Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah- Wataallah aliyetujalia uzima na afya njema katika miezi hii mitukufu tunayoendanayo; na wale wanaofunga inshallah Mwenyezi Mungu awabariki na funga zao azikubali.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Mtambile kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, lakini hasa pale ambapo Katibu Mkuu, kipenzi chetu, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye alikuwa akipita katika ziara zake za kuongoza chama chetu. Hongera wananchi wa Jimbo la Mtambile, hongera Katibu Mkuu Mstahiki Maalim Seif Shariff Hamad, wewe ni kiboko ya viboko, tuendelee na kazi, hakuna Katibu Mkuu mwingine mpya. Ni wewe tuliyekuchagua katika Mkutano Mkuu mwaka 2014, hakuna Mkutano mwingine Mkuu uliofanyika. Chapa kazi Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad, songa mbele, aluta kontinua.
Mheshimiwa Spika, la pili. Naomba niendelee. Kwenye ukurasa wa 10 wa Kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kupata viti 19 vya Udiwani katika chaguzi zilizopita.
Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Chama cha Mapinduzi kilipata pigo, kilishindwa vibaya katika uchaguzi wa marudio wa Lindi Mjini; mitaa yote saba Chama cha Wananchi – CUF kilishinda. Naomba, hawa ni jirani zako, CCM ilipata kipigo
kitakatifu; CCM ilishindwa vibaya na wananchi walisema hiyo rasha rasha tu, 2020 ndiyo muziki hasa. Hawa jirani zako lazima ilikuwa uwakumbuke kwamba CCM ilipigwa vibaya Lindi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze mitaa ambayo ilishinda katika Mitaa ya Mnubi, Migombani, Ndolo Juu, Mnazi Mmoja, Nachingwea, Tulieni na Runyu. Mitaa yote saba hii ilichukuliwa na Chama cha Wananachi – CUF kama taasisi. Hongera sana wananchi wa Lindi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mambo ambayo tunakwenda nayo naomba niseme kwamba, Serikali kwa wakati huu haioneshi wazi kwamba ina dhamira ya kuleta maendeleo. Kwa sababu, hata pale ambapo bajeti imepangwa itekelezwe, basi imekuwa ni kizungumkuti.
Mheshimiwa Spika, ni aibu na fedheha iliyotosha kwamba hadi hivi sasa bajeti ya maendeleo ambayo imeletwa ni 34% tu, hii ni aibu. Tena na bajeti hiyo, kinachosikitisha ni kwamba ilikuwa ni bajeti ya shilingi trilioni 29, mara hii Serikali imeleta bajeti ya trilioni 31, miezi iliyobakia ni mitatu wanasema kwamba fedha zilizobakia eti wataweza kuzileta. Hiyo miujiza itatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikiwa miezi tisa Serikali haikuweza kukamilisha fedha za 100%, eti miezi hii iliyobakia mitatu watakamilisha bajeti ya 66%. Ni aibu na fedheha kwa Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba, katika hili, jambo ambalo linatushangaza hata bajeti yako ya Bunge, bajeti ya maendeleo 2016/2017 ilikuwa ni bilioni saba, hadi leo ninavyojua, labda wameweka fedha jana au mchana huu, wametoa shilingi milioni 200 tu. Aibu na fedheha iliyotosha.
Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa kwamba Serikali haina dhamira iliyo wazi; ukiangalia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali bajeti iliyopita alitengewa fedha za maendeleo shilingi bilioni 10, lakini amepata shilingi bilioni 2.4 tu. Tena asilimia 90 ya fedha hizi, ni fedha za wafadhili. Ni aibu kwa Serikali inayosema hapa kazi na mwendokasi. Kasi iko wapi? Kutakuwa na kasi kweli mwaka huu hapa! Hii ni fedheha na aibu kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba wakati sisi Wabunge tunapitisha bajeti za maendeleo Serikali iwe makini kuangalia ni jinsi gani ambavyo fedha za maendeleo zitatolewa kwa wakati, vinginevyo ni aibu na fedheha kwamba tunapitisha bajeti za maendeleo, lakini Serikali
inaendelea kutumia fedha za maendeleo kwa mambo ambayo Wabunge hatukupitisha. Ni jambo baya sana.
Mheshimiwa Spika, nini athari yake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali? Ni kwamba hapewi fursa iliyo nzuri kuangalia miradi mbalimbali ili kuanika uozo na uovu ambao unaonekana kwenye Serikali. Huu ni mkakati maalum wa Serikali kwamba mnamdhibiti asifanye kazi zake vizuri kwa sababu mnajua kuwa kwenye Serikali kuna maovu yaliyo mengi. Hii ni aibu na fedheha kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali ikubali ushauri kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali apewe fedha inayostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aibu nyingine na aibu iliyoje, katika miaka kadhaa iliyopita sisi vyama vya siasa tumekuwa tukilelewa na mtu anayejulikana kama Msajili wa Vyama vya Siasa. Leo Msajili wa Vyama Vya Siasa amethubutu na kutoa ruzuku shilingi milioni 369 kwa akaunti isiyostahiki. Mbaya zaidi imekwenda mbali zaidi, huu ni ufisadi wa hali ya juu, fedha hizi kwenda katika benki isiyostahiki, NMB, baadaye fedha hizi kuhamishwa kupelekwa kwa mtu binafsi, fedha hizi zikatumika isivyo. Hii ni kama Escrow! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa na fedheha. Kama taasisi naiomba Serikali iangalie sasa fedha za Msajili wa Vyama vya Siasa zinatumikaje? Hii ni aibu na fedheha kwamba fedha unazipeleka katika akaunti isiyostahili, baadaye fedha zinachukuliwa zinapelekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi; zinachukuliwa zinatumika visivyo na bado Serikali ipo inachekacheka tu! Tatizo nini kwa Serikali? Aibu kwa Serikali inayosema Hapa Kazi na Mwendokasi. Kama kasi ndiyo hii, aibu kubwa! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, aibu nyingine ambayo inakuja, Serikali inasema tuko katika mkakati wa uchumi wa viwanda, lakini siyo muda mrefu Kiongozi wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe amesema hapa jinsi gani ambavyo fedha za viwanda zilivyotolewa asilimia ngapi ya fedha za Wizara ya Viwanda. Kama kweli tuna nia nzuri, inakuwaje hadi leo unaendelea kutoa 8% ya fedha za viwanda? Serikali ambayo inasema
tunaelekea katika uchumi wa viwanda! Hiyo ni aibu nyingine.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwa kusema kwamba ndani ya uchumi wa viwanda tuna sababu gani ya msingi, baadhi ya viwanda vilivyopo, baadhi ya wafanyabiashara bado wanaagiza baadhi ya bidhaa kama ngano kutoka nje? Leo viwanda hapa vipo. Kuna kiwanda
cha ngano cha Bakhresa, lakini 90% Bakhresa anaagiza kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, hapa Serikali kazi yake ni kuchukua mikasi kukata utepe, ati mnazindua viwanda. Kazi gani! Njombe ngano inastawi, Iringa ngano inastawi, maeneo mengine ngano inastawi, lakini 90% ya ngano ya Bakhresa inatoka nje. Sisi kazi yetu ni kutembea na mikasi tu,
tunazindua viwanda. Si aibu hiyo! Aibu kubwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naliona, tunazungumza habari ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); tumeshuhudia kwamba wakati wa ukame Serikali ina mpango wa kudhibiti na kuweka chakula kwenye ghala la chakula – NFRA.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini tunaona mifugo yetu inakufa kwa kukosa majani au nyasi wakati tungeweza kuweka mkakati wa udhibiti katika maeneo mbalimbali ili hawa ng’ombe wetu wapate nyasi za kutosha? Hivi jamani hata hilo linahitaji mshauri mwelekezi kutoka nje?
Mheshimiwa Spika, ukienda katika mapori mbalimbali wakati wa ukame, unaona jinsi gani ambavyo ng’ombe wamekufa, lakini kumbe tuna nyasi za kutosha katika mikoa mbalimbali. Hili ni jambo ambalo Serikali ni lazima mliangalie. Sasa huo mkakati wa kupunguza umaskini uko wapi kama wafugaji wameachwa ng’ombe wao wanakufa, lakini nyasi kumbe zipo?
Mheshimiwa Spika, nchi nyingine duniani wanafanya hivyo, wanavuna nyasi, wanavuna yale majani wanayaweka kwa wakati maalum na wakati ukifika ule wa ukame ng’ombe wanapatiwa majani na wanakula, hawafi. Binadamu Tanzania wana njaa, ng’ombe wana njaa; shida
kweli! Hapa kazi kweli mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwa Walimu. Walimu mara nyingi wamekuwa na malalamiko yao na mara nyingi Walimu wamekuwa wakipuuzwa.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Walimu madeni yao yanayostahili hawalipwi kwa wakati, ndio maana Walimu wanakuwa ni maskini. Walimu wana malalamiko mengi, lakini kwa sababu inaonekana labda watu hawaelewi maana ya Ualimu; Mheshimiwa Simbachawene herufi ‘U’ maana yake ni uvumilivu. Kwanza ni usumbufu; “A” maana yake ni adha wanayopata walimu; ‘L” ni lawama wanazopata walimu. Inda, mahangaiko, mwisho ni uvumilivu na umaskini… (Hapa kengele ilila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, naomba walimu wapewe stahiki zao zinazostahili. Nakushukuru sana.