Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kuweza kupata fursa hii ili niweze kutoa maoni yangu kufuatia ripoti ya Kamati ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nionyeshe masikitiko yangu ya kwamba katika ripoti hii ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ni robo moja tu ndiyo tumeletewa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu. Tuko robo ya tatu sasa hivi kwa hiyo nilitarajia kabisa tungeweza kupata mpaka robo ya pili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017. Cha kusikitisha zaidi tunaona ni kwa kiasi gani bajeti hii haitekelezeki kama vile ambavyo tuliletewa hapa. Ikumbukwe wakati tumeleta hii bajeti mwanzoni nilisema kabisa kwamba hii bajeti haina uhalisia na nitashangaa sana kama hata itafikisha asilimia 70 ya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongea hivi leo, fedha za maendeleo hazijakwenda kwa kiasi kikubwa sana lakini zaidi madeni. Juzi wakati Waziri anatoa kuhusu hali ya madeni na hapa nisikitike kidogo kwa mwanafunzi wangu Stanslaus anasifia kwamba wanalipa sana madeni. Nizungumzie tu baadhi ya haya madeni ya Watanzania wa ndani ambao wanaidai Serikali na inapelekea hata hawa Watanzania wanauziwa mali zao na wengine wanajiua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa aliyotoa Waziri mwenyewe hapa ndani anaeleza kabisa kwamba mathalani wakandarasi wanadai shilingi trilioni moja, bilioni moja na milioni mia nne na mpaka sasa hivi wamelipa tu shilingi bilioni 360. Wanaotoa huduma za ndani wanadai shilingi bilioni 237 na wamemaliza kulipa shilingi bilioni 11 tu. Wazabuni wanadai shilingi bilioni 900 na kwa mujibu wa taarifa ya Waziri ya tarehe 19 wamelipa shilingi bilioni 49 tu. Hivi tunavyoongea hawa watu wanaotoa huduma hospitalini, shuleni, majeshini wanasitisha kwa sababu Serikali mmeshindwa kuwalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti sasa ningependa kujua mkakati wa utekelezaji wa ulipaji madeni haya ukoje. Jana mnasema madai ya Walimu mnafanya uhakiki yaani sasa hivi Serikali inajificha kwenye kufanya uhakiki. Madeni ya pembejeo tunafanya uhakiki, madeni ya Walimu tunafanya uhakiki, madeni ya wazabuni mnafanya uhakiki, kuajiri watu mnafanya uhakiki, muwe wazi mseme Serikali haina fedha ili Watanzania wajue kwamba Serikali haina fedha, kama wanauziwa mali zao ni kwa sababu Serikali haitaki kuwalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho kinasababisha hata Serikali isipate mapato kama ilivyokuwa ime-project, tulisema hapa kuna kodi zingine mmeziweka ambazo hazina uhalisia, hazitekelezeki, kodi kwenye sekta ya utalii, kodi kwenye transit goods. Ikasikitisha zaidi Mheshimiwa Rais anasema kabisa ni bora aje mtalii mmoja lakini alipe kodi, waje watalii wachache walipe kodi kuliko kuacha tusiweke hizi kodi ili watalii waje wengi. Mtalii akija alikuwa analipa hiyo kodi, akilala hotelini analipa na sehemu zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa tumewekeza kimkakati kwenye utalii kuhakikisha tunakuwa na angalau watalii hata milioni tatu, milioni nne ingesaidia kwani ni sekta pekee ambayo inatoa ajira nyingi, ni sekta pekee ambayo ingekuwa inaingiza fedha za kigeni. Leo Tanzania tuna vivutio vingi sana, tuna utalii wa fukwe, ukilinganisha hata na Afrika Kusini tu, wenzetu on average wana watalii zaidi ya milioni 15 sisi Watanzania eti milioni moja, halafu tunakaa hapa tunafikiri nchi yetu itaenda, tuna utalii wa kila aina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Afrika Kusini pale Soweto utakuta watu wamepanga foleni kuangalia sehemu aliyoisha Baba wa Taifa Mandela lakini hapa kwetu ukienda Butiama ambayo ni makumbusho ya Baba wa Taifa utashangaa. Uwanja wa ndege wa Musoma tumesema mturekebishie ili watalii waweze kwenda pale watu wanaenda kujenga Chato, ndiyo vipaumbele! Yaani badala uboreshe Musoma, uboreshe na kwa Baba wa Taifa ili watalii waje wengi kwenye makumbusho unaenda kujenga Chato! Vipaumbele vya nchi hii, inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke mkakati wa kuhakikisha angalau tunapata watalii milioni tatu, milioni nne, Taifa letu litasonga mbele. Tuna vivutio vingi sana, eti vi-table mountain vya South Africa, sisi tuna milima mingi tu hapa, tuna fukwe nyingi. Leo Brazil fukwe zao wanazitumia vizuri sisi Watanzania tupo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, uwekezaji kwenye bahari kuu, wanasema Chenge report na vitu kama hivyo. Serikali ingeamua kujielekeza kutafuta wawekezaji kwenye uvuvi wa bahari kuu ingekuwa ni chanzo kingine kizuri tu ambacho kingeweza kutupatia mapato. Hii ina maana wale watu wavue wale samaki, tuwe tumejenga viwanda hapa hapa waweze ku-process hapa hapa itatoa ajira nyingi lakini pia tukisha-process na ku-pack tutasafirisha ina maana tutapata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote hayaonekani kama ni chanzo, tunabaki kusubiria Watanzania wakamatwe kwa boda boda, matrafiki siku hizi wanakaa kwenye magari wanasema kabisa sijui mnawa-promote, leo nimekusanya shilingi bilioni moja kutokana na makosa ya barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi huko mikoani, walala hoi waendesha pikipiki wanakamatwa, Tarime mfano hata tumeona Mheshimiwa Lacairo wa Rorya analalamika, mtu ameajiriwa na kapikipiki kake unamwandikia faini Sh. 90,000 atoe wapi wakati mwisho wa siku anatakiwa apeleke Sh.10,000 kwa tajiri wake, akishindwa pikipiki inachukuliwa na magari hivyo hivyo. Yaani sasa hivi Serikali hii ya Awamu ya Tano chanzo kikuu cha mapato ni kupitia makosa ya barabarani, aibu! Kama Taifa tuwekeze kwenye bahari, viwanda viwe vikubwa, kama nilivyosema vichakate hapa hapa, ajira zitapatikana tutasafirisha nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kingine cha mwisho ni kilimo. Zaidi ya Watanzania 80% wamewekeza kwenye kilimo lakini kilimo chetu hakina tija kwa sababu hata vichocheo vya kuhakikisha kilimo kina take over vyenyewe bado viko hoi. Huwa tunaimba hapa kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kwa sababu mimi nikilima niko kule kijijini lazima niwe na barabara ambayo itanisababishia lori kubwa lifike niweze kusafirisha mazao yangu kutoka point A kwenda point B, barabara ni mbovu, hazijatengenezwa kabisa. Tunaona lami tu za kwenye highway, mkatengeneze na huko ambako ndiko wakulima wako wengi ili waweze kusafirisha mazao yao kutoka vijijini kuja mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ni umeme. Kaka yangu hapa Profesa Muhongo alisema ame-invest kwa mwaka huu ni zaidi ya shilingi trilioni moja na bilioni mia ngapi kwamba tutaona umeme unawaka vijijini. Ni matarajio yangu kwamba tutaona umeme unawaka huko ili hao wakulima wanaolima waweze kusindika yale mazao yasiharibike, waweze kujenga viwanda vidogo vidogo kuviongezea thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiwa na umeme, tukiwa na miundombinu mizuri ya barabara, maji yakawa yanapatikana tutaweza kuona kweli tunasonga mbele vinginevyo hatutaweza kuwa na mapato kabisa. Tutakuja hapa tunatoa bajeti, mapato ni hayo unaelekeza kwenye vinywaji, unaelekeza kwenye vikodi vya utalii kwa hiyo watalii hawaji mnakosa, tuwe na watu ambao wamesomea mambo haya waweze kuishauri Serikali na kuleta bajeti ambayo inaakisi uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimekuwa nawatetea sana hawa ndugu zangu wa Magereza. Naambiwa Askari Magereza wanaidai Serikali kuanzia mwaka 2012/2013, 2013/2014, 2015/2016 ndiyo nimesikia sasa hivi mmewapelekea ya 2015/2016 nataka kujua 2012/2013 na 2013/2014 ni lini mtaenda kuwalipa? Pia tuweze kujua fedha za kuweza kufidia yale maeneo ambayo mmechukua…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.