Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijasema mengi, kwanza niunge mkono hoja hii ambayo imeletwa mbele yetu toka Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na machache sana, lakini moja kubwa naomba tu kwa namna ya pekee niwapongeze wenzetu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri na watendaji wake, timu nzima ya Serikali, mmefanya kazi nzuri sana na hasa hii kazi ya kurejesha nidhamu Serikalini,
hongereni sana. Hili ni jambo jema na kila mmoja anaona tofauti iliyokuwepo siku za nyuma na siku za sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niendelee kuwashauri, kama ilivyo kazi yetu Wabunge ni kuwashauri Serikali, kwamba tunaomba utaratibu huu wa nidhamu ya watumishi wa Serikali ujikite katika kulinda misingi ya sheria. Tafadhalini sana, endelezeni nidhamu ya watumishi wa umma, tuwaheshimu watumishi wa umma kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya pekee naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kumaliza ligi hii ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ya kuwaweka ndani watumishi wa umma hovyo hovyo. Kwa kweli juhudi zimekuwa nzuri, sasa tunaona mashindano haya hayapo tena, maana huko nyuma ilikuwa Mkuu wa Mkoa akijisikia, Mkuu wa Wilaya akijisikia anaweza kumweka ndani ofisa yeyote wa Serikali bila utaratibu. Tunashukuru sana, jambo hili wenzetu wa Utumishi, TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu mmelisimamia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, Mheshimiwa Simbachawene najua amefanya vizuri katika jambo hili, na tunakupongeza sana kwa kazi nzuri anayoifanya. Lazima Wakuu wetu wa Wilaya na Mikoa wafuate sheria kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda nilisemee limeainishwa ukurasa wa 31 na 32 wa hotuba ya Waziri Mkuu ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Tunaishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe, Mheshimiwa Jenista, reli ya kati tafsiri yake ni reli inayotoka Kigoma kwenda Dar es Salaam ikiwa na matawi ya kutoka Tabora kwenda Mwanza na matawi kutoka Kaliua kwenda Mpanda, ndiyo reli ya kati hiyo. Sasa nimeona kwenye kitabu cha Waziri Mkuu, kuna juhudi kubwa zimefanyika katika ujenzi wa reli ya kati na hususan kuanza kufanya feasibility studies katika matawi haya ya reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashauri kwamba ili reli hii iweze kuwa ya kiuchumi, maadamu inaanza kujengwa kwa kiwango cha standard gauge ni vizuri reli hii ikatoka Dar es Salaam ikaenda Kigoma kwa sababu ya mzigo mkubwa, tani milioni nne zilizoko katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ambayo zinahitaji njia kwenda kwenye masoko ya Kimataifa. Tusipofanya hivyo, tutajikuta mbele ya safari, hii reli haitakuwa na faida za kiuchumi mbali na kusafirisha abiria peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda niliseme ni uwiano wa maendeleo katika Mikoa yetu. Waheshimiwa Mawaziri mlioko hapa nadhani Waziri wa TAMISEMI unanisikia, nchi yetu hii ina mikoa takribani 25.
Uwiano wa Mikoa hii umetofautiana katika sekta mbalimbali, ni vyema sasa Serikali yenyewe kama ambavyo mwaka wa 2016 mlitupa takwimu za hali ya umaskini katika nchi yetu tukawa na utaratibu wa kuiinua mikoa ambayo iko nyuma, mikoa hiyo iko nyuma kwa sababu za kihistoria tu. Mikoa kama Kigoma, Dodoma, Singida, Katavi, iko nyuma kwa sababu za kihistoria. Ni jukumu la Serikali kuweka uwiano sawa wa mikoa hii katika sekta mbalimbali kama elimu, maji, afya, kilimo, barabara na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine yana nafuu kidogo na maeneo mengine yana shida kubwa sana na wananchi wote hawa ni Watanzania hawa hawa.
Kwa mfano, Mkoa wetu wa Kigoma mpaka leo bado ni mkoa haujaunganishwa na Tabora kikamilifu, haujaunganishwa na Katavi, haujaunganishwa na Geita, haujaunganishwa na Kagera, haujaunganishwa na Shinyanga, hali ni mbaya sana.
Sasa naomba sana TAMISEMI mko hapa, Ofisi ya Waziri Mkuu, angalieni uwiano ambao una afya katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa wana haki sawa. Maeneo mengine yana unafuu na mengine yana shida kubwa. Kwa hiyo, naomba kama ushauri Serikalini kwamba ni muhimu sana kuweka uwiano wa maendeleo katika mikoa ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa niishauri Serikali ni suala la kilimo. Katika nchi yetu kuna maeneo yanapata mvua, Mwenyezi Mungu ameyabariki tu, yanapata mvua za kutosha na tunalo tatizo kubwa sana hata la kuzalisha mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu kwa kweli kwa miaka yote hii, miaka 50 ya uhuru sasa hatuwezei kujitosheleza hata kwa mbegu za mazao ya nafaka. Nilikuwa nafikiri ni wakati muafaka wenzetu wa kilimo na Serikali, yale maeneo yanayopata mvua za kutosha kwa mwaka mzima tuyape kipaumbele ili tuweze kuzalisha mbegu za kutosha ili tujitosheleze kwa mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha kwamba mpaka sasa nchi yetu tunazalisha mbegu asilimia 40 ya mbegu zilizobaki zinatoka nchi jirani kama Kenya, Zimbabwe na mataifa mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nizungumzie juu ya umeme wa Malagarasi. Niwapongeze wenzetu wa nishati wamefanya kazi kubwa na taarifa niliyonayo ni kwamba wenzetu wa Benki ya Dunia na African Development Bank wametoa fedha kwa ajili ya kuanza kujenga umeme wa
Malagarasi. Huo umeme ni muhimu sana kwa maendeleo ya watu wa Kigoma na ni dhahiri umeme huo utaingizwa pia kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa nizungumzie suala la maji, maji ni uhai na ni dhahiri kwamba maeneo yenye vyanzo vya maji vingi na mikoa ambayo ina vyanzo vya maji vingi tu sasa kwa sababu ya matatizo ya tabia ya nchi, uharibifu wa mazingira, naishauri Serikali
kwamba wakati umefika maeneo yenye vyanzo vya maji tuyalinde, kuwe na mkakati wa kitaifa wa kulinda vyanzo vya maji. Kwa mfano, katika Mkoa wa Kigoma, katika Wilaya ya Kasulu peke yake tuna vyanzo vya maji takribani 600 ambavyo havikatiki mwaka mzima. Vyanzo hivi vinapeleka maji yake katika Mto Malagarasi kwa kiwango kikubwa na maji hayo hatimaye yanakwenda kwenye Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mpango kabambe wa kupeleka maji Malagarasi, Urambo, Kaliua na kwingineko kama hakuna mkakati endelevu wa Serikali nina hakika tutafika mahali maji ya Mto Malagarasi yatakuwa hayatutoshi, hayataweza kuzalisha umeme na kufanya
shughuli za kilimo. Kwa hiyo, nashauri strongly kabisa kwamba wenzetu wa Serikali hata kama ni mwakani tuleteeni a comprehensive plan ya kulinda vyanzo vya maji. Iko mikoa yenye vyanzo vingi, Morogoro wana vyanzo vingi, Katavi wana vyanzo vingi tuwe na mpango mkakati kabisa kitaifa wa kulinda vyanzo vya maji katika maeneo ambayo maji hayakauki mwaka mzima. Ni kweli yako maeneo yenye shida lakini tukiwa na mkakati endelevu nina hakika maji haya hatimaye yatatusaidia sisi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, Mheshimiwa Simbachawene ulitembelea Kigoma, ulitumwa na Mheshimiwa Rais kule Kigoma…
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.