Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai kwetu sote tulio hapa, ambao tunaweza kushiriki katika mjadala huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imetupa dira ya nchi yetu inakoelekea kwa kazi zilizofanyika pia mwaka mmoja katika awamu hii ya uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.John Joseph Pombe Magufuli. Natoa pongezi kwa uongozi mzima na namshukuru Mungu kwamba nchi yetu iko salama na tuko tayari sasa katika kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kuzungumzia suala zima la ajira. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ametueleza kwamba vijana wapo wengi na wamepelekwa mafunzo lakini katika hao vijana aliotueleza wamepelekwa kwenye mafunzo hatukuambiwa lengo lilikuwa ni kiasi gani. Tumeweza kupewa takwimu pale kwamba vijana waliopelekwa mafunzo katika kipindi hiki walikuwa wawe vijana ambao watarudi ili waweze kuwa wameandaliwa vizuri, lakini je, lengo lilikuwa ni vijana wangapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata hofu kwa kasi ya maendeleo. Naona kwamba kwa speed tunayoenda siamini kama endapo hatutaongeza kasi tutaweza kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Nasema hivyo nikiwa na maana kwamba, pamoja na kuwa na rasilimali nyingi katika
nchi yetu, rasilimali kubwa sana ni rasilimali watu lakini watu hawa lazima waandaliwe na waandaliwe vizuri ili wanapohitajika watumike vizuri. Kwa hiyo, naomba au nashauri Halmashauri zote ziweze kujua hawa vijana walio katika umri wa kufanya kazi wameandaliwa kiasi gani?
Nikifika hapo nataka nisisitize tu kwamba tuwe na takwimu sahihi za kuweza kujua ni wangapi na wanapelekwa vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni bei kupanda hasa za vyakula. Muhimu zaidi nikienda kwenye ukurasa wa 21 inapozungumziwa kilimo, sikuona walipozungumzia kilimo au upatikanaji wa sukari katika nchi yetu. Sukari ni bidhaa ambayo imekuwa
ikipanda bei kila mwaka. Sukari ni bidhaa ambayo inatumika kila siku kwenye nyumba na kwenye familia. Sukari ni kitu ambacho tunaita ni kifungua kinywa, maeneo mengine kama ninakotoka ukitaka baraka, basi unampelekea bibi au babu sukari na anakubariki. Sukari imekuwa ni tatizo inapopanda bei na hasa tunapoelekea kwenye kipindi cha mfungo wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kama huu mwaka jana sukari ilianza kuadimika na mpaka sasa sijui kama Serikali imeshapata ufumbuzi kwamba mwaka huu sasa ifikapo mwezi Mei wakati wenzetu watakuwa wanafunga, sukari hiyo itabakia na bei ileile ili kila mtu afuturu kwa raha. Mara nyingi unakuta familia ambazo ni duni, wanafuturu kwa uji wa chumvi. Kwa kweli, katika nchi kama Tanzania haipendezi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, kipindi kama hiki, kabla hatujafikia ule wakati ambapo, nadhani sasa hivi viwanda vimefungwa tayari lakini Serikali iwe imefanya mpango mahsusi wa kuona kwamba, akiba ipo, wamewakutanisha wenye viwanda, waagizaji na wale wafanyabiashara wakubwa. Jukumu la kuagiza sukari litolewe kwa wale wenye viwanda. Hii inayokuja ghafla, sukari inaagizwa na watu ambao wapo tu, wafanyabiashara wamekaa tu wanangojea ili watupige bei siyo jambo zuri kabisa. Naomba hilo liangaliwe kwa sababu kila mtu ana haki ya kupata kifungua kinywa katika nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mbegu za mazao mbalimbali kwa wakulima wadogo. Hapa ndani ukizungumzia mbegu zinazozungumziwa sana ni korosho, kahawa, mahindi na mtama yaani zile cereals. Hata hivyo, sasa hivi tunazungumzia pia kilimo cha mihogo na viazi, sijasikia wala sikuona katika hotuba ya Waziri Mkuu akizungumzia tutapataje sasa mbegu ya viazi vitamu na mbegu nzuri ya mihogo katika Halmashauri zetu. Kwa sababu haya ni mazao mbadala na yote ni ya wanga lakini ikipatikana mbegu nzuri basi tutakuwa katika hali nzuri sana ya kuweza kuwa na mazao mengi ya kutosha na tutaweza kusahau hayo mambo mengine ya njaa. (Makofi)
Naomba nizungumzie jambo lingine kuhusu wanawake wetu na inavyozungumzwa katika Ilani ya CCM kwenye ule ukurasa wa 117, ibara ya 61, 62 na 63(a),(b), (c), (d) na (e), kuwawezesha wanawake kiuchumi. Imewekwa vizuri sana katika Ilani na imezungumzwa jinsi gani watasaidiwa au wataelekezwa kuwa na vikundi kama VICOBA na SACCOS lakini inapokuja kuwapa elimu wanaachiwa. Unakuta wanawake wako kwenye VICOBA lakini mwanamke mmoja anakuwa kwenye VICOBA zaidi ya kimoja akiamini kwamba nikivunja mzunguko hapa
nitapokea mwingine na mwingine, hiyo ni dhana potofu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwasiliane na vyuo au watu wanaotoa elimu ili wanawake wetu waweze kupatiwa elimu ya ujasiliamali na uwekezaji. Ukimuelimisha mwanamke umeelimisha familia nzima. Mwanamke akiwa na elimu ya kufanya ujasiriamali ambao unaeleweka, akiwa na elimu ya kuwekeza na hivi leo umetueleza hapa kwamba tutapata semina ya hisa na mwanamke huyo huyo akiwa na elimu ya hisa basi atakuwa amefungua milango ya kupata kipato ambacho kitakuwepo siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu na Tukufu itoe fursa kwa wanawake kupatiwa elimu na wasimamiwe na Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum. Wabunge hawa wa Viti Maalum wana muda wa kuzunguka mikoani na kwenye Taifa zima kuona kwamba wanawake hawa wanapata elimu. Tunaomba Serikali iweze kuzungumza na taasisi na vyuo mbalimbali, wanawake hawa wapatiwe elimu ambayo ina muendelezo, elimu ambayo kila leo watajua nikiwekeza hivi ni benki au kwenye hisa naweza nikasimama na nikawa nimeimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niseme kwamba jambo hili la elimu bila malipo limeleta faraja kwa wazazi wengi. Kuna wazazi ambao walikuwa hawawezi kupeleka watoto wao shule lakini sasa mtoto akiandikishwa akienda shule ana uhakika wa kusoma kutoka darasa la kwanza mpaka darasa la 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ninayoiona hapa wadau wengine wa elimu wamerudi nyuma, hilo neno bure limeleta shida. Maana yake ni kwamba mpeleke mtoto wako shule atapatiwa elimu bila malipo lakini haikutoi wewe mzazi kutokununua uniform, kumlisha mtoto wako na
kutokuangalia uhakika wa vitabu vya mtoto wako, madaftari na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jinsi gani tutaelimisha wananchi wetu waondoe hiyo dhana potofu kwamba elimu ni bure basi mtoto akishaandikishwa wewe mzazi usiangalie tena, hivi kweli? Hata mbwa anazaa mtoto wake anamtunza, anamtafutia maziwa, anajua saa za
kunyonyesha sembuse mwanadamu mwenye utashi, akili na anayetawala vyote, anashindwaje kujua kuwa mwanangu anatakiwa kula? Hii ni dhana potofu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba itolewe elimu kumwambia mtu sawa Serikali itakupa mwalimu, itatoa vitabu vya kufundishia na itahakikisha mwanafunzi anafika shuleni na anasimamiwa lakini wewe ukiwa kama mdau unatakiwa uchangie mambo yafuatayo na usikwepe majukumu. Hakuna mzazi anayezaa mtoto wake amuache hivi hivi. Naomba sana nyie Waheshimiwa Wabunge tushirikiane pamoja kutoa elimu hiyo lakini pia na Serikali iendelee kuelimisha kila wakati ili wajue kwamba wanawajibika na wanatakiwa kuendelea kutoa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nizungumzie suala la ajira. Vijana wengi wanamaliza vyuo na kuhitimu lakini wanatarajia kupata white collar jobs na kweli siyo wote wanaweza kwenda kulima. Pia wale wanaotaka kulima kama wanatokea eneo ninalotokea mimi Kilimanjaro wala hakuna ardhi ya kilimo. Niombe kama Serikali imejipanga vizuri iko tayari sasa kufungua maeneo mapya kwa vijana ambao wanamaliza vyuo waweze kupatiwa ekari za kwenda kufungua mashamba darasa ambapo pia yatakuwa ndiyo maeneo yao ya kuishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya kugawa vihamba yamekwisha, vihamba havipo tena na vijana ni wengi, nchi hii ilikuwa na watu wachache sasa hivi tupo karibu milioni 50. Nashauri na napenda sana watu wapate baraka wazae watoto wengi tu lakini na nchi yetu ihakikishe kwamba watoto hao wanapatiwa mahali pa kukaa na mahali pa kujiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema ni mwisho lakini sitaitendea nafsi yangu haki kama sitazungumzia suala hili la tabia nchi na jinsi ya kuboresha mazingira. Naomba sana wote tuwe tayari sasa kuotesha miti.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.