Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Mbarouk Salim Ali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MABROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia fursa hii ya kuweza kuchangia katika hoja hii ya bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kiongozi wangu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa ziara ambazo anaendelea kuzifanya za kuimarisha chama katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa ujumla. Lakini pia nimpongeze kwa hotuba yake ya tarehe tisa pale Lamada hotel Dar es Salaam kwa kweli ilikuwa hotuba nzuri sana, nampongeza sana Mwenyezi Mungu amjalie na amfanyie wepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba Inna-Lillahi Wainna-Ilayhi Rajiun na nasema hivyo kwa sababu mwelekeo wa nchi yetu kwa kweli unasikitisha sana. Unasikitisha kwa sababu inawezekana tunacheza na Mungu; binadamu hatakiwi kucheza na Mungu, tunacheza
na Mungu na kwa sababu mwanzoni katika kipindi cha kampeni tulikuwa tunaomba sana dua tunawaomba Watanzania watuombee dua na Watanzania wamefanya hivyo na viongozi wa dini wote wamefanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapomwomba Mwenyezi Mungu akusaidie na akakusaidia, lakini badala yake ukarudi sasa ukafanya mambo ya kimaajabu ajabu ya kutesa watu, kunyanyasa watu na kudhulumu watu kwa kweli hapo Mwenyezi Mungu anakuwa hayupo. Kwa hiyo, hili
jambo la kucheza na Mungu ni baya sana na hili halitotupeleka pazuri Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana kwamba hakuna linalokwenda, hali ya uchumi ni mbaya, hakuna ajira, kila linalopangwa halienda na hapa tulifanya fanya tu kidogo kwa sababu kulikuwa na pesa za kuokota za madawati ndio ikaonekana kwamba tulijitahidi tukafanya kidogo lakini hakuna lolote ambalo linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye issue ya Muungano; Waziri Mkuu katika hotuba yake amesifu sana vikao vinavyofanyika baina ya SMT na SMZ kuhusu kero za Muungano. Niseme tu kwamba kwa kweli tumechoka na kuona idadi ya vikao; wananchi wameona idadi ya vikao vinavyofanyika baina ya SMT na SMZ lakini hatuoni matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muungano sio wa viongozi, sio wa Mawaziri; waasisi wa Muungano walikusudia kwamba Muungano ni wa watu wa Zanzibar na watu wa Tanganyika. Sasa inapotokea kwamba kuna vikao vinakaa lakini haijulikani linalotatuliwa wala linalozungumzwa hilo ni
tatizo na hatuwezi tukaenda hivyo kwa sababu kero zipo pale pale. Kila siku vikao 13, 16, 20 lakini huoni jambo ambalo linatatuliwa, kwa hiyo hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kusikitisha zaidi ni kwamba hata zile mamlaka ambazo zinahusika na zile kero ukienda wanakwambia sisi hatujui, kama wametatua, wametatua wao juu. Sasa wanasiasa tunatatua kero lakini watendaji hawajui; kwa hiyo kero zinabaki zipo pale pale. Kwa hiyo, hili kwa kweli halitendeki vizuri hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu Msajili. Kwa kweli hatuwezi kuidhinisha pesa kwa ajili ya kwenda kufanya au kutumia mtu anavyotaka. Kama hatukupata maelezo mazuri ya Ofisi ya Waziri Mku ya pesa milioni 369 zilivyotumika kwa kweli hapa patachimbika, hatuwezi kuruhusu hiyo kitu, kwa sababu tunakaa hapa tunaidhinisha pesa kwa matumizi ambayo tunakubaliana halafu anatokea mtu tu wakati yeye mwenyewe ameshaandika barua kumpelekea Katibu Mkuu wa CUF kwamba Chama cha Wananchi CUF kwa sababu ya mgogoro tunakizuia ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa iweje tena urudi uipitishe ruzuku kwa mtu ambaye ameshafukuzwa, sio mwanachama lakini pia ruzuku hiyo hiyo ikatembea mpaka kwenye akaunti za watu binafsi, hatuwezi kufanya upumbavu wa aina hiyo. Kwa kweli hatukubali; hii ni lazima tupate
maelezo ya kutosha na vinginevyo hatuwezi kupitisha hii bajeti, lazima pachimbike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu Mfuko wa Jimbo hususan kwa sisi Wazanzibari. Pamoja na kwamba Mfuko wa Jimbo bado pesa ni ndogo sana yaani pesa ambazo zilikuwa zinatolewa kwa idadi ya watu kidogo sana ndio zile zile mpaka leo haubadiliki; nafikiri kuna mjumbe mwenzangu aliwahi kusema hilo. Lakini tatizo kubwa la Zanzibar hizi pesa zinachelewa sana; ile Serikali yenu ya Zanzibar inazikopa pesa kwa sherehe za Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila zikitolewa Disemba wanazichelewesha mpaka Juni ndio pesa tunazipata. Tunashindwa kufanya mambo ambayo tumeahidi kufanya sasa naomba patafutwe utatuzi wa tatizo hilo, sio mara moja mara mbili wala mara tatu, kila siku pesa hizi zinachelewa.
Wenzetu huku wanatumia pesa wanamaliza sisi bado kule tunaulizia kila siku; tumechoka kuja kuulizia pesa hii. Hili jambo hebu litafutiwe ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka nizungumzie kidogo kuhusu Bandari ya Wete. Bandari ya Wete pana kaofisi kidogo kabanda tu; hicho hicho wanatumia wavuvi na hilo hilo wanatumia wasafiri na hilo hilo wanatumia Ofisi ya Uhamiaji. Kwa kifupi ni kwamba pale pana movement kubwa sana ya wasafiri baina ya Pemba na Mombasa Kenya lakini kuna tatizo kubwa hakuna Ofisi ya Uhamiaji, forodha wala Ofisi yoyote. Kwa hivyo, inawezekana kuna upotevu mkubwa wa mapato. Namwomba Waziri Mkuu hili jambo tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu iliyopita ilisemekana kwamba pesa za ujenzi wa Ofisi pale tayari zilishatoka kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini la kusikitisha mpaka leo hatujaona lolote ambalo limetendeka. Hili Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba tulipatie majibu sijui
limefikia wapi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.