Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

Hon. Godbless Jonathan Lema

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ili kuepuka miongozo mingi naomba nianze na neno la Mungu kutoka kitabu cha Ufunuo mstari wa nane, inasema “bali waoga, na wasioamini na wachukizao na wauaji na wazinzi na wachawi na hao waabuduo sanamu
na waongo wote sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto wa kiberiti.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu waoga, Biblia imewafananisha na wazinzi; watu waoga biblia imewafananisha na wanaoabudu sanamu; watu waoga
Biblia imewafananisha na waongo na biblia ikasema hawa hukumu yao ni ziwa la moto.
Mheshimiwa Spika, nilipokuwa Magereza nimekuombea sana, Mungu ni shahidi. Ili Bunge hili liweze kutenda haki, wale watu waliotajwa hapa kama wapo, wakatae kufanishwa na wazinzi na waabuduo sanamu.
Mheshimiwa Spika, nchi hii inapokwenda, kama leo Bungeni pasipokuwepo na uhuru wa majadiliano wananchi wataongelea wapi? Tukiongea nje, tunakaa ndani, tunanyimwa dhamana, tunapelekwa Magareza kwa miezi minne. Tukiongea Bungeni haturuhusiwi. Leo haturuhusiwi
kuisema Ofisi ya Rais, mnafikiri mnamsaidia Rais! Ipo siku atatafuta watu makini. Huko mlikuwa wengi sana, wengine sasa hivi wako huku. Atatoka mmoja mmoja na wote mtakuja huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namna ya kuisaidia nchi ni watu kutokuwa waoga. Ni watu kusema ukweli! Leo Taifa linayumba! Hakuna mtu ambaye hakuona Siku ya Sheria Duniani, lakini hapa kila mtu anatetea chakula, anatetea mshahara kuliko utu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watoto na wajukuu wa Taifa hili wanaangalia kizazi cha Bunge hili kinatunga Sheria za aina gani? Maombi yangu ni kila Mbunge angalau apite jela kwa miezi minne ili mjue ninachokisema.
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Waheshimiwa Wabunge tuisaidie nchi. Kuna siku mke wangu alikuwa anawaambia wanangu, nataka msome sana muwe kama profesa. Mtoto wangu mmoja akamwuliza, kama profesa nani? Mke wangu akasema ngoja ni-google!
Mheshimiwa Spika, tunataka Madaktari na Maprofesa walioko ndani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi wawe mashuhuda wa kupigania haki ya Taifa hili. Leo msiporuhusu mijadala huru ambayo imeruhusiwa na Katiba hii kwa Wabunge, ndani ya Bunge, tunaenda kuongelea wapi
mambo ya kulisaidia Taifa hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Hussein Mwinyi ni mtoto wa Mzee Mwinyi; baba yake leo ana faraja mtoto wake ni Waziri yuko Bungeni. Ben Saanane ni mtoto wa Mzee Focus; Ben Saanane amepotea, hajulikani alipo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imemtafuta Faru John kwa gharama zote; imemtafuta Faru John kwa nguvu zote; kuna mtoto anaitwa Ben Saanane, ana wazazi kama ambavyo Mzee Mwinyi ana mtoto anaitwa Hussein; kama ambavyo Mzee Maghembe ana mtoto wake, juzi tumemchagua kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, akampa mkono akifurahi; leo kuna binadamu ana ndugu zake, ana wadogo
zake anaitwa Ben Saanane; baba yake aliniambia maneno haya, “CHADEMA na Serikali nisaidieni kumtafuta mtoto wangu. Ben sio mbuzi wangu, Ben ni mtoto wangu.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imemtafuta Faru John. Leo nimeshangaa yaani wanyama wamekuwa na hadhi katika Taifa hili mpaka leo kuna mnyama anaitwa sijui Yusta na mnyama mwingine anaitwa Ndugai, wewe mwenyewe! Aisee! I am wondering! Yaani mpaka leo wanyama
wanakuwa na thamani mpaka wanabatizwa majina ya binadamu na kuna mtu anapotea hapatikani.
Mheshimiwa Spika, Mawazo aliuawa, Geita. Mawazo ameuawa Geita, mahabusu wale wakalala barabarani wanasema Serikali ilete viongozi wakubwa tuwaambie watu waliomuua Mawazo. Serikali haikuchukua hatua. Faru John ametafutwa kwa nguvu zote. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, kuna maiti Ruvu, nilikuwa Magereza nasoma kwenye magazeti, saba; DNA yake haijapimwa, taarifa yake haijatolewa, lakini Faru John na Faru mwingine sijui Yusta sijui nani, ametafutwa kwa nguvu zote.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, haya mambo yanayoendelea mnakaa kimya; mnasikia mtu amepotea mnakaa kimya; mnasikia kuna damu imemwagika mnakaa kimya; mnafikiri hao sio watu; hii damu itanena. Hii damu itanena! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yaliyomkuta Mheshimiwa Nape juzi, yametukuta sisi siku za nyuma, yatamkuta kila mtu. Kama ambavyo wema ni mbegu, ubaya pia ni mbegu, kila mtu anavuna anachopanda. Wakati utafika, leo mko wengi, tulitarajia nyie ndio msaidie Taifa hili kwenda mbele.
Mheshimiwa Spika, leo alikuwepo Mwalimu Mwakasege hapa, wakati tunasali tukawa tuko na Wabunge wa CCM wengi tu, nami nilikuwa karibu na Mheshimiwa Juliana Shonza. Nikafumbua macho kidogo nikaona Wabunge tunasali kwa pamoja. Nikasema hivi zile kura za hapana hawa hawakuwepo! Nikasema hawa kwenye kura za hapana hawakuwepo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi hii isipoacha usiasa ndani ya Bunge, upande huu na upande huu, tusipoacha siasa za vyama ndani ya Bunge, Taifa hili tunalipasua! Leo inaonekana Vyombo vya Dola vina nguvu, leo inaonekana mna majeshi. Tumeongea habari ya Mahakama hapa mkasema tusiingilie Mahakama.
Mheshimiwa Spika, mimi nilishawahi kupewa mdhamana na ikasainiwa remand order. Nimekaa jela miezi minne, nina dhamana lakini sina masharti ya dhamana. Hakimu aliyefungwa mikono kuninyima masharti ya dhamana, alifunguliwa mikono kutoa masharti ya dhamana.
Tunapokuja kuongea habari ya Mahakama, hamwezi kujua vizuri mpaka mwende jela.
Mheshimiwa Spika, nimetoka jela, kuna mtu yuko jela mwaka wa tatu kwa kesi ya bangi ambayo akienda akaplead guilty Mahakama Kuu faini yake ni 18,500/=. Kuna Mwanasheria, Mheshimiwa Mwakyembe anamjua, amekaa jela anaanza mwaka wa saba, kesi yake ni money
laundering. Miaka saba! Hiyo kesi akikutwa na hatia pengine ni miaka minne jela. Kuna watu wanaozea jela. Ofisi ya DPP inatumika vibaya, tumetunga kesi mbaya. Nenda Keko, zimejaa watu kesi za money laundering. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hasira inakusanyika kwenye mioyo ya watu. Hamuwaoni watu wanaandamana barabarani, watu wanaandamana ndani ya mioyo. Ipo siku watatoka barabarani bila sauti ya CHADEMA! Iko siku watatoka barabarani bila sauti ya CUF! Iko siku mtawakuta
barabarani!
Mheshimiwa Spika, Taifa hili litapasuka vipande viwili! (Makofi). Mheshimiwa Spika, huu uonevu mnaotufanyia, hatufanyi mikutano ya hadhara leo. Leo mkutano wachadhara nchi hii tumekatazwa…
SPIKA: Mheshimiwa Lema, muda hauko upande wako. Muda, muda, umekwisha.
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Spika, nina dakika zangu mbili, nilikuwa naangalia hapa. Dakika zangu mbili.
Mheshimiwa Spika, leo tumezuiwa kufanya mikutano ya hadhara. Tunaambiwa tufanye mikutano ya hadhara 2020. Ni sawa na kuliambia Kanisa lifanye Ibada Christmass. Ni sawa na kuuambia Msikiti ufanye Ibada Siku ya Idd! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nyie mnafikiri ni kwetu, wakishamaliza kutushughulikia sisi, meno yale yale, msumeno ule ule, utakuja upande wenu. Ngoja watumalize kwanza, utakuja upande wenu. Nawaambia, kila mbegu mnayopanda mtavuna na tuko kushuhudia haya na Mungu ni shahidi. (Makofi).
Mheshimiwa Spika, ahsante.