Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata hii nafasi ili kuweza kuchangia katika taarifa hii ya Kamati. Kwanza naipongeza sana Kamati kwa taarifa nzuri ambayo wameiandaa ambayo na mimi pia ni Mjumbe wa hii Kamati, kwa hiyo nashukuru sana kwa taarifa nzuri hii.
Mheshimwa Mwenyekiti, tunapozungumzia maendeleo na tunapotaka maendeleo ya nchi lazima tuangalie ni vipaumbele gani ambavyo vitaashiria na vitafanya nchi ionekane imeendelea. Nasema hayo nikianzia na suala la kilimo. Katika kilimo asilimia zaidi ya 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, nchi yetu hii tumesema tunataka sasa kujenga nchi ya viwanda, hatuwezi kujenga nchi ya viwanda, hatuwezi kukamilisha hilo kama hatutaimarisha kilimo. Viwanda vinategemea malighafi na malighafi hizo lazima zitoke kwenye kilimo. (Makofi)
Hata ukiangalia nchi za wenzetu, ukiangalia Ulaya industrial revolution ya Europe ilianzia kwanza na agricultural revolution, ilianzia kwanza na mapinduzi ya kilimo; mapinduzi yale ya kilimo yakaleta mapinduzi ya viwanda. Kwa hiyo, tunaposema maendeleo lazima tuweke tuzungumzie bayana kabisa, tuwe na mkakati wa makusudi wa kuimarisha kilimo chetu na ambacho ndicho kinatoa ajira kwa watu wengi, ambacho ndiyo kitatupatia malighafi za kutosha kwenda kwenye viwanda na kitachangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, hivi sasa kilimo chetu kinategemea mtu mmoja mmoja kilimo kidogo, hii haitatupeleka mbele kama Taifa. Lazima pia tuweke mkakati wa makusudi wa kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo yatakayosaidia katika kuimarisha Pato la Taifa.
Mheshimwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumzia kilimo nchi yetu sasa inakabiliwa na ukame katika maeneo mengi ambao tunaamini itaathiri kwa kiwango kikubwa sana maendeleo yetu ya kilimo. Mikoa ya Nyanda za Juu kama kule kwetu Songwe sasa hivi bado mvua zinanyesha na tena zinanyesha vizuri sana na wananchi wamelima mazao yanakwenda vizuri, tatizo lipo kwenye pembejeo, pembejeo sasa hivi kule Mkoani Songwe zimepanda vibaya sana. Katika kipindi cha nyuma Serikali ilitamka kwamba kwa mfano mbolea ya kukuzia ingeuzwa shilingi 26,000 lakini hivi leo ninapoongea pembejeo zimepanda sana kule Mbozi, mbolea ya kukuzia ni zaidi ya shilingi 50,000, sasa hii itasaidiaje? Hatuwezi kuendelea kwa namna hiyo. Kwa hiyo, naiomba Serikali itafute uwezekano wa kusaidia kilimo ili angalau tuweze kuinua pato la Taifa na kutoa ajira kwa wananchi walio wengi, hilo ni suala la kwanza.
Mheshimwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu usimamizi wa bajeti na nidhamu ya bajeti. Mimi nashukuru uchambuzi wa Kamati ulivyofanywa, lakini naomba nitoe ushauri wangu, fedha nyingi zinatoka kwenye Wizara ya Fedha, zinapopelekwa kwenye Serikali za Mitaa na kwenye taasisi za umma ni namna gani Serikali inasimamia na kufuatilia kwamba hizo fedha zinatumika kama zilivyopangwa, hilo ni suala la msingi sana.
Mheshimwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na tabia kwamba katika baadhi ya maeneo watu wamekuwa wakibadilisha matumizi ya bajeti kinyume na Sheria ya Bajeti, hii siyo sawasawa. Mimi naamini Bunge baada ya kuidhinisha bajeti, bajeti inatakiwa itumike kama ilivyo na kama kuna mabadiliko basi hatua zinazoweza kuchukuliwa zifuatwe, kuliko sasa hivi mabadiliko ya bajeti yanatokea, bajeti tunapanga hapa inakuwa sasa haitekelezeki, kwa kweli hiyo itakuwa haitusaidii kama nchi, ni vema tukawa na msimamo na tukasimamia vizuri bajeti ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, lazima tuweke vipaumbele vichache vinavyoonekana kwamba kwa mwaka huu tunataka tuwe na kipaumbele gani? Tusichukue vipaumbele vingi, hiyo itatufanya kwamba tusionekane kama mwaka huu kipaumbele ni kusambaza maji tuhakikishe mwaka huu tunasimamia kusambaza maji. Kwa hiyo, bajeti ya maendeleo ilenge katika hayo maeneo, mwaka unaofuata tunaelekeza tena upande mwingine, hiyo, itatusaidia sana katika kuweza kuharakisha kuleta maendeleo na kuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha.
Suala lingine ambalo ningependa kuchangia linahusu mapato yasiyotokana na kodi. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuvuka malengo ya mapato yanayotokana na kodi kwa kweli naipongeza sana Serikali. Katika mapato ambayo hayatokani na kodi yaani non-tax revenues tumeweza kufikia asilimia 54; sasa asilimia 54 ni ndogo. Lazima tuwe na mikakati ya kutosha, tuchukue hatua zinazowezekana kuhakikisha kwamba tunaimarisha hili eneo maana lina vyanzo vingi, tunaweza tukapata mapato mengi.
Mheshimwa Mwenyekiti, ninaamini kama tukisimamia vizuri mashirika ya umma yakafanya kazi yao inavyotakiwa, yakafanya kazi kwa ufanisi, mashirika kama EWURA ambao wanakusanya fedha nyingi, mashirika kama TCRA, Civil Aviation, Reli, Shirika la Ndege na Bandari. Tukisimamia haya mashirika vizuri yataisaidia sana nchi hii kuweza kupata fedha na kupata mapato mengine yasiyokuwa yana kodi. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nchi nyingi zinahitaji kuwa na bandari; sisi tuna bandari nzuri. Bandari yetu ile tukiimarisha nina uhakika kabisa tunaweza tukapata fedha nyingi sana na ikiwezekana mara mbili ya bajeti tuliyonayo, lazima tuweke mkakati wa kutosha katika kuhakikisha hilo eneo tunafikia malengo. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nichangie pia kwenye eneo la ulipaji mzima wa kodi. Mimi naamini Watanzania lazima tuwe ni wazalendo wa kweli. Sasa hivi elimu ya mlipa kodi bado haitoshi, wananchi walio wengi bado elimu haitoshi ya ulipaji kodi. Katika maeneo mengi mimi nimeona pamoja na jitihada za Serikali, pamoja na mkazo ambao umekuwa ukitiliwa katika kukusanya kodi na watu kuwahamasisha maeneo mengi ukienda dukani mtu anakuuliza; nikupe risiti au nisikupe risiti? Risiti ni haki, risiti ni wajibu wa kila mtu kutoa na wanapopanga bei zao lazima wajue kwamba kuna wajibu wa kulipa kodi, kwa hiyo, lazima hilo lizingatiwe.
Mheshimwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Fedha iweke mkakati kwamba, sisi Viongozi wa Siasa, Wizara ya Fedha na Serikali lazima tufanye jitihada za makusudi za kuhamasisha ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kulipa kodi, bila kulipa kodi hatuwezi kuleta maendeleo, tutakuwa tunaimba tu. Lazima wananchi wetu walipe kodi na lazima tuisimamie vizuri.
Mheshimwa Mwenyekiti, VAT (Value Added Tax) nina uhakika kama tutaisimamia vizuri itasaidia sana……
Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.