Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: …..watu 20,000 wapelekwe kule wanafunzi waweze kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chuo kikuu kingine napendekeza kijengwe Mtwara kwa ajili ya Mikoa ya Kusini. Na Chuo Kikuu cha Lake Tanganyika ama kijengwe Katavi au Kigoma au Tabora kwa ajili ya Mikoa ya Magharibi; hapa tutakuwa tumejenga uwezo wa kuwa na watu 60,000 zaidi kwenye vyuo vikuu vya umma na tukitanua vyuo vikuu ambavyo tunavyo sasa hivi, uwezo wa wanafunzi wote wanaostahili kuingia kwenye vyuo vikuu vya umma utakuwepo na hivyo tutaweza kuhakikisha ya kwamba tunaondokana na tatizo kubwa la ubora kwenye vyuo binafsi, ambalo tunalo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninalipendekeza, na hili ni kwa Kamati zote ni kwamba Kamati zinatoa maoni yao hapa na mapendekezo, mapendekezo yanapitishwa. Mfumo tulionao hivi sasa na mapendekezo haya kufuatiliwa na Kamati yenyewe, na kulingana na wingi wa kazi za Kamati jambo hili limekuwa halifanyiki. Wabunge ambao ni wazoefu wa muda mrefu wanafahmu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na Kamati Maalum ya Bunge ya Ufuatiliaji wa Mapendekezo ambayo yanakua yametolewa na Kamati za Bunge. Vinginevyo tutakuwa tunaongea hapa tunaonekana kama tunaimba tu. Kila mwaka tutakuja tutapokea taarifa, tutakuwa kama tunaimba tu na hatutakuwa na msaada wowote ambao tunakwenda nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka kulizungumza lipo kwenye Kamati ya UKIMWI. Kamati hii imeshughulikia suala ambalo sasa hivi ndiyo ajenda. Sasa hivi kila mtu anazungumzia vita dhidi ya dawa za kulevya, ambayo imeanzishwa na mmoja wa Wakuu wa Mikoa hapa nchini katika eneo lake, lakini imekuwa kama vita ya kitaifa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Waheshimiwa Wabunge wakijielekeza kusoma kwenye ukurasa wa 11 wa Taarifa ya Kamati ya UKIMWI, imeeleza kinagaubaga kwamba, mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya ambayo imeundwa kutokana na Sheria ya Bunge hapa haipewi uwezo kabisa wa kufanya kazi. Kwa hiyo, hata tukiendesha kampeni hizi namna gani, kila mtu atakuja na kampeni yake, lakini hatutaweza kuzifanya kampeni hizi kuwa endelelevu kwa sababu, vyombo ambavyo tumeviweka kwa ajili ya kupambana na tatizo hili sisi wenyewe hatuvipi uwezo wa kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ina ajenda ya kubana matumizi. Inabana matumizi mpaka kwenye vyombo ambavyo vinapaswa kufanya kazi ambayo sasa yanatoka matamko ambayo dhahiri kabisa yanaenda kinyume na mfumo wetu wa utoaji haki. Sasa jambo hili tusiliangalie kishabiki, tusiangalie ni mtu gani amesema, amepingwa na nani anaungwa mkono na nani, tutakuwa tunakosea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi hii kwa mujibu wa Katiba, you are innocent until proven guilty. Tunachojengewa sasa hivi moja ni kwamba once you are accused you are guilty, hili ni tatizo na hili ni tatizo ambalo Bunge hili lazima ilikemee, kwa sababu Waheshimiwa Wabunge hii ni kama mtego wa panya huu, leo hii kuna watu wamekamatwa, kesho Mkuu wa Mkoa mmoja ana chuki na Mbunge anasema nenda karipoti polisi una dawa, utasema nini? Na sisi kama hatukusimama kuhakikisha kwamba mfumo wa haki unafanya kazi hakuna atakayesimama kututetea atakapotufikia sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana, kwanza hakuna mtu anayeweza kuthubutu kukataa kwamba tuna tatizo la dawa na ni lazima kulifanyia kazi, hakuna mtu ambaye anakataa. Lakini ni lazima sisi kama watunga sheria, sisi kama wasimamizi wa Serikali tusimame kidete tuseme kwamba ni lazima taratibu zetu za kisheria na Katiba ziweze kufuatwa, na hii itatusaidia sana. Maana matamko ambayo wakati mwingine yanaweza kuwa ni matamko ya kawaida yanatoka lakini madhara yake yanakuwa ni makubwa sana katika vita yenyewe ambayo tunakuwa tunapambana nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi rai yangu, na mengine nimeyotoa kwa maandishi kwa sababu nilidhani kwamba muda utakuwa ni mfupi sana; rai yangu kubwa ni hiyo; na kwamba kama vita hii ni vita ya zaidi ya mkoa mmoja, basi vita hii iendeshwe na viongozi wa kitaifa wenye mamlaka katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Kigoma kule huwa tuna msemo, “ukiona kifaranga yuko juu ya chungu ujue chini kuna mama yake. Tukiendekeza hali hii tutakuja kupata matatizo makubwa sana; tulaani, lakini tuhakikishe haki inatendeka. Tushiriki kwenye kupambana, lakini tuhakikishe haki inatendeka. Hata siku moja tusionee mtu wala tusimfanye raia yeyote nchi hii aonekane kwamba anaonewa kwa sababu yeye hana madaraka, kwa sababu yeye ni mnyonge, kwa sababu yeye hana vyombo vya ulinzi na usalama vya kuweza kuagiza na kufanya vitu ambavyo anaweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi yangu ni hayo. Nakushukuru sana.