Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami vilevile nianze kwanza kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mbalimbali kwenye taarifa yetu.
Nitoe shukrani vilevile kwa Wajumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambao tulifaya kazi bega kwa bega bila kuchoka. Vilevile nitoe shukrani kwa michango iliyotoka kwa Mawaziri kuhusu kuboresha taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ilishindwa kutekeleza baadhi ya majukumu kama ulivyosikia michango mbalimbali ya Wajumbe kutokana na ufinyu wa bajeti uliokuwepo. Kuna baadhi ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameitoa lakini haimo ndani ya taarifa yetu mfano mdogo ni suala la RUBADA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la RUBADA kwenye mipango ya Kamati yetu ya Utekelezaji ya mwaka 2016 tulitakiwa twende RUBADA kuangalia na kufanya kazi lakini pesa haikuwepo kwa hiyo tulishindwa kwenda kule na ndiyo maana hata kwenye taarifa yetu suala la RUBADA halikuwepo. Nipende tu kulitaarifu Bunge lako kwamba siku pesa itakapopatikana tutakwenda na tutakuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kuweza kuishauri Serikali yetu nini cha kufanya kuhusu RUBADA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea michango kwa maneno ya Waheshimiwa Wabunge 22 lakini nimepokea ya maandishi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge 16. Nashukuru sana kwa michango yao yote, michango ambayo ilijaa uzalendo wa hali ya juu na uchungu wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upimaji na urasimishaji wa ardhi lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana, ni kweli kwamba sehemu nyingi sana za miji yetu haijapimwa na hiyo ni changamoto ambayo Serikali inatakiwa iangalie kwa makini. Kamati inaishauri Serikali itenge pesa za kutosha kuwezesha upimaji na urasimishaji wa ardhi kwa wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu cha ajabu, juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwamba Wizara ya Maliasili iende ikatambue mipaka ya baadhi ya hifadhi. Sisi kama Kamati tulishangaa, tuliamini kwamba ilitakiwa na Wizara ya Ardhi nayo ishirikishwe katika kutambua mipaka ya hifadhi za maliasili, lakini hatuoni kama hilo lilitendeka na tuna wasiwasi kama kweli hilo zoezi litaweza kufanyika kwa Wizara ya Maliasili peke yake bila kushirikisha Wizara ya Ardhi. Kama Kamati tunaishauri Serikali Wizara zishirikiane katika kufanya kazi ili kuleta tija katika mambo mbalimbali ambayo wanaelekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea mchango kutoka kwa baadhi ya Wabunge kuhusu ile Kamati ya Wizara Tano inayoshughulikia migogoro. Sisi kama Kamati tumeipokea na tunazidi kuisisitiza Serikali ihakikishe kwamba ile Kamati inaleta ripoti yake kwa wakati ili tuweze kupunguza kama sio kuondoa kabisa migogoro kati ya hifadhi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Ngorongoro vilevile hatukuweza kuliingiza kwenye taarifa ya Kamati yetu kwa sababu tuliliweka kwenye ratiba ya kwenda kutembelea Ngorongoro ili tuweze kuishauri vizuri Serikali, lakini kama kawaida tuliambiwa bajeti haitoshi tukashindwa kwenda. Ni ngumu sana kutoa taarifa na kuzungumzia kitu ambacho hujawahi kukiona. Tunachelea kuzungumza taarifa ya sehemu muhimu kama Ngorongoro kwa kutegemea makaratasi tuliyoletewa mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mjumbe mmoja wa Kamati yangu vilevile ameulizia kuhusu suala la Faru John. Nilitegemea suala hili lingeulizwa na Wajumbe wengi kweli, lakini nashukuru kwamba wengi walielewa kwamba hili suala lipo kwenye uchunguzi, liko chini ya Waziri Mkuu kuna tume imeundwa kulichunguza. Tunaamini tume hiyo itatuletea ripoti baada ya hapo tutaanza kulijadili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la askari wa wanyamapori. Kwa ujumla kama Kamati hata sisi tunasikitishwa sana na baadhi ya askari wa wanyamapori ambao wanaamua kuchukua sheria mkononi na kuua Watanzania wenzetu. Kwa hiyo, kama Kamati tunashauri Wizara ya Maliasili na Utalii iongeze mafunzo kwa askari wetu, lakini vilevile tuishauri Serikali kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu hifadhi zetu kwa sababu bila wananchi kupata uelewa wa kutosha migogoro kati ya askari na wananchi itaendelea kuwepo na hatupendezwi na madhara yanayotokana na vifo vya Watanzania wanaoingia kwenye hifadhi zetu. Kuna njia rahisi zinaweza kutumika ambazo haziwezi kuleta madhara sana kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la ongezeko la VAT kwenye suala letu la utalii. Wakati tunaandaa ripoti yetu tulikutana na Wizara nayo ikatuahidi kwamba mwisho wa mwaka wa fedha watakuwa na taarifa kamili ya hali ya utalii. Kwa hiyo, naomba kama Kamati na Bunge tuvumilie, tusubiri Wizara ituletee taarifa hiyo na kama kutakuwa na upungufu tutaangalia namna ya kuboresha zaidi ili hifadhi na utalii wa nchi yetu uendelee kukua na utuletee tija katika mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la National Housing. Wabunge wengi sana wameongelea sana suala la National Housing. Kama mapendekezo ya Kamati yalivyojionyesha ni kweli kwamba maeneo mengi ambayo National Housing wanakwenda kujenga wanalazimika kununua ardhi, halafu wakishajenga wanalazimika kuleta miundombinu ya barabara, wanaleta umeme na maji. Wakati mwingine National Housing wanapata viwanja sehemu ya mbali na maeneo ambako hivyo vyanzo vipo na wao wanalazimika kuchukua hizo gharama na kuzigawa kwa kila nyumba moja moja. Hali hiyo inasababisha nyumba za National Housing zisionekane ni za gharama nafuu kwa sababu ukishalipia vitu vyote hivyo huwezi kupata gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa natamani sasa Serikali ishirikiane, taasisi zote zinazohusika zishirikiane. Haiwezekani National Housing wagharamie suala la maji halafu Mamlaka za Maji ndiyo ziende zisome bili na kupata pesa kama zenyewe, hiyo ni kumbebesha mwananchi mzigo usikuwa na tija. Vilevile kwa masuala ya umeme, haiwezekani National Housing wasafirishe nguzo hamsini kupeleka kwenye destination ya site halafu TANESCO waje wachukue bili kwa sababu tu umeme ni wa kwao. Naamini TANESCO wakichukua jukumu lao na Mamlaka za Maji zikichukua jukumu lao pamoja na Halmashauri zetu zikichukua jukumu la kupeleka miundombinu ya barabara nyumba zetu za NationalHousing zitakuwa za gharama nafuu na sisi kama Kamati tunalitetea Shirika letu la National Housing liweze kuendelea kufanya kazi zake za kuwahudumia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea amendment kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kuhusu suala la Kigamboni Development Agency. Kamati inakubaliana nayo na tutaomba iingizwe kwenye taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na hifadhi zetu. Kwenye taarifa yetu tumeiweka wazi kwamba kuna mifugo ambayo ipo ndani ya hifadhi zetu. Bado tunasisitiza kwamba kikanuni na kisheria mifugo hairuhusiwi kuwemo ndani ya hifadhi. Tuwashauri Waheshimiwa Wabunge wawaeleweshe wananchi. Nilifurahishwa sana na Mheshimiwa Sannda ambaye alichukua jukumu la kuwaelimisha wananchi na wanaheshimu hifadhi na hawaingilii hifadhi. Hizi hifadhi kama zikivurugika, nchi yetu itakuwa jangwa na hatutapona. Hiyo mifugo tunayoitetea leo na yenyewe itakufa. Kwa hiyo, tujitahidi tushirikiane tuhifadhi misitu yetu ili kuhifadhi mazingira yetu yasiharibike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nitaongelea suala la mashamba makubwa yaliyotelekezwa. Kamati yetu imependekeza Serikali ifanye uhakiki wa haraka mashamba yote makubwa yaliyotelekezwa yachukuliwe yapangwe na yagawiwe kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Vilevile kama itawezekana na Serikali tunatamani iwe na land bank ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya viwanda kwa sababu tunakwenda kwenye dunia ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la shoroba, siwezi nikazungumza moja kwa moja migogoro ya tembo na wananchi inayotokea sehemu mbalimbali hasa Mkoa wa Mara. Nachelea ku-confirm moja kwa moja kwamba inawezekana shoroba zimeingiliwa, inawezekana zimeingiliwa au hazijaingiliwa. Hata hivyo, natamani Serikali sasa iamke na iende kutambua shoroba zote ambazo zimeingiliwa kwa sababu baadhi ya shoroba Halmashauri imejenga, baadhi ya shoroba kuna shule zimejengwa na hizo zote ni za Serikali. Kwa hiyo, ushirikiano kati ya Wizara mbalimbali ni muhimu sana kuhakikisha tunalinda shoroba zetu na zile ambazo kweli kabisa taasisi za Serikali zimejenga basi Serikali iangalie namna ya kufidia ziondolewe ili wanyama wapate mahali pa kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo sehemu aliyopita miaka hamsini iliyopita habadilishi anapita palepale. Kwa hiyo, ukijenga aki-escape lazima atadhuru mifugo na mazao ya wananchi kwa sababu sehemu anakopita ni palepale hata miaka mia inayokuja. Kwa hiyo, tulinde shoroba zetu ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata changamoto kidogo kutoka kwa Mheshimiwa Kanyasu kuhusu pori la Geita kuvamiwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kuonesha uchungu wa kutaka kuhifadhi pori letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kutoa hoja kwamba Bunge sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati pamoja na maoni na maendekezo yalimo katika taarifa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja!