Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naitwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi niungane na wengine waliotangulia kusema kukupa pole na mtihani mzito uliokukuta tangu tukupitishe huna hata siku tatu humu Bungeni. Lakini mimi nishauri vyombo vya ulinzi na usalama hali hii ilionekana kwa muda mrefu tumeiachia kwa muda mrefu, na kilichonisikitisha kwa sababu nimekuwa Mkuu wa Wilaya karibuni miaka kumi, ni pale ambapo na vyombo vyetu vya dola vilipoingia humu ndani vikaanza ku-negotiate muda wote waliosimama tunajiuliza hivi wanafanya nini pale wakati kitu umeshatoa amri. Mimi niombe sana tukiendelea kufanya hivi wenzetu hawa watadharau na vyombo vya dola, yaani imeniumiza sana nimeona hili niliseme kabla sijachangia kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nizungumzie sekta ya viwanda, kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini tunalima michikichi, michikichi ndiyo inaleta mafuta ya mawese, lakini kinachosikitisha kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Rais anazungumzia dhamira yake ya kuanzisha viwanda kwenye ukurasa wa 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wamalaysia walikuja Kigoma kwa ajili ya kuchukua mbegu, leo Wamalaysia ndiyo wanaoongoza kuzalisha mafuta ya mawese lakini Kigoma kama Kigoma mpaka leo tumebaki kwamba tumetoa mbegu na mbegu zimekwenda Malaysia hata kama na wao walikuwa na michikichi yao walitambua fika kwamba mbegu ya Kigoma ndiyo mbegu bora, wakaipeleka Malaysia na kwenye takwimu zao wanakuambia mwaka 2011 Pato la Taifa Malaysia zao la mchikichi lilikuwa ni kama zao la nne kuwaingizia mapato, income ile ya Taifa, na wanakwambia walipata kwenye ile ringgit pesa yao ile wanaita ringgit, ringgit bilioni 53 sawa na dola bilioni 16,000.8.
Lakini sisi Kigoma mpaka sasa hivi mawese yanatengenezwa na wanawake wale wa kijijini na tunatengeneza kwa ile teknolojia ya kizamani ya asili, tunachukua masufuria makubwa tunachukua katika ule mti wa mchikichi ukishatoa ngazi kuna yale yanayobaki yale ndiyo tunakoka moto, tunaweka masufuria makubwa au mapipa tunachemsha ngazi, tukimaliza tukamua, ndiyo haya mawese mnayoyaona kwenye soko la Kariakoo pale Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana mimi inaniuma sana nilikuwa nimeingia kwenye website inayozungumza masuala ya palm oil, nikaona kwamba Tanzania yaani sisi tumejiweka kabisa kwamba Tanzania siyo nchi ambayo iko tayari ku-produce mafuta ya mawese. Inasikitisha kwa sababu moja, sisi pale tuna Lake Tanganyika, Congo DRC, lakini hata Congo Brazzaville, Burundi, Rwanda, Zambia tuna uwezo pia wa kuwapelekea mawese, kwa sasa tu kwa teknolojia yetu hiyo ya kizamani lakini bado tunayatoa mawese Kigoma, tunayapeleka Burundi, tunayapeleka Rwanda, tunayapeleka Congo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe sana hii dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu, hebu tuombe Wizara husika ione namna ya kutuletea wawekezaji kwenye Mkoa wa Kigoma watuanzishie basi kiwanda cha mawese. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mchikichi hili ni zao la mchikichi tunatoa pia sabuni, wengi mnazifahamu zile sabuni za rangi mbili ambayo ina rangi nyeupe na blue, zile sabuni zinatengenezwa kwa mise. Mise ni ile mbegu ya mchikichi tukishatoa mawese tunabaki na ile mbegu ya ndani ndiyo inayotengeneza sabuni. Sasa mimi niombe viwanda vya sabuni inawezekana kabisa tukavitumia pale Kigoma na angalau uchumi wa wanawake, hasa wanawake wa Kigoma ukaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile huwezi kuzungumzia viwanda bila kilimo, hapa wajumbe wengi wamezungumzia kilimo cha tumbaku. Kilichonisikitisha ni kama vile tumbaku inalimwa tu Tabora, jamani tunalima tumbaku Wilaya ya Uvinza na ndiyo maana Tarafa ya Nguruka pale taasisi ya kifedha hii ya CRDB imeona umuhimu kuja kufungua benki pale hawafungui hivi hivi. Kama wangekuwa hawapati faida wasingekuja kufungua branch ya CRDB pale Nguruka, wamefungua kwa sababu wanajua zao la tumbaku ndiyo zao ambalo pia linatuingizia sisi Halmashauri ya Uvinza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka Disemba Halmashauri ya Uvinza, tumepata shilingi milioni 800 kwenye zao la tumbaku, ndiyo Halmashauri inayoongoza kupata ile own source kupitia zao la tumbaku. Kwa hiyo, mimi niombe Mheshimiwa Waziri Mwigulu anapokuja asisahau kulifuatilia na hili zao la tumbaku hata kama hatuna Chama Kikuu ndani ya Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie reli. Kwenye ukurasa wa 12 Mheshimiwa Rais amezungumzia umuhimu wa kujenga reli kwa maana ya kuboresha inayotoka Dar es Salaam, Tabora, Mwanza na Kigoma. Lakini vilevile amegusa reli ya Uvinza, kwa maana ya kutoka Uvinza, Msongati, Burundi, Isaka, Kigali, Rwanda.
Mimi niombe sana Wizara husika tusiwe tunazungumza tu maneno ambayo hayatekelezeki, niombe kweli kweli Uvinza siyo ile mnayoifahamu, maana tatizo ukisema wewe Mbunge wa Kigoma Kusini, watu wakikumbuka Mbunge aliyepita alikuwa maneno mengi humu Bungeni wanadhani tuna hali nzuri, tuna hali mbaya sana Jimbo la Kigoma Kusini. Hatuna maji, barabara hatuna, umeme wenyewe umewashwa wiki tatu zilizopita tangu uhuru, umeme kwenye Jimbo la Kigoma Kusini tulikuwa hatuna umeme. Tumewashiwa umeme kwenye Kata tatu, Kata ya Kandaga, Kata ya Kazuramimba, Kata ya Uvinza na kwa kupambana mimi kuongea na Mkurugenzi wa TANESCO Ndugu Mramba na namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mengi hatuna maendeleo yoyote katika Jimbo la Kigoma Kusini, niombe sana Serikali iliangalie Jimbo la Kigoma Kusini kwa jicho la huruma, safari hii wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini wamepata Mbunge, wamempata Mbunge wa vijijini, hawajapata Mbunge wa Mataifa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kigoma Kusini na niwaambie ule upotevu na maneno mengi ya propaganda yanayoenezwa kule Jimboni, mimi ndiyo Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana nitawatumikia na tumeshaanza kazi nzuri, sasa hivi tunajenga zahanati karibu vijijini 20; tunaongeza madarasa kwenye shule ambazo miaka kumi shule ina darasa moja hapa mtu alikuwepo anajiita eti Mbunge wa Mataifa, Mbunge wa Dunia, Mbunge wa Dunia kwa wananchi waliokupa kura. Mimi niwaombe sana wananchi wa Jimbo langu la Kigoma Kusini kwamba niko imara nachapa kazi propaganda zinazoendelea Jimboni msizisikilize Mbunge wenu niko hapa, nitawafanyia kazi na Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaniunga mkono kuhakikisha tunatekeleza ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala moja lililozungumzwa hapa nadhani alikuwa Msigwa maana wote tumemsikia, tusiwa-criticize ma-RC na ma-DC. Bila ma-RC na ma-DC amani na utulivu kwenye maeneo yetu…
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja hotuba ya Rais. (Makofi/Vigelegele)