Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru sana kunipa nafasi niweze
kuchangia. Naomba nitoe pongezi, lakini pia niwapongeze Mawaziri wote kwa kazi nzuri
ambayo wanaendelea katika uwasilishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwangu mimi ni maeneo mawili makubwa. Jambo la
kwanza ni suala la umeme. Wajumbe wenzangu waliotangulia wameshazungumza sana lakini
kwa kuonesha msisitizo na kwa kuonesha tatizo ambalo mikoa yetu ya Lindi na Mtwara
tunakabiliwa nalo naomba nilirudie pia kulizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme Mkoa wa Lindi na Mtwara ni tatizo, kwa siku umeme
unakatika si chini ya mara saba mpaka mara nane. Kila Mbunge anaesimama anaetoka Lindi
na Mtwara jambo hili amekuwa analiulizia na kulitolea ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba pamoja na jitihada na kazi zote
zinazoendelea kufanyika, suala la umeme, kile kituo ambacho tumeahidiwa kitajengwa pale
Mnazi Mmoja kwa ajili ya kusambaza umeme katika maeneo ya Kanda nzima tunafikiri sasa ni
wakati muafaka wa kuweza kulitekeleza jambo hili. Kwa kufanya hivyo tutaendana sambamba
na kauli ya kujenga uchumi kupitia viwanda ambavyo tunaendelea kuvihamasisha. Nje ya
hapo kwa kweli hali itaendelea kuwa mbaya na watu wetu kwa kweli wanaendelea kupata
shida wakati hatuna sababu ya kupata shida ukizingatia gesi sasa hivi kwa sehemu kubwa
inatoka katika ukanda wa kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika umeme ni suala la umeme vijijini. Naomba
niishukuru Serikali, kwa awamu ya pili vijiji vingi vya Wilaya ya Nachingwea vimepata umeme,
lakini nilikuwa naomba katika hii Awamu ya Tatu basi ni vizuri, kama ambavyo wenzangu
wametangulia kusema msisitizo uweze kuanza ili vijiji vilivyobakia katika Tarafa tano za Wilaya ya
Nachingwea viweze kupatiwa umeme wa uhakika ili wananchi waweze kupata huduma
ambayo kimsingi inahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni suala la barabara. Mwaka jana tumezungumza
habari ya barabara, lakini mwaka huu tunapokwenda kuanza kutekeleza mambo yetu
ingawaje tuko ndani ya bajeti bado kuna umuhimu wa kujenga barabara kwa kiwango cha
lami. Hapa naomba niizungumzie barabara ya Masasi - Nachingwea, Nachingwea -
Nanganga, ni kilometa 91. Jambo hili wananchi wa Jimbo la Nachingwea, Masasi pamoja na
maeneo ya jirani limekuwa linatunyima raha sana na limekuwa linatuchelewesha kwenye
shughuli za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri pamoja na watu wa
Wizara katika utaratibu tunaoenda kuuweka basi kwa sababu tayari feasibility study imefanyika,
tunaomba barabara hii watu wa Mkoa wa Lindi, watu wa Wilaya ya Nachingwea tuweze
kupatiwa ili tuweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni suala
la madini. Mheshimiwa Naibu Waziri, mwaka wa jana niliuliza swali hapa alinipa takwimu ya
makampuni zaidi ya 240 yanayofanya utafiti katika Mkoa wa Lindi, lakini baada ya kufuatilia
mpaka sasa hivi makampuni haya yote ambayo yametajwa katika orodha yao sijaona kampuni
hata moja inayoendelea na utafiti wa madini katika maeneo yetu. (Makofi)
Kwa hiyo, nilikuwa naomba kutoa masisitizo, wananchi wanataka wapate fursa ya
kuchimba madini katika maeneo yanayozunguka Nachingwea, lakini bado jitihada za utafiti
hazijafanyika. Kwa hiyo, nitoe msisitizo, yale makampuni yaliyotajwa tunaomba yaje na tuyaone
bayana ili tuweze kuwasaidia kuwaonesha maeneo gani tunaweza tukapata madini na hivyo
tuweze kusaidia vijana wetu kupata ajira wajikwamue kupitia shughuli zao za kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda naomba niseme hayo lakini pia naomba
niunge mkono hoja. Ahsante sana.