Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo matatu. Nitazungumzia suala la madawa ya kulevya lakini nitazungumzia hali ya usalama hasa Zanzibar na muda ukipatikana nitamalizia na suala la magereza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nilieleze Bunge hili Tukufu kwamba kuna kazi kubwa sana ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikiifanya, imefanya na inaendelea kufanya katika kukabiliana na janga hili la madawa ya kulevya katika nchi yetu. Yapo mambo yameendelea kufanyika waziwazi na yapo mambo ambayo yamefanyika kimya kimya hayajulikani na mengine hayatajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika haya mapambano ya dawa za kulevya, nataka niwahakikishie kwamba tunaendelea vizuri na imani yangu ni kwamba kwa mwelekeo huu tunaoenda nao tunaelekea kushinda na hatutarudi nyuma. Silaha yetu kubwa ni dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. Wewe na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi wakati Mheshimiwa Rais alivyokuja kuzindua Bunge hili alizungumza kwa msisitizo na toka wakati ule mambo mengi na makubwa yamefanyika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja ya msingi ni kwamba tumefanikiwa kiasi gani, changamoto ni zipi na tunaelekea wapi. Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, ni watumiaji na wauzaji wa madawa ya kulevya wakubwa, wa kati na wadogo wengi ambao wamekamatwa na wengi kesi zao zinaendelea na wapo wengi ambao wameshafungwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima tukiri kwamba kulingana na mabadiliko ya mfumo wa kidunia zamani nchi yetu ilikuwa inatumika kama ni eneo la kupitishia madawa ya kulevya lakini sasa hivi ongezeko la matumizi ya ndani la madawa ya kulevya limekuwa ni kubwa. Madawa ya kulevya yanatumika hovyo, hilo lazima tukiri kama ni changamoto. Changamoto hii Serikali hatuwezi tukaifumbia macho na ndiyo maana tumebadilisha style ya kukabiliana na matatizo ya madawa ya kulevya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu hapa katika ziara zake nyingi Mheshimiwa Waziri ambazo amekuwa akifanya mara ya mwisho alikuwa Ifakara amezungumzia hilo, ametoa mwelekeo huo na mimi nilikuwepo Mbeya takribani wiki mbili zilizopita kabla hata ya operesheni moja haijafanyika ikiwemo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tumewaelekeza ma-RPC kwamba kwa uzito wa tatizo la madawa ya kulevya katika nchi yetu, tuliwaelekeza Mbeya tukawaambia wafanye operesheni kabambe kabisa na wakafanya operesheni kali sana wakawakamata watumiaji wa madawa ya kulevya na wauzaji. Wale watumiaji wa madawa ya kulevya ndiyo waliotusaidia kuweza kuwapata wale ambao wanashughulika na kuuza madawa ya kulevya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, tulidhamiria kwamba tutumie utaratibu huo ili kuweza kupata taarifa na kuukamata mtandao mzima wa madawa ya kulevya na hatimaye kuangamiza na kupunguza matumizi makubwa ya madawa ya kulevya yaliyopo mitaani. Jambo hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa sana kwa upande wa Mbeya peke yake watu zaidi ya 17 ambao walikuwa either wanatumia au wanauza madawa ya kulevya walikamatwa na kesi zao wengine zinaendelea. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika Wakuu wa Mikoa ambao ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Mikoa yao ikiwemo Mkoa wa Mbeya wameendelea kusimamia hilo na mikoa mingine ikiwemo Dar es Salaam na Shinyanga na kadhalika. Kwa hiyo, tunataka tulihakikishie Bunge hili Tukufu kwamba vita hii ni vita ambayo hatutarudi nyuma na tunaomba ushirikiano wa wananchi na Waheshimiwa Wabunge waliomo humu kuweza kuhakikisha kwamba tunaimaliza. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la usalama wa nchi yetu. Naomba nigusie mambo madogo mawili kwa sababu ya muda. Kumekuwa kuna hoja ya mashaka kuhusiana na majibu ambayo tunatoa kuhusu hali ya ugaidi katika nchi yetu. Naomba nirudie tena kwamba nchi yetu hakuna ugaidi bali kuna vimelea vya ugaidi. Vimelea hivi vya ugaidi havijafanikiwa kuzaa matukio makubwa ya ugaidi kwa sababu ya kazi kubwa ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambayo vimeendelea kufanya katika nchi hii. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachia tukio moja ambalo limewahi kutokea katika miaka ya nyuma ya ulipuaji wa Ubalozi wa Marekani lakini mpaka sasa hivi tumeweza kudhibiti kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo, msimamo wa Serikali ndiyo huo, msimamo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo huo na msimamo wa Wizara ya Katiba na Sheria kama alivyozungumza Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe ni hivyo hivyo hakuna mgongano wowote katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ambalo limezungumzwa sana ni suala zima la hali ya usalama Zanzibar, tusichanganye vitu. Tulichokizungumza ni taarifa ambayo imekuwa ikiletwa hapa na Wabunge mbalimbali, wengine wamekuwa wakisambaza picha kwenye Facebook wakichukua watu wengine hatujui walikuwa wanaumwa malaria au kitu gani wakisema tumepigwa na watu ambao wanaitwa Mazombi. Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasema kwamba Zanzibar hali ya usalama ni shwari na Tanzania hali ya usalama ni shwari. Hata hivyo, kwa kusema hivyo, hatuna maana kwamba hakuna element za uhalifu, wezi, walevi wanaokunywa pombe haramu watakuwepo na kadhalika. Hao watu ambao wanaitwa Mazombi sisi tumesema kabisa kwamba kama kuna mtu yeyote ana taarifa ya watu hawa aiwasilishe katika vyombo vya dola. Mpaka sasa hivi hakuna mtu yeyote ambaye amewasilisha taarifa hii rasmi katika vyombo vya dola na ndiyo maana msimamo wetu unaendelea kubaki pale pale kwamba taarifa hizo kama Serikali hatuna. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa haraka haraka kuzungumzia suala la magereza. Kuna mambo makubwa matatu ambayo tunayasimamia kwa nguvu zetu zote. Jambo la kwanza, kama Mheshimiwa Rais alivyosema kwamba wafungwa wafanye kazi tumelisimamia hilo kwa mafanikio makubwa. Leo tunavyozungumza tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Magereza Ukonga. Katika ujenzi ule tumetumia wafungwa na tumefanikiwa kuokoa fedha ambazo zimewezesha kujenga zaidi ya nyumba 80. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kana kwamba hiyo haitoshi matumizi ya wafungwa yametusaidia sana katika kuweza kufanya kazi mbalimbali za ujenzi katika magereza yetu. Katika Wilaya na Nkasi kulikuwa kuna changamoto sana ya mahabusu. Tulifanya ziara huko hivi karibuni na hivi tunavyozungumza ni kwamba shughuli za ujenzi wa mahabusu katika Wilaya ya Nkasi zinaanza kwa matumizi ya nguvu kazi za wafungwa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja.