Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu na nianze na migogoro kati ya watumiaji wengine pamoja na hifadhi zetu. Inawezekana tutapiga kelele kuhusu jambo hili, lakini tukubaliane tu kama Bunge kwamba Serikali inalea na inachangia sana mauaji na mapigano ya wananchi pamoja na wanajeshi wetu katika maeneo ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pasipo shaka Serikali ina tathmini ya watu waliouawa katika hifadhi. Juzi waliuawa watu wanne kule Arumeru, hakuna kauli ya Serikali wala ziara yoyote ya Serikali iliyotembelea eneo hilo. Ikitokea ugomvi kati ya mkulima na mfugaji Serikali itapeleka polisi, Serikali itapeleka kila kitu, lakini akiuawa mwananchi katika eneo la hifadhi wala Serikali haijali na ndiyo maana Serikali inatoza watu wakiua tembo dola 15,000 lakini mwananchi analipwa shilingi milioni moja akiuawa. Kwa nini tusiseme Serikali ina ajenda ya kuua watu wake kwa kisingizio cha uhifadhi wa wanyamapori? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengi ya hifadhi, zile buffer zone ambazo Serikali inasema mita 500, maeneo mengine kuna maji, lakini mwananchi anaambiwa buffer zone zile zinaanzia mita 500 katika eneo la mto ambalo kuna maji. Mwananchi atapataje nafasi ya kwenda kuyatumia yale maji? Ndiyo chanzo cha migogoro mingi. Maeneo mengine ukienda kama Ngorongoro, ukienda kule Sikonge, tumepata taarifa wananchi wameuawa wanapigwa risasi ya kisogo na askari, lakini Serikali imaficha. Jana tumepata taarifa ya kule Morogoro Serikali ya Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa waliwanyima Civil Society na Waandishi wa Habari kuingia kwenda kukusanya taarifa ya hali ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naliona ni kwamba Serikali haijawa tayari kushughulikia matatizo haya. Kwa mfano, zimekuja ripoti mbalimbali, Operation Tokomeza, Ripoti ya akina Mheshimiwa Jenista Mhagama, wakati ule ilikwenda kutafuta tatizo la wafugaji na wakulima, Serikali imekalia ripoti, hakuna taarifa yoyote ambayo so far Serikali imeyafanyia kazi mapendekezo ya Wabunge! Hivi tutaendeea kukaa kwenye Bunge mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Bunge hili litoe Azimio, Serikali itoe commitment leo kwamba matatizo ya wafugaji na wakulima yataisha lini nchi hii? Vinginevyo tutagawa Taifa hili, vinginevyo tutawagawa wananchi wetu hawa, vinginevyo tutatengeneza uadui ambao ni mbaya kuliko uadui ulioko nje ya nchi yetu, kama Serikali haitoi commitment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesababisha haya kwa sababu Wizara hizi hawashirikiani, Waziri wa Kilimo anaenda peke yake, Waziri wa Ardhi anaenda peke yake, Waziri wa Maliasili anaenda peke yake. Naomba wakati naendelea hivi, tunaomba Kauli ya Serikali. Hivi kauli kubwa kuliko yote ni ipi? Rais amesema wafugaji wasisumbuliwe kwenye hifadhi mpaka Serikali itakapopata maeneo ya kuwapeleka, ananyanyuka Waziri wa Maliasili anasema ondokeni leo, bila kutuambia tunaenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani yule ambaye anaweza akatengua kauli ya Rais aliyesema tutengewe maeneo ya kwenda kwenye mifugo kabla ya kutuondoa katika maeneo yale? Waziri ananyanyuka anasema wafugaji waondoke, twende wapi? Mazingira ambayo tunayaonesha kama Serikali haitatengeneza utaratibu wa matumizi bora ya ardhi kwenye nchi yetu, migogoro hii haitakaa iishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha sheria hapa ya kuweka chapa mifugo, tumepitisha sheria ya kutenga maeneo ya mifugo, lakini mpaka sasa hakuna hata sehemu moja ambayo Serikali ime-declare kwamba eneo hili ni la wafugaji. Matokeo yake wafugaji wanaondoka wanaenda kwenye mashamba ya watu na hakuna mkulima yuko tayari kuona mfugaji akilisha ng’ombe kwenye shamba lake. Hicho ni chanzo cha migogoro na hatuna kauli thabiti ya Serikali ya kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kusikia wakisema tunalaani, tutaendelea kusema watu wakipelekwa mahakamani, lakini watu wanahonga na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Hatuwezi kama Bunge kuona wananchi wetu wanauawa kwa sababu ya uzembe wa Mawaziri na uzembe wa Serikali yenyewe. Tunataka commitment ya Serikali tunamalizaje tatizo la wafugaji na wakulima nchini mwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini miaka ya nyuma tulikuwa hatugombani? Ni kwa sababu ardhi ilikuwa inatosha, sasa ardhi imekuwa ndogo, Serikali haina mikakati. Mnasema Idara ya Ardhi watenge maeneo lakini hamuwapi bajeti. Kama kweli Bunge hili tunatamani kuwaunganisha Watanzania ni muhimu kuibana Serikali itoe commitment na schedule program ya kuhakikisha inamaliza tatizo hili ambalo la wakulima na wafugaji ambalo limekuwa kubwa kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba nilichangie ni suala la Wizara ya Ardhi. Wengine wamechangia na Kamati imeona kwamba tatizo kubwa ni kwamba kuna mashamba makubwa ambayo yamehodhiwa na watu ambao hawajayaendeleza. Nitasema mashamba manne tu Monduli, ambayo watu wanne wanamiliki zaidi ya ekari 32,000 na mpaka sasa hawajalima hata nusu ekari, lakini mpaka leo Serikali haitoi kauli kwamba mashamba hayo yanarudi lini kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo shamba la Sluiz, tunalo shamba la Tan Farm, tunalo shamba la Stein ambalo lina ekari 16,000 peke yake hajaendelezwa na Serikali imeendelea! Kwa nini migogoro isitokee? Kwa hiyo, tunafikiri kama Serikali imedhamiria kweli kuyarejesha mashamba haya kwa wananchi ni muhimu ikafanya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni kuhusu ukame ambalo limekuwa kubwa. Mmesema tusiseme kuna njaa, tukisema hivyo tunafunguliwa mashtaka. Mimi nafikiri mtalifungia Bunge lote hili, hakuna Mbunge asiyejua kwamba wananchi wanaenda kwenye maeneo wakilalamika njaa na tunaona. Tunaona mifugo yetu ambayo ni rasilimali yetu ikiteketea, tunaona mashamba yakikauka. Ni kweli Serikali haijaleta ukame, lakini tusikatae kwamba kuna taizo la njaa linalotokana na ukame ili tuende tukajadiliane kama Taifa tunafanyaje kuwaokoa watu wetu wasife, kuliko kuendelea kusema kwamba hatuna tatizo, lakini tatizo hili linatumaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu asiyeona kwamba mvua zimechelewa kunyesha, lakini Serikali inakataa hakuna njaa ili Watanzania hawa wafe, tunaogopa nini wakati ninyi hamjaleta ukame au labda ninyi ndiyo mmeleta ukame? Kama siyo ninyi msizuie watu kusema kuna tatizo. Anayeopata neema ya mvua ni ya Mungu tu. Sasa msiwacheke wale ambao neema hiyo haijawafikia, tukifanya hivyo tutasaidia Taifa letu kutafuta namna ambavyo tutapambana na majanga haya yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, tunalo tatizo la hifadhi zetu na wafugaji. Tunataka Serikali ituambie kwa nini Serikali isishirikiane na wananchi wa vijiji katika maeneo yao katika kutafuta suluhu ya kukubaliana mipaka mipya ya hifadhi zetu na wananchi wetu? Katika eneo la Ngorongoro peke yake mnataka kuchukua square metre 15,000 kilometa 1,500 ya wananchi kwa kisingizio kwamba kuna wahamiaji haramu, naitaka Serikali wakati inafanya majumuisho ituambie…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Laizer.