Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dokta Ndugulile asisahau amendment ili tuweze kufanya hiyo amendment jioni kwa ajili ya kusaidia watu wa Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina mambo matatu tu, mawili ni ya jimboni kwangu na moja ni la Kitaifa. Jambo la kwanza ni kuhusiana na mradi wa maji Kigoma. Tulikuwa tuna mradi wa maji ambao una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 16 ambao ungeweza kutatua tatizo la maji la Manispaa ya Kigoma-Ujiji kwa asilimia mia moja na mradi ule ulikuwa uishe mwezi Machi, 2015. Bahati mbaya mpaka sasa mradi ule bado haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge la mwezi Februari, 2016 niliuliza swali hapa Bungeni na Wizara kupitia kwa Naibu Waziri wakasema kwamba mradi huu utakwisha mwezi Oktoba, 2016. Baadaye Mheshimiwa Waziri akafanya ziara katika Mkoa wa Kigoma na akatembelea mradi huu na akawa ametuahidi kwamba mradi huu utakamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu Bungeni mwezi Mei mwaka jana niliitahadharisha Serikali kwamba, mkandarasi aliyepewa kazi hii ya ujenzi wa mradi huu tayari amefilisika na anatumia fedha ambazo tunamlipa kulipia madeni yake katika maeneo mengine ambako anadaiwa; kwenye miradi mbalimbali duniani, lakini Serikali ikasema kwamba italishughulikia suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, mwezi Januari mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ametangaza rasmi kwamba mkandarasi huyu amefilisika. Imeleta taharuki kubwa kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji na hawaelewi sasa nini hatma ya mradi huu tena. Kwa hiyo, naomba Serikali iweze kutoa maelezo ya kina katika majibu yake kuhusiana na suala hili, kwa sababu ni mradi muhimu sana ni mradi ambao tumeuhangaikia, ni mradi ambao fedha za wafadhili zimetoka zaidi ya Shilingi bilioni 32 na tunashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali haijachukua hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia mkandarasi huyu hana mradi Kigoma peke yake, ana mradi pia Musoma na mradi huo pia na wenyewe unasuasua. Kwa hiyo, Waziri atakapokuwa analieleza hili, si kwa maslahi ya Kigoma peke yake, pia aangalie namna gani ambavyo tunaweza tukapambana na wakandarasi wa namna hii ambao wanachukua miradi hawaimalizi na kusababishia wananchi kero nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la umwagiliaji. Mwaka jana nilizungumza kwenye Bajeti ya Wizara ya Kilimo na vile vile nilizungumza kwa maandishi kwenye Bajeti ya Wizara ya Maji na pia nilizungumza na Waziri mwenyewe na Waziri alikuja Kigoma na akatembelea Mradi wa Umwagiliaji wa mto Rwiche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 5 Juni, 2015, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje alimuandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Chakula wakati ule kuhusiana na mradi wa umwagiliaji wa mpunga katika bonde la Mto Rwiche. Barua ile ilikuwa na kumbukumbu namba CHC.325/395/01/42 ambapo Katibu Mkuu aliisaini na kuagiza jambo hili liweze kufanyiwa kazi. Katika barua ile Katibu Mkuu wa Wizara wa Mambo ya Nje aliambatisha barua kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Quwait (Quwait Development Fund), barua ile ilikuwa ni ya tarehe 24 Mei, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichopaswa kufanywa upande wetu sisi ni kufanya detailed feasibility study ya mradi huu ili mradi huu uweze kufadhiliwa na Quwait Development Fund na hivyo tuweze kuwa na mradi mkubwa sana wa umwagiliaji na kuzalisha zao la mpunga katika Manispaa ya Kigoma katika bonde la mto Rwiche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa na nilikuwa naangalia bajeti hapa ya Tume ya Umwagiliaji nimeona kwamba pamoja na kwamba tulipitisha bajeti ya Shilingi bilioni sita katika bajeti ya mwaka huu, fedha ambazo zimeshapelekwa Tume ya umwagiliaji ni asilimia 13 tu ya fedha ambazo zilitakiwa na sasa hivi tumeshafikia nusu ya mwaka wa fedha wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo ya Serikali na jambo hili linahusu Wizara tatu. Linahusu Wizara ya umwagiliaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Fedha, kwa sababu Quwait Fund wana-desk pale Wizara ya Fedha. Tuweze kupata suluhisho la jambo hili kwa sababu mradi huu ni mradi mkubwa sana na ni mradi ambao unaweza ukatatua tatizo la chakula katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu sasa hivi nchi yetu inakabiliwa na baa la njaa, chakula ni kichache hakitoshi, kwa hiyo, ni muhimu sana kuwa na miradi mingi ya umwagiliaji na mradi mmoja muhimu sana ni huu mradi wa bonde la Mto Rwiche. Nitakachokifanya kwa mara nyingine nitampatia Waziri barua zote hizi ili aweze kushauriana na Mawaziri wenzake; Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Nje tuweze kupata suluhisho la jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni la Kitaifa. Kamati ya Kilimo imependekeza kwamba tuongeze Sh. 100 kwenye bei ya mafuta ili tuweze kupata fedha za kutosha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Maji. Sipishani kabisa wala sibishani na Kamati juu ya suala zima la kuongeza uwezo wa Mfuko wa Maendeleo ya Maji ili kuweza kutatua tatizo la maji kwa sabaabu ndilo tatizo kubwa ambalo wananchi wetu wanalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu tu ni kwamba lazima tuwe aware kwamba kwa wiki tatu zilizopita bei ya mafuta kwenye soko la dunia imeongezeka kwa asimia 30. Kwa hiyo maamuzi yoyote ambayo tunayafanya, tuangalie namna gani ambayo tusipeleke mzigo kwa wananchi wa kawaida. Hata hivyo, tunalo suluhisho katika jambo hili, miaka takribani 10 iliyopita tulipitisha Sheria kwa ajili ya kutoa fedha kwenda REA, fedha kwenye mafuta ya taa, mafuta ya diesel na mafuta ya petrol.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiwango kikubwa sasa hivi, REA imefanikisha malengo yake ya kuweza kufikisha umeme vijijini. Kwa hiyo tunachoweza kukifanya kwenye Sheria ya Fedha; na ningeomba tufanye marekebisho kidogo kwenye mapendekezo haya; ni kupunguza Sh. 50 kutoka kwenye fedha ambazo zinakwenda REA kutoka Sh. 100 mpaka Sh. 50 na tupunguze Sh. 100 kwenye fedha za mafuta ya taa zinazokwenda REA, fedha hizi sasa tuzipeleke kwenye maji. Kwa maana hiyo ni kwamba tutakuwa tumebakiza gharama za mafuta zitakuwa ni vile vile na sekta ya maji itakuwa imepata fedha za kutosha kwa ajili ya kuweza kutatua tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kuweza kufanya hivi kwa sababu baadaye tunaweza tukajikuta tumesababisha mfumuko mkubwa wa bei bila kufanya mambo haya kwa uangalifu ambao unatakiwa. Kwa hiyo , naomba tu watu wa Kamati ya Maji, sipingi hoja yao, naiunga mkono lakini tuirekebishe kwa namna ambayo itaweza kuondoa mzigo wa….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zitto muda wako umekwisha.