Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijadili taarifa hizi mbili
lakini nitajikita sana kwenye Taarifa ya Nishati na Madini. La kwanza, kwa sababu Kamati zetu
hizi zinatoa mapendekezo na maoni mbalimbali; tunatumia karibu siku tano, sita kutoa
mapendekezo; tulishawahi kufanya hivyo siku za nyuma, lakini tukijiuliza: Je, haya mapendekezo
mwisho wa siku nani anakuja kuyajadili?
Taarifa hizi tunazopendekeza, zinaletwa Bungeni lini na kujua kwamba kweli haya
tuliyopendekeza yametekelezwa? Kama yametekelezwa, ni kwa kiasi gani? Nani anajua? Au
kazi yetu sisi ni kutoa mapendekezo, yanakwenda Serikalini halafu basi yanaishia hapo hapo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba ule utaratibu wa zamani kweli kwenye enzi za
akina Mheshimiwa Shelukindo, taarifa zilikuwa zinasomwa, mapendekezo yanatolewa,
baadaye Serikali inakuja inajibu pale ambapo imetekeleza; kwa nini imeshindwa na kwa nini
imefanikiwa, ili kusudi kuweza kujua haya yote ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge tunakaa siku
mbili tatu humu ndani tunayasema. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, hili wala siyo la Serikali hata kidogo, ni letu sisi Waheshimiwa
Wabunge. Kwa sababu tukisema kwamba tunataka kufanya jambo hili, lakini lazima tujue
kwamba mambo haya yanatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba unikubalie niipongeze Serikali kupitia Shirika la
Umeme (TANESCO); sijui wamefanya miujiza gani. Siku hizi sijasikia kukatika katika kwa umeme,
lakini mgao wa umeme; hata kama unakatika labda ni bahati mbaya. Lazima niseme ukweli, ni
tofauti na siku za nyuma. Sasa hivi kukatika kwa umeme kumepungua sana, lakini hata mgao
wa umeme nchini sasa hivi hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaiomba Serikali kupitia TANESCO waongeze ile kasi
ya kulisimamia Shirika hili la TANESCO, kwa sababu yapo mambo mengi. Jambo la kwanza
ambalo naiomba Serikali, tulikubaliana katika kutekeleza kwamba ipunguze gharama za pale
tunaponunua huu umeme. Kwa mfano, Symbion, Aggreko na Songas ambayo kwa taarifa ya
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, mpaka sasa TANESCO
inadaiwa shilingi bilioni 63. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, hapa
kuna mkanganyiko wa madeni ya TANESCO. TANESCO inadaiwa kiasi gani na TANESCO inadai
kiasi gani? Mfano, kwa mujibu wa taarifa ambayo imesomwa sasa hivi na Mwenyekiti wa
Kamati, wanasema kwamba TANESCO inadaiwa shilingi bilioni 822, lakini kwa mujibu wa taarifa
ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, wanasema TANESCO inadai shilingi bilioni 796. Sasa ipi ni ipi?
TANESCO inadaiwa au TANESCO inadai?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri tukapata mchanganuo vizuri ili sisi
Waheshimiwa Wabunge tuweze kujua, kwa sababu hii inachanganya. Kwa mujibu wa taarifa
ambayo imesomwa sasa hivi hapa, wanasema Serikali na taasisi inaidai TANESCO shilingi milioni
269. Sasa hii inachanganya. Tunaomba Serikali, itakapokuja kujibu au Mheshimiwa Mwenyekiti
wa Kamati mtusaidie kujua hasa. Mtupe mchanganuo halisi TANESCO inadai kiasi gani na
TANESCO inadaiwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba tusaidiwe tu, ni haya katika utekelezaji.
Lipo suala la Sera ya Gesi na Mafuta kutafsiriwa katika lugha ya Kiswahili. Tulikubaliana kwenye
Kamati na tukaleta mapendekezo ndani ya Bunge, ndiyo maana nikasema mambo haya kama
hatufuatilii utekelezaji wake, inaweza ikawa ni tatizo. Jambo hili tumelisema humu ndani lakini
imekuwa halieleweki.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, mpango maalum kuhusu mageuzi katika Sekta ya
Madini; tulikubaliana na hili nafikiri hata Mheshimiwa Rais alilisemea siku moja, kuhusu kuweka
uzio. Hili lilikuwa ni pendekezo la Kamati ya Nishati na Madini, ndani ya Bunge na tukaazimia
kwamba uwekwe utaratibu sasa wa kulinda madini yetu ya Tanzanite huko Mererani; na bahati
nzuri na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati amelisema hili kwamba hatuoni tija ya uzalishaji
katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako tulikubaliana kwamba iangaliwe namna nzuri zaidi
ya kuweka uzio, tanzanite inapatikana Tanzania peke yake, hakuna sehemu nyingine. Sasa
kama hatuweki utaratibu mzuri wa kuweka uzio kwenye eneo hilo, itasaidia mambo mawili;
wale walanguzi; kutorosha madini; lakini na kutokujua uhalisia wa madini yenyewe. Kwa hiyo,
bado Serikali ituletee majibu. Je, suala zima la uzio, ni lini litakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kabla kengele haijalia, Waheshimiwa Wabunge,
suala zima la ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo; wiki mbili au tatu zilizopita,
baadhi ya Wajumbe wa Kamati walikwenda Nkasi ili wachimbaji hawa wadogo wadogo
waende kupata hela yao ya ruzuku. Inasikitisha kwamba walikwenda Mpanda, kwamba hawa
wachimbaji wadogo wapate hela ya ruzuku. Wamefika kule, hela ya ruzuku haipo. Kwa hiyo,
hawa waliokwenda kule wakatumia hela za Serikali bila manufaa yoyote yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili la ruzuku ya Serikali lisitumike kisiasa kwa
sababu hawa wachimbaji wadogo wadogo wangependa zaidi wanufaike kama
tulivyokubaliana. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, mnapozungumzia kwamba mnakwenda
kutoa ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo, basi iwe kwenda kutoa ruzuku kweli kweli, lakini
siyo kuwabeba kutoka maeneo ya huku na huko, halafu wanakwenda kwenye eneo husika
wasikute chochote kile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iyatekeleze haya, lakini tunapenda zaidi
tuwe tunapata mrisho nyuma kwa yale ambayo Bunge linapitisha ndani ya Bunge, kwamba hili
limetekelezeka, hili halijatekelezeka; ili tuweze kuishauri vizuri Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono taarifa zote
mbili.