Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii nichangie kidogo kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa muda mfupi aliokuwa Waziri Mkuu alikuja Namanyere akafanya ziara katika Jimbo langu la Wilaya ya Nkasi akatembelea mpaka vyanzo vya maji ambavyo nilikuwa napiga kelele hapa kila mwaka habari ya shida ya maji Namanyere. Sasa mwaka huu tatizo la maji Namanyere litakuwa historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile namshukuru Waziri wa Maji, alifika Namanyere mpaka kwenye vyanzo vya maji na akaahidi kusaidia mitambo ya kusukumia maji. Namshukuru vile vile Waziri wa Mambo ya Ndani alifika Namanyere, pia Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Makamba alitembelea Namanyere. Mawaziri wote walitembelea Namanyere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa namshukuru Mheshimiwa Magufuli. Mimi nilikuwa Bunge la Nne hapa ndugu zangu, nilikuwa msumari nazungumza ukweli kuhusu mafisadi, wezi wa mali ya umma, nilizungumza mpaka makaburi yao yafukuliwe wafungwe minyonyoro kwenye makaburi. Nilizungumza vile vile safari za Wabunge kwenda nje hazina manufaa, tunapishana airport kama wakimbizi. Nilizungumza hapa kabla Mheshimiwa Magufuli hajawa Rais, nilisema hizi safari hazifai! Hebu niambieni Mbunge hata mmoja aliyekwenda nje alete tija hapa kama sio ubadhirifu wa hela humu. Wengine walikuwa wanarudia airport, nimezungumza hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushahidi wakamate hata passport zao waangalie, kama walipewa hela wakaenda, passport zitaonesha. Wengine wanapewa siku kumi wanakaa siku mbili wanarudi. Ndugu zangu tumsifu Magufuli amedhibiti nchi! Nilimwambia Rais Magufuli Kinyerezi kwenye kuzindua mtambo wa umeme nikasema; spidi yako bado sijaiona, bado spidi ni ndogo. Nchi hii bado mafisadi wengi, wanatuibia! Juzi juzi tu tender ya EWURA wanataka kutuingiza kutuibia bilioni sita kwa mwaka, shilingi bilioni kumi na tatu za Kitanzania kwa miaka mitatu mkataba huo tutaibiwa bilioni 40 wakati hatuna zahanati, hatuna madawati, hatuna kila kitu. Ndugu zangu bado watu hawaogopi Serikali, wapo! Hao wanataka wabanwe ikiwezekana kunyongwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Jimbo. Nimezungumza, Mfuko wa Jimbo kwanza usimame. Wapitie upya majimbo sio sahihi. Uchaguzi uliopita safari hii tumezidishiwa Kata kutoka Kusini kwenda Kaskazini, majimbo yameongezeka. Jimbo langu kata nzima imehamia kwangu
lakini Napata mfuko wa jimbo ule ule, nitahudumiaje kata ile nyingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Simbachawene nikampelekea na taarifa kwamba kata nzima imekuja kwangu. Haiwezekani niendelee kupata mfuko wa jimbo ule ule. Simamisha kwanza nchi nzima, fanya mchakato upya. Wabunge wengi wamelalamika hapa. Halmashauri ya Mji wa Namanyere ina vigezo vyote cha ajabu wamekwenda kutoa halmashauri zingine hazina vigezo! Ushahidi tunao, upendeleo wa hali ya juu na ugawaji wa majimbo vile vile kwa upendeleo. Haiwezekani! Nchi ni moja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majimbo kama kwa ndugu yangu huyu hapa, Sikonge square kilometers 27,000, kwa Malocha, 15,000, kuna majimbo mengine square metre 1,000 humu, kuna mengine 200! Haiwezekani! Hatuwezi kwenda hivyo. Lazima twende sambamba, haiwezekani Mbunge yule yule anapata pesa ile ile, gari ile ile, mafuta yale yale, jimbo lake linakuwa kubwa kama Rwanda, kama Burundi, haiwezekani! Hii ni kuoneana. Lazima Namanyere sisi tupate halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa imeanza juzi juzi halmashauri tano, sita. Cheki Mkoa wa Rukwa, Mkoa mkubwa kabisa halmashauri zile zile nne, haiwezekani! Ni maonezi hatuwezi kwenda. Ahadi ya Rais alituahidi alipokuja, barabara ya lami kilometa tatu tunaitaka Namanyere,
alituahidi kilometa tatu za lami, tunazitaka! Mheshimwa Mwenyekiti, hospitali Namanyere. Tuna miaka 40 Wilaya ya Namanyere haina hospitali ya wilaya, miaka 40! Watu wanasema miaka 20, miaka mitano mpewe hospitali. Kuna wilaya zimeanzishwa juzi zina hospitali ya wilaya, sisi miaka 40 hamna hospitali ya wilaya. Haiwezekani, haya maonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu DC wetu wa Nkasi. Tangu ameanza hana gari, hana usafiri. Anahudumia wilaya square kilometers 13,500 hana gari! Leo kasimamia shule 105 kujenga madarasa matatu shule ya msingi katika kila shule kuhamasisha wananchi na anajenga, anasimamiaje? Hana gari DC, anaombaomba magari. Polisi Namanyere hawana hata matairi. Ndugu zangu tuoneane huruma, kuna wilaya
zingine zinapewa magari matatu, manne hata hadhi ya wilaya hazina, ziko humu humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge hata ukubwa wa Kata kama Kata yangu hakuna! Wanapewa kila kitu. Lazima tufanye mchakato upya. Ikiwezekana Rais Magufuli aangalie, kama majimbo mengine ayafute! Ayavunje majimbo na halmashauri zingine. Hatutaki mambo
ya kuoneana. Kupanua halmashauri ambazo hazina hata uwezo, hazikusanyi chochote! Mzigo kwa Serikali. Tuambizane ukweli hata kama unauma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa ziwa Tanganyika; Awamu ya Nne tumeahidiwa meli mbili katika ziwa Tanganyika lakini nakuja kusoma tena ni utengenezaji wa Liemba ina miaka 113. Ndugu zangu, tunataka usafiri wa ziwa Tanganyika, meli mpya! Liemba itengenezwe maana bado inafaa, bado ni nzuri ikarabatiwe, lakini meli mpya tunaitaka katika Ziwa Tanganyika, wananchi wanapata matatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo. Hao wanaogawa ruzuku ya pembejeo, ndugu zangu haiwezekani mtu anasema ana deni milioni 360 wakati tukipiga hesabu ni mbolea bilioni 1.8 alipeleka katika jimbo langu. Wanachakachua, lazima wafuatiliwe. Nimemwambia hata
Waziri wa Kilimo, Waziri Mkuu nimemwambia, katika Jimbo
langu la Nkasi kuna kata kadhaa, hakuna kuwapa pesa
wamechakachuka, ni wezi wa hali ya juu. Ndiyo hawa Rais Magufuli anawatafuta awafunge mara moja hao. Hawa hawafai katika nchi yetu, haiwezekani anakuja mtu na briefcase anapewa kuleta mbolea, analeta gari moja la mbolea anataka milioni 360, huu ni wizi wa hali ya juu. Hawa ni watu wabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya mbolea ndugu zangu bora iuzwe bei chini, mambo ya pembejeo hakuna tena ruzuku waache ruzuku, kila mtu anunue kama vile ananunua vocha ya simu, mambo yaishe! Wametajirika watu kwa hela za vocha hizi, nchi hii ni wezi wa hali ya juu. Waaminifu ni wachache! Kwa hiyo, agenda zangu ni hizi hizi; nataka Namanyere kuwa Halmashauri ya Mji. Mheshimiwa Waziri Mkuu uliona Namanyere ilivyokuwa, kuna halmashauri zingine ukitembelea hakuna lolote, mnawapa halmashauri, ni uonezi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika; namwomba Rais Mheshimiwa Magufuli aendeleze, azidishe mara mbili. Asionee huruma mtu yeyote anayeiba hela za walipa kodi. Wananchi wetu, ndugu zangu majimboni kwangu kuna matatizo. Nazungumza habari ya usafiri kutoka
Kilado kwenda Kazovu miaka 50, tangu uhuru hatujaona gari! Nashukuru Ofisi ya Rais imenipatia pesa, mwaka huu wananchi wa Kazovu wataona gari! Niseme nini sasa? Nikose kumshukuru? Nilikuwa napiga kelele hapa wananchi hawajona gari, hawajaona bajaji lakini mwaka huu wananchi wataona gari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba na Waziri wa Ujenzi aniongezee tena hela nipasue ile barabara Kazovu kwenda Korongwe, wananchi wafurahie uhuru katika nchi yao. Rais asikate tamaa aendelee kupambana na watu kama hawa. Hakuna kuoneana aibu! Haiwezekani ndugu zangu katika nchi zingine, mtu anaimba wimbo wa matusi kumtukana Rais mwanzo mwisho anaachiwa! Nchi gani hii? Utawala gani huu? Wewe mtu unamtukana Rais unaachiwa? Aende Rwanda kule akaangalie au nchi za Kiarabu, watakunyonga! Wewe unamtukana Rais wa nchi, wewe umekuwa nani? Uhuru gani? Demokrasia gani hii? Unaimba nyimbo, wewe nyimbo na mtu wa studio anarekodi nyimbo, ama kweli sio utawala huu! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wangeniachia mimi dakika mbili niwaoneshe hawa! Haiwezekani! Kiongozi wa nchi anatukanwa na nyimbo, ukiisikia hiyo nyimbo ya Roma sijui Mkatoliki, ndugu zangu nyimbo ya aibu. Haiwezekani mtu unasikiliza nyimbo kama ile. Halafu unamshabikia mtu!
Haiwezekani! Kusema kweli ni makosa, ni kukosa adabu. Rais wa nchi hatukanwi popote pale. Haiwezekani! Nendeni nchi zingine, nenda Rwanda hapo, nenda Burundi, nenda DRC ukaangalie, watakushughulikia! Nyie mnacheka cheka hapa, haiwezekani kumchezea Rais namna hii. Huu ni utovu wa nidhamu. Huyu Rais anaheshimika, dunia nzima wanamsifu Magufuli. Leo nyie wenyewe ndiyo mnamwona hafai kwenu,
kote ukienda wanamsifu, Uarabuni wanamsifu, Ulaya wanamsifu, sijui ukienda… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji). MWENYEKITI: Ahsante