Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwanza
nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati zote mbili, Kamati ya Mindombinu na Kamati ya
Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwa haraka, hoja yangu ya kwanza ni kutoa
msisitizo kwa Serikali juhudi ambazo wameonyesha katika vipande vingine upande wa reli
kwenda kwenye standard gauge basi wasisahau na reli yetu ya Mpanda ambapo inaanza
kuchepuka kutokea Kaliua kwenda mpaka Mpanda na vilevile reli kufanyiwa usanifu kutokea
Mpanda mpaka Karema, upande wa Karema tunatarajia kuwa na bandari ambapo pana
upana mdogo katika Ziwa Tanganyika na upande wa pili wa nchi yetu ya jirani ya DRC.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa hizi reli pamoja na bandari kule Karema ni
kupitisha mizigo, sasa na tunaona nchi nyingi ambazo hazina bandari (landlocked conutries),
tutumie hiyo fursa ili tuweze kuongeza mapato katika bandari yetu. Taarifa ya Kamati
imeonyesha jinsi gani mizigo kwenye bandari imeweza kushuka kwa asilimia 0.1 na sehemu
nyingine asilimia 5.2, kwa hiyo tuombe sana Serikali iangalie reli upande wa Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wetu wa ndege wa Mpanda, uwanja wa
ndege wa Mpanda hauna gari la zimamoto, hamna mkandarasi wa mafuta, kwa hiyo tunahitaji
Serikali iweze kushawishi hivyo vitu. Tuna Mbuga ya Katavi ambapo ni moja ya maeneo ya
mbuga ambayo wanasema ni very virgin, wanyama wana asili sana, ukienda Mbuga ya Katavi
utaona asili yao ukishuka kwenye gari samba anakimbia, tofauti na maeneo mengine kama
Serengeti. Kwa hiyo, uwanja wa ndege huu ni muhimu sana kwa ajili ya utalii kwenye Mbuga
yetu ya Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la mawasiliano tunahitaji kampuni za simu
ziendelee kuimarisha mawasiliano, na hasa Kampuni ya Halotel ambayo ilianzia vijijini, maeneo
yetu mengi tuna matatizo ya mawasiliano. Ukiwa unasafiri kutoka Mpanda kuja Tabora kuna
maeneo ya katikati unatembea kilometa karibu 90 hakuna mawasiliano, sasa inapotokea
dharura yoyote na dunia sasa hivi iko kwenye kiganja, kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la SUMATRA, mamlaka hii ipo lakini usimamizi wa bei
bado ni hafifu sana. Tumepata kero nyingi kwenye ziara tulizozifanya, kwa mfano watu wetu
wanaotoka Mpanda kwenda Ugala wote wanachajiwa shilingi 5,000 lakini katikati hapa kuna
sehemu wanatakiwa walipe shilingi 2,000, shilingi 3,000 na shilingi 4,000 lakini wote wanalipa bei
moja. Kwa hiyo, SUMATRA wasiwe wanasubiri malalamiko ya wananchi, wawe wanafanya
testing ya hizi control zao zinafanyaje kazi na wachukulie hatua watu wenye vyombo hivi vya
usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapohapo kwenye mawasiliano, TCRA watusaidie
Halmashauri zetu, na ningeomba mwongozo wa Serikali, hii minara inakuwa na rekodi ya
mawasiliano yamefanyika katika lile eneo na yale mapato ambayo yametokana na kampuni
za simu kwenye mnara husika.
Sasa ile service levy haya makampuni wanalipa wapi? Kwa hiyo, unakuta Halmashauri
zetu hazipati mapato toka kwenye makampuni ya mawasiliano kwa sababu ya mawasiliano au
muunganiko katika ya TCRA na Halmashauri kidogo uko tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye madini, tumekuwa na changamoto kwa
wachimbaji, wamekuwa na migogoro na watu ambao wamepewa leseni. Kwa mfano kwenye
Jimbo langu la Nsimbo, eneo la Kijani Investment imekuwa ni mgogoro, Kampuni ya Sambaru
imekuwa ni mgogoro wanasema hakuna muhtasari, sasa shida iliyopo ni nini, tungeomba
Serikali itenge maeneo kwa ajili ya watu ambao hawana leseni, watu leo anaamua akachimbe
anunue unga au alipe ada na yawe chini ya uongozi wa kijiji ndiyo uweze kusimamia. Tukifanya
hivyo tutaondoa migogoro kwenye haya maeneo ya watu ambao wanakuwa na leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile upatikanaji wa service levy toka kwenye makampuni
haya yanayochimba yenye leseni ndogo (PML) na leseni kubwa, rekodi zao haziko sahihi kwa
hiyo, Halmashauri zetu hazipati service levy. Kwa hiyo, nashauri Serikali iangalie fixed amount
kulingana na aina ya leseni na sehemu nyingine iwe ya kiasilimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe upande wa nishati, REA III, kwa Mkoa wetu wa Katavi
vijiji 74 haviko kwenye huu mpango wa sasa hivi, kati ya vijiji 191 tumepewa vijiji 117 na ni mkoa
wa pembezoni ambao ulisahaulika sana kimaendeleo. Kwa hiyo, tunaomba vijiji 74 viongezwe
na wakandarasi waongezewe mikataba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tunaomba Serikali iendelee kutoa ushirikiano kwa
kampuni inayofanya utafiti wa mafuta Ziwa Tanganyika na pia gesi na maeneo mengine ya
madini katika Mkoa wa Katavi na mikoa jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja za Kamati
hizi.