Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na afya tele. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kwa kunileta humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze kabisa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa, nami nimeisoma mwanzo mwisho. Nasema mimi nitakuwa wa kwanza na naendelea kuwa wa kwanza kumuombea aishi maisha marefu, awe na afya njema lakini pili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri na mimi nitamsaidia kwa asilimia mia moja kwenye eneo ninalohusika kule Jimboni kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana na yeye mwenyewe kumtegemea Mungu kwenye kazi zake ambazo wananchi wa Jimbo langu wanaziona na watu wa Mungu wengi tunamuombea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie maeneo machache hasa kwenye ukusanyaji wa kodi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha makucha yake kwenye eneo ambalo linaonekana kuna tatizo la ukusanyaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna jambo ambalo kimsingi naomba niliseme hapa leo kuhusu barabara au miundombinu. Kule kwetu Mbulu ni Wilaya iliyoanza tangu mwaka 1905 lakini hatujawahi kabisa kuiona barabara ya lami. Ukitaka kumfundisha mtoto leo kuhusu barabara walimu wanapata shida, ni lazima amtoe mtoto nje ya Wilaya ampeleke Babati au Karatu ili kuweza kuona mfano wa barabara ya lami. Namshukuru Mungu barabara hii ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu. Kwa kuwa Rais ameiahidi barabara hii, niombe sana Wizara hii ya Miundombinu iiangalie maana barabara hii ni muhimu sana kwetu ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na mkoa wetu, kutoka Karatu – Mbulu, Mbulu- Hydom, Hydom –Singida, kilomita 180 zimeandikwa pale. Namuona Mama Nagu akiniambia eleza na ile ya kwangu, mama nitafika huko. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni inayotoka Babati - Dongobesh pale kuna kilomita 63. Bila kuisahau barabara ya Mbuyu wa Mjerumani, Magara kufika Mbulu Mjini na hii ya Hanang kuja Hydom. Tukipata barabara hizi zitatusaidia sisi ambao ni wakulima wa vitunguu pale Mbulu Bashay. Vitunguu hakika vina soko maeneo mengi na eneo maarufu ni pale kwetu Bashay ambapo vitunguu vile zinauzwa maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Zanzibar na Uarabuni. Barabara hii itasaidia sana kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo yale na kupunguza pia umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, pamoja na ahadi kubwa ambayo tumepewa mara nyingi na Mheshimiwa Rais wetu wa awamu uliyopita lakini naamini kabisa Mheshimiwa Rais huyu wa Awamu ya Tano ambaye leo nampongeza hapa kutokana na hotuba yake, yako mabwawa makubwa ambayo yamejengwa pale Dongobesh. Naamini ahadi aliyotoa siku ya kampeni pale Dongobesh ataitekeleza. Kwa nini nasema hivyo? Kilimo chetu sasa kimeingiwa na ukakasi wa ukame lakini tukipata namna ya kutengeneza mabwawa na kuyakinga maji yanayopotea hasa kipindi hiki cha mvua nyingi, mabwawa haya yakiwa tayari yanaweza kusaidia sana kilimo cha umwagiliaji na tukavuna mara mbili kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwaa Mwenyeki, najua eneo langu la Mbulu Vijijini, hakika lina changamoto nyingi. Changamoto ya maji ni kubwa mno. Nashukuru Mheshimiwa Rais ameahidi kupatikana kwa maji katika Mji Mdogo wa Hydom, Dongobesh, Bashay na maeneo mengi ya Laabay. Nina hakika nchi nzima tuna tatizo la maji lakini nafikiri Waziri amekwishakuniahidi miradi iliyotengenezwa au iliyofadhiliwa na World Bank ambayo imesimama katika maeneo hayo itafanyiwa kazi. Mbulu tunahitaji shilingi bilioni tatu tu ili kuweza kumaliza miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna tatizo moja kubwa mno nalo ni umeme vijijini. Mimi nasimama hapa naweza kuwa ni Mbunge wa sita Wilayani Mbulu Vijijini lakini tangu zamani mpaka leo tuna kata tatu tu ambazo zimeweza kupata umeme. Tumeleta maombi na Mheshimiwa Waziri Muhongo ni jembe na nimeongea naye na napenda kumhakikishia atakapofika kule nitamtembeza maeneo mengi sana. Kwa kuwa najua wewe ni jembe utafika maeneo hayo na nakukaribisha sana maeneo ya Maretadu, Tumat, Bashay, Maseli na naeneo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wangu umekuwa mdogo, naomba sasa nishukuru hasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, dada yangu Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama. Juzi wananchi wangu walipata njaa hasa Wahadzabe wa Eda Chini, umewasaidia tani 400, zimekwenda kule, zimesaidia Wilaya nzima, nakushukuru sana, hili lazima niliseme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sitendi haki kama sijasema jambo linaloniuma moyoni. Mwenge wa Uhuru ni jambo imara sana. Mwenge huu aliuanzisha Baba wa Taifa, ni ishara kubwa sana na una maudhui ya kutosha. Mimi kama nisingekimbiza mwenge nisingewajua watu kutoka Zanzibar, tusingekuwa na umoja, nimefahamu nchi hii kwa vile nilitembea sana na mwenge. Nasikitika sana kusikia watu wanasema tuufute mwenge. Kama tatizo ni gharama tutafute namna nzuri ya kuupeleka mwenge bila gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana mwenge umewekwa katika maeneo mengi ya nchi hii na kuna siri kubwa. Viongozi wa majeshi yote nchini wale wenye wenye vyeo vikubwa, vyeo vyao vina alama ya mwenge. Hata motto wa Mheshimiwa Rais wetu wa Hapa Kazi Tu kuna alama ya mwenge. Leo unafutaje kiholela namna hii jambo ambalo Baba wa Taifa amelianzisha?
Mimi nisingewafahamu akina Mwashibanda, Vuai wa kule Zanzibar ni kutokana na kutembea na mwenge. Mwenge unaleta umoja, amani na unamulika mafisadi. (Makofi)
Namuomba Mheshimiwa Rais auongezee nguvu Mwenge wa Uhuru ili uweze kufanya yale ambayo yametokea wakati sijazaliwa, ing‟oe mafisadi, ilete amani na imulike hata nje ya mipaka yetu kama inavyofanywa na ilete tumaini mahali ambako tumaini halimo. Najua wengi watapiga vita sana jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala moja tu, ninaomba niishauri Serikali hii inayoingia sasa tunayo manpower Tanzania yaani idadi kubwa ya watu, China wanatumia idadi yao kubwa kuzalisha. Sisi inabidi kwa kweli Serikali ilete sheria hapa Bungeni, zamani kulikuwa na kitu, watu wanakamatwa wanapelekwa sehemu ambayo nilikuwa siijui, nimepata kwenye historia ya Gezaulole sijui ni wapi huko! Vijana wanaokutwa wanahangaika wanapelekwa Gezaulole, leo vijana wengi tunacheza pool kuanzia asubuhi, bao na karata. Ni lazima kutumia nguvu yetu kuzalisha uchumi kama wa China ili uweze kuendelea na uchumi huu uweze kutusaidia sisi vijana tunaokua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kabisa hotuba hii na kumpongeza na Mheshimiwa Rais, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)