Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Stephen Hillary Ngonyani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, vilevile nitoe pole sana kwa familia ya Dkt. Macha kwa msiba mkubwa ambao umewapata. Nawapa pole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuilinda nchi hii. Wote sasa tumekuwa kitu kimoja na wote tumekuwa sawa.
Vilevile nisiache kumshukuru Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge pamoja na Wizara ya Afya pamoja na Wabunge wote bila kujali Vyama vyao kwa msaada mkubwa walionipitia wakati naumwa pale, hawakujali vyama wala itikadi za vyama vyao, walikuja wakaniona na walinipa faraja sana. Nawashukuru sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, haya mambo msiyafanye kwangu tu, myafanye kwa kila Mbunge msijali vyama vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nianze kwanza kwa kuongelea Mfuko wa Jimbo. Mfuko wa Jimbo toka tumeanza kuupata Mfuko huu wa Jimbo toka mwaka 2009 haujafanyiwa marekebisho ya aina yeyote. Mfuko wa Jimbo umekuwa ni kichocheo cha Wabunge katika kila Wilaya na kila Jimbo ili pale wananchi wanapojitolea sisi tunaongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu umekuwa hauwasaidii sana Wabunge kwa sababu unakuwa na mlolongo mrefu kiasi ambacho Mbunge hana uwezo nao, yeye kazi yake ni Mwenyekiti tu, lakini inapofika kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maendeleo yaliyoanzishwa na wananchi,
Mfuko huu unakuwa ni mgumu sana kama vile ni mfuko ambao tumepewa kama mtego. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, huu Mfuko wa Jimbo usiishie tu kwa Wabunge wenye Majimbo. Hata hawa Wabunge wa Viti Maalum wangekuwa wanapewa kiwango kiasi kwa sababu wengi wa Viti Maalum hawakai katika Majimbo peke yake,
wanazunguka katika mikoa yote. Wanapozunguka katika mikoa wanafika mahali akinamama wanawaambia tuna shida, utatoa wapi hela? Hela yenyewe ndiyo hii ya kuchanganya changanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba nao hawa Wabunge wa Viti Maalum watengewe kiwango kidogo kisilingane na cha kwetu lakini kiwasaidie kuzunguka katika mikoa yao ili itusaidie Wabunge wa Majimbo ili iwe inatupa nguvu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Mheshimiwa Waziri Mkuu akija atuambie sisi sasa hivi tuko wapi, kwa sababu mara nyingi tulikuwa tunaambiwa vifaa vya Wabunge katika Majimbo hasa zile furniture tunapewa na Ofisi ya Bunge, jambo la kushangaza hii taarifa kwa Waraka
wa mwaka 2010 inaonesha kabisa kwamba Mfuko huu uko chini ya Mkuu wa Mkoa, toka Wakuu wa Mikoa wamepewa huu mfuko kwa ajili ya kuwasaidia Wabunge, hakuna hata Mbunge mmoja ambaye amejengewa ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye Ofisi ya Bunge tunaomba vitendea kazi lakini tunaambiwa viko kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa hawatuelezi ukweli. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja kutoa hitimisho lake atuelekeze vizuri Wabunge tusisumbue Bunge. Tukisumbua Bunge wakati kitu hiki kishatengwa kwamba kwenye Waraka wa Rais wa mwaka 2010 unaonesha kwamba Mfuko huu uko chini ya Mkuu wa Mkoa na sisi tukija hapa tunaendelea kuwasumbua wenzetu ili tuonekane kwamba tunafanya kazi nzuri lakini kule vijijini watu hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tusijitetee sisi tu. Hapa tuko katika mazingira mazuri kufuatana na utendaji mzuri wa Rais wetu, lakini kuna Watendaji ndani ya Bunge hili wanafika wakati wao wenzetu ambao wanatusaidia kwa kila kitu hata mishahara wakati mwingine wanakaa miezi mitatu hawapati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge hakuna Mbunge ana mazingira magumu. Tulizoea raha sana ndiyo leo tunaona kwamba kuna ukata. Watu wanakwenda kwenye vyombo vya habari kusema kwamba kuna mazingira magumu, mazingira magumu hakuna. Ukiangalia bajeti yetu
ni ile ile, ila siku za nyuma Wabunge tuli-relax sana tukajisahau ndiyo maana inafika mahali mtu anakimbilia kwenye Vyombo vya Habari kusema Bunge baya, Bunge gumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mazingira ya mwaka 2010 hakuna kilichopungua ila utendaji wetu, raha zetu, maisha yetu, ndiyo tunakimbilia kusema kwamba maisha magumu. Hela tunapata kwa wakati, hela ni ile ile. Tulikuwa tunapata sh. 80,000, lakini sasa hivi tunapata karibu sh. 120,000 na tunapata sh. 200,000. Sasa tukianza kuyasema haya hatutendi haki. Naomba tuwe wawazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana! Niacheni niseme, kila mtu anasema kwa wakati wake, kila mtu yuko huru kusema. Tusiwe tu watu wa
kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niyaseme haya mapema kwa sababu inafika mahali tunakimbilia vyombo vya habari, tukae wenyewe, tuna uongozi wetu, tukae chini, tuangalie upungufu uko wapi, turekebishe kuliko kukimbilia kulalamika, kama sisi tunalalamika na wapiga kura nao watamlalamikia nani? Nimekosea eeh? Kumbe imefika mahali pake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye suala la matibabu ya Wabunge. Tungeomba ikiwezekana Waziri Mkuu amshauri Rais, matibabu ya Wabunge yarudi kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu yalikuwa….
Taarifa....
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei, kama yeye alikuja kufuata maslahi...
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, sasa sipokei taarifa kutoka upande wowote.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachojua kilichotuleta hapa siyo maslahi ya Wabunge ni maslahi ya wapiga kura waliotuchagua kuja kutetea Bunge hili. Kama watu walifuata maslahi basi wakabadilishe kazi ambayo itakuwa na maslahi juu yao lakini ninachokumbuka kilichotuleta hapa ni kutetea wanyonge waliotuchagua ili tuwape maslahi mazuri waendelee kutuchagua kwa namna
yoyote ile. Kwa hiyo, taarifa yake siipokei akatafute sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la matibabu ya Wabunge, naomba mzigo mkubwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu, naona kuna mahali nimewagonga kidogo ndugu zangu. Kama kuna mahali nimewakosea ndugu zangu Wabunge basi kawaida ya mtu huwa tunasameheana basi tugange yanayokuja, ahsanteni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la matibabu. Siku za nyuma suala la matibabu yalikuwa yanapitia Ofisi ya Spika na yeye alikuwa
anajua huyu anaumwa au huyu haumwi, inategemea sasa hivi tumeona kwamba Rais anafanya kazi nzuri sana lakini baadhi ya watumishi wake wanaweza kuchelewesha kitu kwa makusudi na kumfanya mgonjwa azidiwe. Hapa ningeomba Mheshimiwa Rais ambakishie madaraka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kutusaidia katika kututibu au kwenda kuzungumzia suala la aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nizungumzie mambo machache naona taarifa zinakuwa nyingi kwa sababu nimegusa maslahi ya Wabunge, nilichokuwa nataka kujali ni kwamba kauli aliyosema Mheshimiwa Simbachawene kwamba hakuna tunachokidai mambo yote yako sawa, kwa hiyo naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hoja zangu zote alinisaidia kunisafirisha India kwa kunilipia watu zaidi ya wawili. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa msaada wako mkubwa, usifanye kwangu tu, fanya na kwa hawa wengine ambao
maslahi yao wanaona kama yamebanwa banwa, Mungu awasaidie sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.