Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru. Mimi nitakuwa na machache tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja nataka tuweke angalizo kuhusu hifadhi zetu na mifugo. Waheshimiwa Wabunge tusipokuwa makini baada ya miaka michache tutakuwa hakuna wildlife nchi hii. Hii ya wafugaji kung’ang’ania kwenye hifadhi zetu eti tu kwa sababu bwana mkubwa alisema msitoke, hii siyo sahihi jamani. This country tuta-wipe-up wildlife yote ya nchi hii. Nadhani hoja ya msingi ambayo nafikiri Serikali ingekwenda kuifanyia kazi ni ile Tume ya Waziri Mkuu ya zile Wizara tano ziharakishe kufanya zoezi lile ili yale maeneo ambayo yamekosa sifa ya uhifadhi ndiyo mifugo ihamishiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ngorogoro hamjui mkakati uliopo wa Wakenya hapa, wanataka kui-suffocate Ngorongoro hatimaye tuiue Serengeti ili wabaki na advantage ya Masai Mara ya Kenya. Nilikuwa naweka tu angalizo ili tuweze kuelewana vizuri na watu wa maliasili nadhani jambo hili hatuwezi kulifumbia macho, tusipokuwa makini baada ya miaka michache nchi hii itakuwa haina maliasili wala haitakuwa na wanyamapori au watapungua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la tozo. Ukiangalia taarifa ya Kamati yetu ya Bajeti inazungumzia kwamba tozo hizi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kwamba hizi tozo zimeondolewa. Mimi nipo kwenye Kamati ya Kilimo na Mifugo, hizi tozo hazijaondolewa na taarifa niliyonayo ni kwamba Waziri wa Biashara anahangaika kutafuta namna gani ya kuziondoa, sasa hizi taarifa zingine zinakuwa hazina uhalisia. Tozo za mazao, tozo ya Bodi ya Pamba, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Korosho kidogo wameangalia, lakini Bodi ya Chai bado na mazao mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri nikikubaliana na mapendekezo ya Kamati hii ya kilimo madam tunakwenda kwenye bajeti tunaomba tozo hizi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hizi tozo futeni. Waziri Mramba alizifuta hizi sijui kwa nini zinarudishwa. Wale wenye kumbukumbu tozo hizi ziliitwa kodi za kero, kodi za mazao na zikaondolewa, sasa leo kwa nini zishiondolewe? Nafikiri hilo ni jambo muhimu kwa sababu tunajenga na tunakwenda kwenye bajeti ni vema tozo za mazao ya biashara zikaondolewa ili wakulima waweze kuuza mazao yao na hatimaye wapate kipato chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalopenda kuzungumzia ni upatikanaji wa mbegu, Waziri wa Kilimo unajua kwamba nchi hii hatuna mbegu, hata mbegu za mazao ya chakula zinazozalishwa nchini ni asilimia 35 mpaka asilimia 40, mbegu nyingi zinatoka nje ya nchi yetu. Zinatoka Zimbabwe na Kenya. Ushauri wangu kwa Serikali kama tulivyosema kwenye Kamati yetu ya Kilimo haiwezekani tuzungumzie uchumi wa viwanda wakati hatuna hata mbegu za mazao yetu wenyewe ambayo hatimaye ndiyo zitatengeneza hivi viwanda vya agro industries. Sasa suala la mbegu ni la msingi sana na nilikuwa naomba wenzetu wa Serikali mkaliangalie hasa kwa sababu tunajenga upya bajeti yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upatikanaji wa mbolea limezungumzwa. Labda niseme Waheshimiwa Wabunge wananchi wetu wengi wanaishi vijijini na wananchi wetu wengi ni wakulima. Hawa wananchi wetu bado kuna shida ya upatikanaji wa mbolea. Kwa mfano, takwimu za mwaka jana huu mwaka tunaoumaliza sasa, ni kaya 378 tu ambazo zimepata pembejeo nchi nzima ambayo ni sawa sawa na asilimia 0.06 ya wakulima, sasa huu kama siyo mchezo wa kuigiza ni kitu gani? Hatuna mbolea, hakuna mbegu halafu unakuja kuzungumzia uchumi wa viwanda, viwanda vipi hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda tunavyovifikiria lazima viwe ni viwanda ambavyo vitaajiri watu wetu wengi vijijini na viwanda hivyo ni viwanda vya mazao ya kilimo pamoja na michikichi. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo ni jambo la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uzalishaji wa mbegu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Waziri wa Uwekezaji na Waziri wa Mambo ya Ndani jengeni mkakati wa kuzalisha mbegu kupitia Magereza yetu. Jeshi la Magereza Waziri wa Mambo ya Ndani jana umelisema vizuri tu, nina hakika wenzetu wa Magereza wana mashamba makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mkakati maalum ambao umejengwa kibajeti, nina hakika tunaweza tukazalisha mbegu zetu wenyewe na zikatosheleza. Maeneo kama Magereza, JKT na hata watu binafsi wanaweza wakafanya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho ni hii food for thought wenzetu wa Serikali mkalitizame. Kwa maoni yangu na maoni ya watu wengi kwenye Kamati yetu ya Kilimo jamani hii Wizara ya Kilimo ni kubwa sana, hii Wizara ina vitu vingi sana. Ushauri wangu kwa Serikali muangalie namna nzuri ya kumshauri bwana mkubwa hii Wizara muundo wake utazamwe upya. Maana yake una mifugo una kilimo, uvuvi, ushirika, masoko na taasisi zaidi ya 60 chini ya Wizara moja.
Kwa hiyo, nilikuwa nashauri sincerely kabisa, wenzetu wa Serikali mkakae mliangalie hili mumshauri bwana mkubwa namna anavyoweza kuhuisha huu muundo ili uweze kuwa na tija kwa sababu Wizara hii kwa kweli ni Wizara mama. Wizara hii ndiyo roho ya Taifa letu kwa sababu ndiyo inaajiri watu wengi na ni tegemeo la maisha ya Watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni huu Mfuko wa Maji ambao umesemwa sana na kwenye Kamati tulikwenda mbali zaidi tukasema ni vizuri hata hizo fedha zinazotolewa tuwe tunajua ni kiasi gani cha mafuta yameuzwa. Kwa sababu msingi wa Mfuko wa Maji ni hizi fedha zimezungushiwa wigo wake ili zikaondoe tatizo la maji katika maeneo yetu vijijini. Kumekuwa na kuchechemea kidogo kwa Serikali. Tunataka kujua exactly ni kiasi gani ambacho Mfuko wa Maji unapaswa kupata, siyo ku-remit kwenda Wizarani. Mapato halisi ya Mfuko wa Maji lazima yajulikane kwa sababu ni kauli ya Bunge hili, tuli- ring fence zile fedha kwa ajili ya kwenda kuondoa matatizo ya maji katika maeneo yetu ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nimeyasema jana, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.