mkuu, kimsingi inaonyesha ukusanyaji wa mapato umepanda toka shilingi bilioni 850 mpaka trilioni 1.2, hii ni hatua nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze udhibiti na usimamizi bora katika haya yafuatayo:-
(i) Matumizi bora ya fedha inayopatikana;
(ii) Kuziba mianya ya rushwa ambayo ilikuwa imekithiri;
(iii) Kukomesha ubadhirifu wa mali ya umma kwa kuchukua hatua stahiki; na
(iv) Wizi wa mali ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo imeleta imani kubwa sana kwa Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa sana katika afya, elimu, miundombinu, kilimo. Katika mkoa wangu wa Ruvuma ambao unajumuisha Wilaya sita zenye jumla ya majimbo tisa ambayo ni kama ifuatavyo; Songea Mjini, Peramiho, Madaba, Namtumbo, Tunduru Kusini, Tunduru Kaskazini, Mbinga, Mjini, Mbinga Vijijini, Nyasa.
(i) Upungufu wa madarasa baada ya sera ya elimu bure kutekelezwa; (ii) Vifaa vya kufundishia;
(iii) Madeni ya walimu; na
(iv) Nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa afya ndipo penye changamoto lukuki, hapa nitaeleza chache na nyingine nitachangia kwenye Wizara ya Afya:-
(i) Kuna kituo cha afya cha Mjimwema katika Manispaa ya Songea kinahudumia wananchi wengi sana lakini mgao wa dawa wanaopata ni mdogo sana, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgao wa dawa ikiwa ni pamoja na kukamilisha vifaa vya chumba cha upasuaji ili
akinamama ambao wanakufa kwa kukosa huduma za upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hicho cha Mjimwema kipo kwenye mchakato wa kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya tangu mwaka jana, ni lini mchakato huo utakamilika?
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kituo cha afya cha Lusewa (Mji Mdogo) Wilayani Namtumbo ambacho hakina gari la wagonjwa wala vifaa vya upasuaji. Kituo hicho kiko katika jiografia ifuatayo:-
(a) Kutoka Lusewa - Namtumbo - kilometa 80;
(b) Kutoka Lusewa - Songea Mjini - kilometa 150; na
(c) Kutoka Lusewa - Mbesa Wilayani Tunduru - kilometa 150
Mheshimiwa Mwenyekiti, adha wanayoipata wananchi wa Lusewa ni kubwa mno na inatia huruma sana, nimeshuhudia mama anayejifungua akibebwa katika tenga mithiri ya nyanya katika pikipiki akiwa anasafirishwa kilometa 150 toka Lusewa. Pata picha halisi ni maumivu kiasi gani
anayopata mama huyo, hivyo basi akina mama wengi sana wamepoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba yafuatayo kupitia kituo hicho cha afya cha Lusewa; gari ya wagonjwa, vifaa vya upasuaji, dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya miundombinu katika Mkoa wa Ruvuma bado ni tete. Barabara ya kilometa 124 - Lokujufusi - Mkenda bado haijaanza kutengenezwa kwa kiwango cha lami, barabara ya Lumecha - Londo Morogoro bado haijaanza, barabara ya Minga -Nyasa kilometa 66 bado haijaanza, bara bara ya Kitahi - Lituhi bado haijaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mpainduzi kupitia ATCL imenunua ndege sita, kati ya hizo mbili zimeshawasili na zimeshaanza usafirishaji kwa abiria katika mikoa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ndege (usafiri wa anga) utaanza kutoa huduma katika Mkoa wangu wa Ruvuma? Ikumbumbwe kuwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma nao pia ni miongoni mwa Watanzania ambao wanahitaji usafiri wa anga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa usafiri huu wa anga kupitia shirika letu la ndani la ATCL lianze safari Ruvuma kabla hizo ndege hazijachakaa au kabla ya Bunge hili la bajeti kuisha.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kilimo pia kuna changamoto zituatazo; upungufu wa mbolea ya ruzuku, mbegu zinazoletwa nyingine ni fake, pembejeo za kilimo kutokufika kwa wakati katika vituo vinavyotoa huduma, masoko ya uhakika na upungufu wa mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama mara kwa mara kuomba Wizara ya Kilimo kuleta huduma ya kibenki kwa maana ya Benki ya Kilimo ili kukuza mitaji ya wakulima wa Ruvuma ili waweze kupata fursa ya kukopa na kukuza mitaji yao na kufanya kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaimani unatambua kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye mvua ya uhakika hivyo hitaji la benki ni muhimu ili kusaidia wananchi waweze kuzalisha kwa wingi kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania, kwa sababu wakizalisha kwa wingi itakuwa neema kwa Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya maji katika Mkoa wa Ruvuma ni kubwa sana, wananchi bado wanakosa maji safi na salama. Kuna miradi ya maji ambayo ilijengwa na World Bank, miradi hii kwa taarifa za maandishi inaonekana imekamilika lakini kiuhalisia maji hayatoki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya maji ya World Bank imetumia fedha nyingi sana lakini haijazaa matunda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miradi hii inakamilika na inatoa maji? Miradi hii ipo katika Wilaya ya Namtumbo, Mbinga Vijijini na Tunduru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali yangu iendelee kuangalia vipaumbele kwa wananchi ikiwemo maji na kwenye maeneo ya vijijini vichimbwe visima virefu wakati mchakato wa maji ya mtiririko unaendelea basi wananchi waanze kutumia maji ya visima virefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali yangu haya yafuatavyo; zahanati na vituo vya afya vikamilishwe, vifaa tiba na dawa katika vituo vya afya vizingatiwe, pembejeo za kilimo zifike kwa wakati katika vituo vya kusambazia pembejeo, utafiti wa mbegu bora uzingatiwe ili kuleta tija kwa wakulima, ujenzi wa barabara zote nilizoainisha kwa kiwango cha lami, mawasiliano ya simu katika tarafa ya Wino kupitia Halotel ufanyiwe kazi haraka, vita dhidi ya dawa za kulevya uendelee, kulipa stahiki za walimu na madeni ya ndani yalipwe kwa watoa
huduma za ndani (wazabuni).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha na ninaomba pia mchango wangu huu wote uingie kwenye Hansard.