Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima na uhai leo tuko katika Bunge hili tukichangia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Waziri Mkuu unajituma sana, hongera sana na kote ulikopita kuna mafanikio makubwa sana. Naomba tukupongeze sana.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Waziri Mheshimiwa Jenista pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa waliyoifanya. Kama safari hii sisi mmetupa nafasi ya kuwasha mwenge katika Mkoa wetu wa Katavi, tumepata manufaa na mafanikio makubwa, naomba niwapongeze sana.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze Mawaziri, mnyonge, mnyongeni lakini haki yake mpeni. Mawaziri wetu mnafanya kazi kubwa sana, mnatembea usiku na mchana kwa ajili ya nchi yenu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye elimu ya msingi. Serikali imefanya jitihada kubwa, imeondoa kero ya Watanzania na watoto wetu wanasoma bure. Vilevile kulikuwa kuna changamoto ndani ya shule zetu za misingi tulikuwa hatuna madawati lakini Serikali ilifanya jitihada kubwa kutafuta madawati pamoja na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi, wote kwa ujumla wakachangia, sasa shule zetu zina madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini bado tuna tatizo moja kubwa sana ndani ya shule zetu za misingi la vyumba vya madarasa. Sasa hivi kutokana na elimu bure, wazazi wengi wanaenda kuandikisha watoto ili waweze kusoma na kupata elimu ya msingi. Unakuta takibani watoto 1,000 darasa la kwanza hawana sehemu ya kusomea, sehemu nyingine watoto wamepangiwa madawati nje wanasoma. Maeneo yetu kama Mkoa wa Katavi ni ya mvua, mvua ikinyesha wale watoto hawapati elimu, inabidi watawanywe warudi nyumbani.
Mheshimiwa Spika, kwa vile hii ni changamoto, tunaomba Serikali ipange mpango mkakati kuhakikisha tatizo hili linashughulikiwa. Wananchi wanajitoa kwa hali na mali kuchangia elimu. Unaenda unakuta wananchi wamejenga madarasa, wengine wamemaliza wengine uwezo wao wanafika kwenye lenta. Tunaomba Serikali ipange mkakati mpana kwa ajili ya kuongeza madarasa katika shule zetu. Tunapongeza kwa jitihada kubwa wanazofanya lakini inabidi mpango mkakati uwe mpana zaidi ili watoto waweze kupata sehemu ya kusomea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye elimu ya sekondari. Katika hotuba ya Waziri Mkuu ameelekeza wananchi wahamasishwe ili watoto waweze kusoma sayansi. Ni kweli, shule zetu nyingi za sekondari walimu wa sayansi hatuna, wako wachache sana. Unakuta shule ya sekondari ina mwalimu mmoja wa sayansi au hakuna kabisa, watoto wengi wanajielekeza kwenye masomo ya biashara. Tunaomba Serikali iwaajiri walimu wa sayansi ili waweze kwenda kwenye shule zetu za kata kwa sababu ndizo wananchi wengi watoto wao wameenda kusoma huko ili
tuweze kuibua walimu wa sayansi na vipaji vipya. Kuna shule baadhi kama kwetu Shule ya Usevya ina walimu wachache sana wa sayansi lakini wamesaidia kuibua wale watoto wa Form V au Form VI wanatoka wanaenda kusaidia kufundisha wanafunzi sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee maji vijijini. Hakuna Mbunge atakayesimama hapa asizungumzie maji kwa sababu tunavyoenda huko vijijini tunaona hali halisi. Serikali ilifanya jitihada kubwa ya kuchimba visima virefu na vifupi. Hata hivyo, kuna sehemu nyingine watalaam walienda kuangalia wakaona kabisa hapa pana maji lakini walipochimba yale maji yakapotea kutokana na hali halisi sasa hivi Watanzania wengi wanakata miti, wanaharibu sehemu nyingi ambazo maji yanatokea, unakuta kunakuwa kuna ukame mwingi. Naomba Serikali ijipange vizuri upande wa maji. Vijijini wananchi hawana maji kabisa. Unakuta kijiji hakuna hata kisima kimoja. Mwananchi anatoka maeneo husika anaelekea maili 20 au 30 kwa ajili ya kutafuta maji. Tunaomba Serikali ipange mkakati mpana kwa ajili ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunaipongeza Serikali kwa ajili ya maji mijini. Mamlaka za Maji Mijini zinajitahidi, miradi mbalimbali inaelekezwa huko. Tunaomba Serikali, kuna miradi ambayo ipo lakini bado wale wakandarasi hawajaweza kulipwa pesa zile wanazodai. Tunaomba wawalipe
wakandarasi ili waweze kutimiza miradi ile ambayo iko kwenye Mamlaka ya Maji Mijini.
Mheshimiwa Spika, Hospitali yetu ya Wilaya ya Mpanda ilikuwa haina duka la dawa lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyofika alielekeza na leo hii tunajivunia Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mpanda tuna duka la dawa, tunapongeza sana. Hata hivyo, kuna tatizo kidogo, dawa zinakuja chache. Tunaomba dawa na vifaa tiba viongezeke ili wananchi waweze kupata huduma safi na salama kwa ukaribu zaidi.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze kwa Kituo cha Afya Kalema kupata gari na sasa hivi tumepata chumba cha upasuaji, akinamama pale wanazaa kwa uzazi salama zaidi. Pia Tarafa ya Mishamo tuna Kituo cha Afya ambacho upasuaji unafanyika na vilevile tumepewa gari. Bado tarafa nyingine tunahitaji mtufikirie tuweze kupata vyumba vya upasuaji na vilevile tuweze kupata magari ya afya kwa sababu kutoka kwenye tarafa mpaka mjini ni mbali.
Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Serikali, najua Wabunge wa Katavi wengi wanasema hili, sisi Mkoa wetu wa Katavi tuna uwanja mzuri sana Serikali mlitujengea. Naomba tuipongeze Serikali kwa kutujengea ule ule uwanja. Tuna ndege ambazo tumenunua ndani ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Tunaomba basi na sisi Mkoa wa Katavi tuweze kupata huduma hiyo ya ndege hata moja, katika route yoyote ile inayoenda Tabora au Kigoma ili wananchi wa Katavi nao waweze kufurahia matunda ya Serikali yao ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna Ziwa Tanganyika ambalo linapita Ikola na Kalema. Kuna hii meli ya MV Liemba ina miaka 110… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Spika,
tunaomba Serikali ijenge meli hii kwa sababu sisi wa Mkoa wa Katavi inatuhusu kupitia Ikola na Kalema. Tunaona meli
nyingi zinajengwa…
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.