Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa napenda nitoe shukrani kwa Wabunge wote waliotoa michango mizuri kabisa na ushauri mzuri. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri, napenda kusema kwamba naunga mkono hoja ya Mpango kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa Pili kwa kweli ni Mpango mzuri iwapo utekelezaji angalau utafikia asilimia 50 au asilimia 80, tunajua inawezekana kwa namna moja au nyingine inaweza isiwe asilimia 100, lakini basi angalau ikiwa asilimia 80 tutakuwa tumekwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu nizungumzie kidogo upande wa viwanda na maeneo mengine, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi tulipokuwa tunainadi wakati tunaomba kura kwa wananchi, tulisema kwamba tutajikita zaidi kwenye viwanda, tutaanzia kwenye viwanda vinavyotumia malighafi tunazozalisha nchini, kwa maana ya mazao yanayotokana na kilimo (Agro Processing Industry). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika agro processing inabidi tujitahidi tujikite tufanye tafiti mbalimbali tuweze kutafuta mbegu zenye tija, kwa mfano, mbegu za alizeti tunazotumia kwa sasa ni mbegu za miaka ya nyuma, hakuna mkakati madhubuti wa kutafuta mbegu mpya ambazo zinaweza zikatoa mafuta mengi ya kutosha. Mbegu tunazozitumia sasa hivi ni mbegu ambazo tunapata mafuta kwa asilimia 60 mpaka asilimia 70, tunatakiwa tupate mbegu mpya, tafiti zifanyike, ili tuweze kupata mafuta mengi yanayotokana na mbegu tunazosindika nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta ya alizeti tunapata asilimia 70 kumbe tungeweza kupata mbegu ambazo tunaweza tukapata mafuta asilimia 80 mpaka asilimia 90 tukipata mbegu bora, Mtanzania anayelima alizeti, anayelima pamba, atapata kipato kikubwa na mzalishaji au msindikaji wa mafuta atapata faida kubwa na tutapata mafuta mengi ambayo ni kwa gharama nafuu na tutakwenda kuyauza kwenye soko letu kwa gharama nafuu na vilevile tunapokwenda kwenye ushindani wa soko la Kimataifa basi tutauza kwa bei nzuri na bidhaa zetu za Tanzania zitaweza kuuzika katika masoko yote ya Afrika Mashariki na ya Kimataifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulitangaza kwamba, tutajikita kwenye viwanda ambavyo vinazalisha au vinavyozalisha ajira kwa wingi. Viwanda vikubwa, kwa mfano viwanda vya textile (viwanda vya nguo), vinazalisha ajira kwa watu wengi. Unakuta kuna watu wengi wanafanya kazi ya kutengeneza nguo kwa mfano suruali au shati, kila mmoja ana kazi yake mmoja anapinda, mwingine anatengeneza tundu la kifungo, mwingine anafanya shughuli nyingine, kwa ujumla kunakuwa na ajira nyingi sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, tutapata ajira kubwa, watu wataweza kufanya kazi, wataongeza kipato pia itaongeza uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, tujikite kule tusisahau tuliyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tujikite kwenye viwanda mama. Suala la Liganga na Mchuchuma, viwanda vinavyozalisha vyuma, viwanda vinavyozalisha nishati ya umeme, tujikite huko ili tuweze kupata umeme wa bei nafuu, tupate malighafi za bei nafuu na tuweze kuuza kwenye viwanda vidogovidogo hapa nchini, hapo tutaweza kujikwamua. Bila kufanya vile itakuwa ni tatizo kwa sababu hata wenye viwanda waliopo sasa hivi, wanaozalisha bidhaa mbalimbali, bidhaa nyingi tunadhani zinazalishwa nchini lakini ukichunguza kwa nyuma yake unakuta zinaingizwa kutoka nje ya nchi kama malighafi na malighafi zenyewe zinatozwa kodi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake uzalishaji unakuwa ni wa gharama kubwa na uuzaji wa bidhaa unakuwa ni wa bei juu, tunashindwa kuingia kwenye ushindani kwa sababu bidhaa zetu ni za bei ya juu, tunakuta kwamba, bidhaa zetu haziuziki, zinazouzika ni za nje ya nchi na ndiyo maana uingizaji wa bidhaa za nje ni mkubwa kwa sababu bidhaa za nje zinauzwa kwa bei nafuu bidhaa zetu zinakuwa na bei ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie katika masuala ya Mkoa wangu wa Simiyu. Mkoa wa Simiyu ni mkoa wenye malighafi nyingi zinazotokana na kilimo, lakini Mkoa wa Simiyu ni Mkoa mpya, hatuna barabara. Ni miradi michache ya barabara ambayo tayari imeshaanzishwa, lakini utekelezaji ni mdogo.
Tunaomba Mkandarasi aliyeko site apewe pesa ili project iendelee, tutengenezewe barabara ya lami na tukishaunganisha Mkoa wetu wa Simiyu tukaweka kiwango cha lami kuunganisha na barabara ambazo zinakuja Dar-es-Salaam kuna uzalishaji mkubwa wa pamba ambapo marobota ya pamba yanayozalishwa katika Mkoa wa Simiyu yataweza kuja Dar-es-Salaam na kulisha viwanda vyetu vya textile na mambo yanaweza kuendelea na uchumi unaweza kuimarika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuongelea katika Mkoa huo wa Simiyu ni suala la mradi wa maji. Kuna mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria unaotakiwa kuleta maji katika Mkoa wa Simiyu, tunaomba utekelezaji wa mradi huu uharakishwe. Tunategemea maji mengi ya kutoka Ziwa Viktoria kwa matumizi ya aina mbili, kwa maana ya domestic use na vilevile tutumie maji kwa ajili ya irrigation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza ina mpunga wa kutosha. Tunaweza tukalima zaidi kwa maana ya kulima mpunga kwa chakula, tulime mpunga kwa maana ya zao la biashara. Sasa hivi duniani watumiaji wa zao la mpunga ni wengi wanazidi kuongezeka, waliokuwa wanaongoza ni wale watumiaji wa zao la ngano, sasa hivi zao la mpunga limeongezeka, watu wanatumia zaidi mchele, kidogo wanatumia na mahindi, lakini zao la mchele linatumika zaidi. Kwa hiyo, tujitoe katika zao la mchele kudhania ni zao la chakula, sasa tutambue mchele ni zao la biashara.
Mkituletea maji ya kutosha katika Mkoa wetu wa Simiyu, basi tuna hakika wakulima Mkoa wa Simiyu wataweza kulima mpunga kwa wingi na mpunga huo tutaweza kulisha kwa asilimia kubwa Tanzania nzima, tunaomba mradi huo utekelezwe mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo unahitaji pesa nyingi ambazo tuliambiwa kwamba, zimeshatolewa kiasi kidogo na feasibility study imeshafanyika. Tunaomba basi utekelezaji ufanyike mtuletee maji ya kutosha katika Mkoa wa Simiyu tuweze kulima, tuweze kulisha mifugo, tutumie maji yale kwa tija, ili tuweze kuleta maendeleo. Kuna Mikoa mingine ina ardhi kubwa kama Simiyu, lakini ardhi haitumiki kwa sababu hatujaweza ku-facilitate ardhi yetu itumike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kusonga mbele kuna suala la rasilimali watu. Nchi yetu ina watu zaidi ya milioni 46, kuna vijana wengi hawana ajira, vijana wengi wako mtaani ambao kwa kweli tukiweza kuweka mazingira mazuri ile tunasema ni human resources ambayo inaweza ika-generate uchumi wetu ukakua kwa hali ya juu. Tumeshindwa kutafuta namna ya kutumia nguvu za vijana tulionao mjini. Ukienda mjini, ukienda vijijini unakuta vijana wanacheza mpira, wanacheza pool! Mheshimiwa Rais juzi kazuia pool! Wanacheza pool kwa sababu, hawana kazi ya kufanya, tuna nguvu kazi kubwa katika nchi yetu ya Tanzania lakini tunashindwa kutafuta namna ya kuitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa miaka mitano kwenda 2025 tutafute namna nzuri ya kuweza kutumia nguvu ya vijana wetu. Ukienda mjini vijana wanacheza mpira, mpira wenyewe wanacheza wengine wanavuta bangi, wako kwenye vijiwe hawana kazi ya kufanya! Tunaomba tuangalie na upande huu, tusiangalie tu vitu vingine, lakini tuangalie tutatumia vipi nguvukazi za hawa vijana kwa maana ya kunufaisha uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ningeweza kuliongelea katika sekta binafsi, ili tuweze kuimarisha uchumi ni lazima tukumbuke sekta binafsi ndiyo sekta pekee inayoweza ikasaidia kuongeza au kufanya industrialization, twende kwenye nchi ya viwanda, bila sekta binafsi hatuwezi kufika. Tuweke mazingira mazuri kwa sekta binafsi, mazingira mazuri ambayo yatawawezesha watu wa sekta binafsi wafanye kazi zao vizuri, wafanye kazi zao kwa tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama kwa harakaharaka katika masuala ya kodi, ni lazima tuitazame vizuri. Kwa mfano, mtu anaingiza bidhaa kwa maana ya uzalishaji, anaingiza mashine kubwa za uzalishaji, ukifika pale anatozwa kodi ya VAT, mtu analeta mashine ya kuja kutengeneza ajira, analeta mashine kubwa ya uzalishaji, lakini katika importation unakuta anachajiwa VAT! VAT ina-discourage kabisa watu kuingiza bidhaa kwa ajili ya uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia VAT nchi zingine mtu anapo-import capital goods kwa maana ya kwenda kuzalisha hatozwi kodi! Nenda Msumbiji, nenda nchi zingine, hawatozwi hiyo kodi! Sasa asipotozwa hiyo kodi na Tanzania tunatoza, basi mwekezaji huyu hawezi kuwekeza Tanzania atakachokifanya ni kwenda nchi nyingine na kuwekeza na akiwekeza kule ata-create ajira kule, ata-create production kule ya tija, tunajikuta tunabaki palepale na Mpango wetu unabaki kwenye makaratasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tubadilike, twende mbele, tuangalie nini tuanze nacho na nini tumalize nacho, lakini tukienda kwa kubeba mambo yote tunaweza tukajikuta tunamaliza miaka mitano bado hatujafika kule tunakotakiwa kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme suala lingine kuhusu uwekezaji kwa maana ya uwekezaji wa nje na ndani. Tunayo TIC, tutazame TIC ijikite kwa kuwawezesha wawekezaji wa ndani waweze kuwekeza vizuri. Wawekezaji wa nje wanapokuja nchini kwetu na wao wanakutana na mazingira mabaya vilevile. Ukiangalia nchi yetu katika huu Mpango wa Serikali wa miaka mitano tumeweka katika namba mia moja thelathini na kitu! Ina maana kwamba, hatuna mazingira mazuri ya uwekezaji! Ni lazima tuangalie leo tunapoamua kuwekeza au kukaribisha wawekezaji tuangalie Central Government inasemaje na Local Government inasemaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna conflict kati ya Central Government pamoja na Local Government, Central Government tunakaribisha mwekezaji, lakini mwekezaji akienda kule kijijini, akienda kuwekeza, akikutana na watu wa Serikali za Mitaa kule wanamuona mwekezaji kama ni adui. Mwekezaji anakutana na mazingira magumu, anafukuzwa na wakija watumbua majipu wananchi wakisema huyu mwekezaji hafai watu wa chini wanashangilia. Tunamwona kama mwekezaji ni mwizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba itolewe elimu, mwekezaji atambulike kwamba huyu ni mwekezaji anakuja kwa faida ya nchi yetu, mwekezaji anakuja kutengeneza ajira, mwekezaji siyo mwizi. Elimu maalum itolewe watu watambue kama mwekezaji ni mwenzetu. Kinachoendelea sasa hivi wawekezaji wamekutana na mazingira magumu, unakuta watu wa NEMC wanasimamisha kiwanda huyu anachafua mazingira, kiwanda kinasimamishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisimamisha kiwanda palepale umesimamisha ajira ya watu walioajiriwa pale, ukisimamisha kiwanda production inasimama, huyu mtu ana-fixed cost unamwingiza kwenye gharama kubwa, unadhani kesho atakuja kuwekeza Tanzania? Tunaomba uwekwe utaratibu, elimu itolewe, kama ni watu wa NEMC wanakwenda kusimamisha viwanda visifanye kazi eti kwa sababu ya mazingira, basi hao watu wa NEMC wawe wameshatangulia kwenda kutoa elimu ya kutosha kumwelekeza mwekezaji ni namna gani ya kutunza mazingira ili tusiwe tunasimamisha production unnecessary kusema kwamba huyu mtu anaharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mazingira mazuri ya kumfanya huyu mtu aone kwamba kuwekeza Tanzania ni vyema, kuwekeza Tanzania utapata faida, hakuna anayewekeza bila kupata faida, lazima tuwawekee mazingira mazuri ya wao kupata faida na tuweke mazingira mazuri ya sisi kama Watanzania kupata faida, tuweke mazingira mazuri kwa vijana wetu kupata ajira kama Watanzania kupitia uwekezaji wa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kusema kwamba kuna tafiti mbalimbali za kibiashara zinafanyika, tunazibeza hatuzifanyii kazi. Ukienda kwenye Vyuo Vikuu kuna tafiti mbalimbali zinafanyika, yaani Marketing survey na marketing research, tafiti hizo ziweze kutumika. Wengine wanafanya tafiti kwa maana ya kupata degree zao, kuna wengine wanafanya tafiti kupata masters zao na wanafanya tafiti ambazo ni za kweli, wanakwenda field wanakusanya data za kutosha, wana-interpret zile data walizozipata kule na vilevile wanakuja na mapendekezo nini kifanyike. Tunaomba tutumie tafiti hizo tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.