Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru sana. Na mimi naungana na wenzangu kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana, yeye pamoja na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumzia mambo manne ambayo nimepanga kuyazungumzia, nina salamu za pongezi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Sengerema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tunaipongeza Serikali, lakini kwa hapa tunazungumza mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tufikie salamu kwa viongozi wote wakuu wa nchi yetu pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo mnaratibu shughuli za maendeleo ya Taifa letu. Tunazungumza kama Wabunge tukiwa tumejumuika kutoka katika maeneo mbalimbali. Yapo maeneo ambayo sisi wenyewe kutoka kwenye maeneo tunayofanyia kazi ni mashahidi kwa namna ambavyo shughuli za maendeleo zinafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa namna ambavyo imeshughulikia jambo moja kubwa ambalo lilishakuwa kidonda ndugu kwa Taifa letu nalo ni nidhamu ya kazi. Taifa lilikuwa limefikia mahali pabaya. Sisi wote ni mashahidi, tumekuwa tukifika kwenye taasisi za umma na kuona namna ambavyo huduma zimekuwa zikitolewa miaka iliyopita, lakini tuseme kweli kabisa, katika hii Awamu ya Tano, tumeshuhudia mageuzi makubwa ya uwajibikaji kwa
Watendaji wetu. Kwa hilo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, lakini kiranja mkuu katika usimamizi wa Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa namna ambavyo unalifuatilia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Sengerema tuna mambo makubwa yamefanyika, moja, namshukuru sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Jimbo la Sengerema. TAMISEMI pale, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Waziri Simbachawene, kile Kituo cha Afya cha Ngoma A ambacho mmekitengea fedha, wananchi wa Sengerema wamenituma nifikishe salamu zenu kwa shukrani kwa namna ambavyo mnatufanyia kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Engineer Lwenge na msaidizi wako Naibu Waziri, ule mradi mkubwa kabisa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ngazi ya Halmashauri na Wilaya unaofanyika Sengerema, sasa uko katika hatua za mwisho kabisa. Shukrani kwenu pamoja na Serikali nzima kwa namna ambavyo mmesimamia mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Simbachawene tuna kiporo. Tumezungumza miezi michache iliyopita. Kwenye hesabu za Mfuko wa Jimbo zilizofanywa hivi karibuni, yapo baadhi ya Majimbo ambayo tulipunjwa. Halmashauri ya Sengerema ni mojawapo hali iliyotokana na makosa ya kimahesabu. Mmetuahidi kwamba kufikia mwisho wa mwezi huu fedha zile zitakuwa zimeshafika, lile salio. Naomba Mheshimiwa Simbachawene na Serikali kwa ujmla, jambo la mapunjo ya Mfuko wa Jimbo mlifanyie kazi, fedha zifike mahali pake, zifanye kazi kwa ajili ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizamie kwenye mchango, la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaanzia kwenye ukurasa wa 43. Umeanzishwa mfumo wa wazi wa kielektroniki kufuatilia uwajibikaji na utendaji wa Serikali, jambo hili ni kubwa sana. Ni muhimu tuipongeze Serikali.
Wamesema, kwa kupitia utaratibu huu, wata-track utekelezaji wa ahadi ambazo zimefanywa na Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, matamko, ahadi za viongozi wakuu wa Serikali akiwepo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali katika hili ni kwamba kwa sababu hatuna mashaka yoyote kuhusu umakini na Serikali yetu, lakini pia kwa kutambua kwamba sisi Wabunge ndio daraja la wananchi na Serikali, nilikuwa naomba uandaliwe utaratibu ambao Serikali kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, watakuwa wanatushirikisha Wabunge, tujiridhishe kujua yale ambayo tunaya-track katika maeneo yetu ya kazi ni yapi? Miradi gani ambayo inaonekana katika ule mfumo? Mahali ambapo pamesahaulika, sisi tuwakumbushe kwa kusema hili nalo ni sehemu ya yale mambo yaliyokusudiwa, yafanyiwe kazi kupitia huu mfumo wa kielektroniki ambao utawasaidia Watanzania kufahamu shughuli ambazo zinafanywa na Serikali. Kwa hiyo, naomba na nilikuwa naamini kwamba atakapokuwa anafanya majumuisho Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake, atatusaidia kuona umuhimu
wa kutushirikisha sisi Wabunge tujue miradi ambayo ukigoogle ama ukibonyeza ule mfumo unakuletea miradi iliyotekelezwa katika maeneo yetu. Tusipofanya hivyo, narudia tena kusema kwamba, sina mashaka na utendaji wa Watumishi wa Serikali, lakini binadamu ni binadamu. Sisi ni jicho la pili kusaidia kufikia yale yaliyokusudiwa katika kuyasimamia yaliyotekelezwa kwa namna ambayo tunakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia jambo moja la kufanya maendeleo katika maeneo yetu ya kazi. Tunapanga bajeti, kila mwaka tunaipitisha hapa. Tumekuwa na changamoto ambayo sijapata jibu lake, tutasaidiana kadri ambavyo siku zinaendelea. Suala la disbursement,
kufikisha pesa ambazo tunazipitisha hapa kwenye bajeti kwenda kwenye maeneo yetu. Ninazungumzia kutotimiza jukumu hili ama wajibu huu ambao sisi tunaufanya Kikatiba, tumekuwa tukipitisha bajeti kila mwaka. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hapa
Sengerema kwenye OC ambazo ndizo fedha ambazo zimeidhinishwa kufutilia miradi mbalimbali ambayo tunazungumzia hapa tuna asilimia 20 tu, lakini shughuli za maendeleo tuna asilimia 30. Nafahamu Waheshimiwa Wabunge wengi wanalalamika. Hilo siyo la kumnyooshea
mkono mtu yeyote, lakini ushauri wangu kwa Serikali, tusaidiane kupitia chombo hiki cha uwakilishi wa wananchi tuone namna bora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza na mwaka 2016 tumeshauriana hapa, yapo mambo tulikubaliana kwamba yako mambo hayakunyooka sana, lakini tutumie nafasi hii katika Bunge hili tuelewane vizuri kwa mfumo huu wa bajeti tulionao, tuone namna ambavyo tunaweza kutekeleza bajeti ambazo tunazipeleka kule. Haina maana yoyote kupitisha mafungu hapa kwa kiwango fulani halafu utekelezaji wake unakuwa chini ya asilimia 50. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza, hili ni letu sote, halina itikadi ya vyama kwa sababu tunazungumzia utekelezaji wa mambo ambayo kwa pamoja tumekubaliana kuyatekeleza. Kwa hiyo, nashauri sana Kamati ya Bajeti pamoja na Serikali kwa ujumla, tushauriane namna bora ya kuhakikisha kwamba mafungu tunayoyapitisha, fedha zilizokusudiwa zinafika mahali pake palipokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, ukisoma Mkataba wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo sasa ziko sita, ukisoma Ibara ya 49 inayozungumzia namna ambavyo tunaweza kuimarisha mtengamano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Inazungumzia habari ya Bunge Sports Club ikiwa ni chombo mahsusi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika michezo hiyo ambayo inafahamika kutokana na Mkataba wa Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia jambo hili kwa sababu ninaona kuna masuala yanaingiliana na hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa lile Fungu la Mfuko wa Bunge. Bajeti ya Bunge Sports Club inatokana na huo mfuko. Naomba Bunge pamoja na Serikali kwa ujumla tuone kwamba ushiriki wa Bunge Sports Club katika michezo siyo jambo la anasa ama la kwenda kutumia pesa hovyo, bali ni nyenzo ya utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Watendaji wote wa Serikali na Bunge kwa namna ambavyo mliwezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 tulikwenda kwenye mashindano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mombasa; tuliondoka katika mazingira magumu kidogo, lakini ninavyozungumza sasa hivi mambo yote yako level seat. Shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Spika na Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo mliwezesha jambo hilo. Tunasema ahsanteni sana. na imeandikwa katika maandiko matakatifu, asiyeshukuru kwa
kidogo hatashukuru kwa kikubwa. Sisi tumepata kikubwa, kwa nini tusishukuru? Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo inayoongozwa na Mheshimiwa Mtemi Chenge. Unapozungumzia fedha nyingi ambazo tunazipitisha hapa, utekelezaji wake unakwenda kutekelezwa kutokana na miongozo na sheria zilizotungwa katika Halmashauri, Taasisi zetu mbalimbali zikiwemo Wizara za Serikali. Ninachotaka kuzungumza hapa ni kwamba tunapozungumzia Sheria zinazotungwa na Halmashauri zetu, ndiyo mpango wa fedha wenyewe. Tumeshuhudia wote kama Taifa, wakati mwingine viongozi wakuu wa Serikali wamekuwa wakitamka matamko ambayo wakati mwingine katikati ya safari wanaamua kuondoa tozo ambazo zimeshakubalika kwa utaratibu wa kisheria kwa namna ambavyo tumekasimu madaraka kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, silaumu katika hilo kwa sababu kama kuna kero ni lazima ishughulikiwe hapo hapo, lakini ninachosema, tuboreshe utaratibu wa namna ambavyo tunaweza kukatiza katikati ya safari, kwa sababu hizi Sheria Ndogo ndiyo zinaongoza mafungu ya kule Halmashauri na hasa mafao yale ambayo yanakwenda kuwawezesha hata Madiwani wetu ambao sisi tulioko hapa tunawategemea na ni Madiwani wenzetu kutekeleza miradi
mbalimbali ambako fedha nyingi zinakwenda. Tusiwakatishe katikati ya safari. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya bajeti hizi, kuwe na utaratibu mzuri wa kukaa pamoja tuelewane kwamba mwaka huu tutaondoa tozo hizi na hizi ili wasizifuate kwenye bajeti zao wanazoziweka. Tukikatisha katikati tutakuja kuwalaumu hawa wawakilishi wa wananchi wenzetu kwamba hawatimizi wajibu wao, lakini kwa kweli mazingira ambayo yamesababisha kumbe nasi tumeyachangia. (Maiofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hili narudia kusema, simlaumu mtu yeyote lakini naomba tulifanyie kazi kwa uzuri kwa namna ambavyo tutaweza kuwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji). MWENYEKITI: Ahsante.