Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mnafiki, tena mnafiki sana nisipoanza kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais na Baraza lake la Mawaziri kwa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kwa weledi mkubwa na wananchi wa Tanzania wana matumaini makubwa sana na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimepitia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa ā€žAā€Ÿ mpaka ā€žZā€Ÿ, pia nimesoma Hotuba ya Upinzani maoni yao juu ya Mpango huu, kitu cha kusikitisha hotuba ya Mheshimiwa David Silinde rafiki yangu, yeye kama Msemaji Mkuu wa Upinzani, Nasikitika sana hotuba yake imetumia takwimu za kupotosha Bunge lako Tukufu na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukurasa wa tatu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani juu ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano, kwa kutolea mfano, kuna sentensi inasema takwimu za Wizara ya Fedha zinaonesha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano fedha ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni wastani wa asilimia 26 tu, hiyo tunazungumzia historia. Watanzania wanataka kujua tunapokwenda mbele tumejipanga vipi? Ukiangalia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano ijayo tunatoka kwenye hii asilimia 26 kwenda asilimia 40 ya bajeti ya maendeleo imetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika hotuba hii, kwa mfano, Kambi ya Upinzani wanadai kwamba Mpango wa Maendeleo wa Kwanza na huu wa Pili umeasisiwa na Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani na wahisani. Hii siyo kweli, mpango huu uliletwa Februari, 2016 katika Mkutano wa Pili tukaujadili, maoni na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge yameingizwa katika Mpango huu wa Pili ambao uliwasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa jana. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba mpango huu unaasisiwa na Mashirika ya Kimataifa, huo ni upotoshaji kwa Bunge lako Tukufu na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashangaa sana ndugu zetu wa Upinzani kule kuna wasomi wengi tu nawajua, lakini nashangaa katika hotuba yao kuna mapendekezo kwamba Mpango huu utengenezewe sheria. Mimi sijawahi kuona Mpango unatengenezewa sheria kwa sababu sheria iko fixed Mpango ni dynamic. Sasa ukitunga sheria kwa Mpango ambao uko dynamic ina maana kila mwaka tutakuwa tunatunga sheria ya kutekeleza Mpango, hiyo inawezekana kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalam Mpango unakuwa na monitoring and evaluation framework, kazi yetu kama Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali, baada ya kuupitisha huu Mpango wa miaka mitano kazi yetu ni kila mwaka tunaletewa taarifa ya utekelezaji, tunapitia na kuangalia kama utekelezaji wa kila mwaka unaendana na Mpango wa miaka mitano, lakini siyo kusema tutunge sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukurasa wa nne pia kuna upotoshaji mwingine wa takwimu. Paragraph ya mwisho inasema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulithibitishia Bunge hili na wananchi kwa ujumla kama shilingi 4,970.04 kwa siku zinatosha kuhudumia familia nzima. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri haijasema familia nzima, imesema income per capita, wastani wa pato la mwananchi, sasa humu wanatuletea taarifa za eti pato la familia, mmeitoa wapi hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa tano, deni la Taifa ukiangalia takwimu toka National Bureau of Statistics na Wizara ya Fedha, Deni la Taifa sasa hivi liko 20.9% na maximum debt sustainability threshold ni asilimia 50 ya GDP. Kwa hiyo, tukisema kwamba Deni la Taifa siyo stahimilivu hizo takwimu tunazitoa wapi na wakati nchi yetu ina takwimu ambazo tunazitumia hizi hapa? (Makofi)
Pia ukiangalia katika debt sustainability threshold pia kuna kuangalia asilimia ya deni as percentage ya total export. Takwimu zinaonesha ni asilimia 104.4 na ukomo ni asilimia 200, sasa hii hatari inatoka wapi Waheshimiwa Wabunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukurasa wa nane, kushuka kwa thamani ya shilingi. Mimi nashangaa hapa kuna hoja kwamba kushuka kwa thamani ya shilingi kutaathiri utekelezaji wa maendeleo, sijui ni logic ya wapi.
Ninavyofahamu kama nchi ikikopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo tunakopa kwenye dola. Dola ikija hapa nchini inaweka pressure kwenye shilingi, kwa hiyo, shilingi inapanda against dola, sasa ukisema kwamba kushuka kwa shilingi kutaathiri maendeleo pia sioni logic. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichotegemea katika hotuba hii ya Kambi ya Upinzani ni kuuleta mpango mbadala kwamba Mpango wa Miaka Mitano mliouleta siyo mzuri, mzuri ni huu hapa ndiyo tuuangalie lakini siyo kuleta taarifa ambazo zinapotosha umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia kuhusu upotoshaji wa takwimu, hii inanikumbusha wakati niko chuo, Profesa wetu wa Statistics...
KUHUSU UTARATIBU
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu....
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa siikubali kwa sababu tukisema kila mwaka tuwe tunaletewa sheria ambazo tunazipitia kwanza ni utumiaji mbaya wa fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maslahi ya muda sasa naomba niende kwenye ushauri juu ya Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Karagwe ni sehemu ya nchi na pia linastahili kuwekwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Karagwe tuna tatizo kubwa la maji na Mheshimiwa Rais Mstaafu, Jakaya kikwete aliahidi mradi wa Lwakajunju, naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano imeniahidi kwamba katika kipindi cha miaka mitano itahakikisha mradi huu unatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa jiografia ya Karagwe tuna miji mikubwa mitano ya Afrika Mashariki inayotuzunguka, ninaiomba Serikali katika Mpango wa Miaka Mitano watujengee barabara ya kuanzia Nyakasimbi kwenda Nyakakika, Nyabionza, Kibondo, Kiruruma mpaka Rwabwele, kwa sababu barabara hii itafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Karagwe na Kyerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Mpango wa Miaka Mitano napenda kuiomba Serikali iweke mpango wa kujenga hospitali ya Wilaya kwa sababu sasa hivi tunagemea hospitali ya kanisa la ELCT ya Nyakahanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia pia kuhusu umuhimu wa kujenga reli ya Kati ambayo itatuunganisha na nchi za jirani ili tuweze kutumia bandari zetu na reli yetu kupata mapato kupitia customs.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni la muhimu sana na ninawaunga mkono Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuchangia katika kusisitiza umuhimu wa kujenga reli ya Kati na reli ambayo itatuunganisha na nchi za jirani ili iweze kutusaidia katika kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, ili Serikali isiendelee kukopa sana ninaishauri Serikali iangalie mikakati ya kupata wawekezaji kupitia PPP framework na pia kuangalia ni namna gani tunaweza tukakopa kwenye International Capital Markets badala ya kuweka pressure ya kukopa ndani na kukopa kwenye soko la nje ambalo riba zake ni za gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera hatuna Chuo cha VETA napenda kuiomba Serikali katika huu Mpango wa Miaka Mitano pia waweke mpango wa kujenga chuo cha VETA katika Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia asilimia kubwa ya Watanzania wako kwenye bottom of pyramid, inabidi mpango wa Serikali wa viwanda uangalie zile sekta ambazo zinaajiri Watanzania wengi kama sekta ya kilimo. Tuwekeze kwenye kujenga value chain katika sekta ya kilimo ili iweze kutengeneza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Pia inatubidi kuwa na SME developments plan sijaona mkakati wake, kwa sababu ukiangalia kampuni za size ya kati tukiweza kuzisaidia zitaajiri watu wengi na itatusaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna haja ya kuunda SACCOS za vijana kwa sababu SACCOS hizi zikiwekewa mitaji zitasaidia kuwakopesha vijana ili waweze kujiajiri na kwa kufanya hivyo tutatatua tatizo la ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.