Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kupata fursa hii ya kuchangia kwenye hoja hizi mbili muhimu. Nikushukuru wewe kwa kunipa fursa na pia niwashukuru Wenyeviti wa Kamati hizi mbili kwa taarifa zao muhimu sana wakati Bunge linapotekeleza jukumu lake la kikatiba la kuishauri na kuisimamia Serikali. Mimi kwa moyo mmoja niseme kwamba naunga mkono hoja za Kamati hizi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichosemwa katika taarifa hizi zote mbili ni cha kweli. Nilikuwepo wakati Mheshimiwa Shangazi anachangia kilichojiri juu ya hadhi na mazingira ya kazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipokuwa anazungumza kuhusu Mbunge mmoja aliyezimia alisema ni Wizara ya Katiba lakini ukweli ilikuwa ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, hii inaonesha ni kwa kiasi gani hizi taarifa zimezungumza ukweli. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamepata fursa ya kuchangia hapa kuisaidia Serikali iweze kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushauri, imetolewa hoja kwa mfano juu ya wafungwa wa kunyongwa, wanaitwa condemned kwamba labda wanakaa sana pale na hawanyongwi labda tubadilishe sheria, hapana. Mamlaka haya yapo kwenye Katiba, Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo imempa Rais mamlaka ya kusamehe kosa lolote lile hata hilo la kunyongwa au kuwashushia adhabu. Inategemea kwamba hawa waliotumia fursa yao kutokuwanyonga wametumia mamlaka yao ya Kikatiba halali kabisa. Pia hatuwezi tukafuta hili kwa sababu anaweza akaja Rais mwingine akasema aah aah, hawa wawe wananyongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge Law Reform Commission, ile Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ilishafanya utafiti hii miaka ya karibuni tu kwamba hii adhabu tuiondoe au tusiiondoe? Wananchi walisema hii adhabu ibaki pale. Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliwahi kusema kwamba hii ni adhabu halali kwa hiyo, iko pale. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wale watu kuwepo pale isitufanye tukawa na nia ya kutaka kurekebisha ile sheria. Hilo la kwanza niliomba nichangie kwenye hilo.Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, imezungumzwa juu ya ukiukwaji wa taratibu na Sheria za Uchaguzi wakati wa uchaguzi wa Madiwani. Wote tunajua utaratibu, kama sheria au utaratibu umekiukwa, ushauri wangu tu ni kwamba yule ambaye anaona taratibu zimekiukwa basi anaweza akaenda Mahakamani akafungua shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi. Ndivyo tulivyofanya hata katika uchaguzi mkuu, huo ndiyo utaratibu. Ndiyo ushauri wangu kwenye suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limezungumzwa pia na Mheshimiwa Mussa na amelizungumza kwa hisia, hata mimi linanihusu, linaumiza. Wakati fulani unaenda gerezani unamwona mama ana mtoto mdogo na mimi nimeenda sana magerezani. Nimemsikia Mheshimiwa Mwamoto akizungumzia lile Gereza la Kahama pale, mimi nilienda pale kwa mara ya kwanza Desemba, 2003 nikiwa na Waziri Mwapachu, wakati huo mimi ni msaidizi wake, Mzee Mwapachu alilia machozi kutokana na hali iliyopo pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali imechukua hatua imeboresha hali hii. Kifungu cha 144 cha Sheria ya Mtoto sasa kinaweka utaratibu wa namna gani mama aliye na mtoto gerezani anapaswa atendewe. Siwezi kutafsiri kwa Kiswahili hapa, lakini nisome, kinasema hivi:-
“(1) Where a mother is in prison with her child under any circumstances, all measures shall be taken by the prison authorities to ensure that the child receives the required child care in the form of adequate diet, nutrition and child health care including immunization”.
(2) The prison authorities shall inform the District Social Welfare Officer about the child who is in prison with his mother and who is no longer breastfeeding.
(3) Where the social welfare officer has received information from the prisons authority, he shall determine the most suitable place for the child, which may be –
(a) the parent who is not in prison;
(b) a relative;
(c) a guardian; or
(d) a fit person;
(4) In the absence of persons referred to under subsection (3), the Social Welfare Officer shall cause the child to be admitted in an approved residential home until such times when the mother is discharged from prison.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sheria ya Serikali tayari imeshaweka utaratibu wa aina hiyo. Hata hivyo, tunakubali ushauri ambao umetoka kwa Mheshimiwa Mussa kwenye suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumzwa hapa ni hii hoja ya msongamano wa mahabusu magerezani na ni kweli Wabunge wamesema kwa hisia. Sisi jana tulikuwa pale Dar-es-Salaam kwenye Law Day na ndicho ambacho pia Rais amesisitiza sana. Taasisi za umma ambazo zimepewa majukumu ya kusimamia administration ya justice tutekeleze majukumu yetu kwa ufanisi. Kama ni Mahakama hivyohivyo, kama ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni hivyohivyo, kama ni Jeshi la Polisi hivyohivyo, kama ni Jeshi la Magereza hivyohivyo, kila mmoja awajibike. Kwa hiyo, nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge ambao wamesema kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo pengine ningeomba kulichangia, limezungumzwa hapa suala kuhusu kauli za Rais. Kwanza niseme hivi, kwa kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 18(a) inatamka kwamba kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; inawezekana kwamba baadhi ya wananchi mara nyingi labda wanatafsiri hizo kauli za Rais kwa sababu ya kutumia haki hii. Nilivyokuwa nasoma Lake Secondary, Mwalimu mmoja alitufanyia zoezi akasema hivi, kadri habari inavyotoka kwa mtu mwingine kwenda kwa mtu mwingine ndivyo inavyobadilika. Akatufanyia zoezi, akamnong‟oneza kitu mwanafunzi wa kwanza kwenye dawati pale, yule wa mwisho kabisa alikuja na taarifa tofauti kabisa na alichoambiwa na Mwalimu na mengine haya huwa tunayasikia wakati hata sisi hatukupata kusikiliza kitu kama hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwanza Mheshimiwa Rais anatambua na anazingatia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola. Pili, anatambua na kuzingatia utawala wa sheria…
Anachokifanya Mheshimiwa Rais ni kuhimiza utawala wa sheria na uwajibikaji wa taasisi na vyombo vya umma na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao na hili ni sharti la msingi.
Kwa sababu hata Ibara ya 26 ya Katiba ndiyo inayoweka utawala wa sheria na ndicho Rais anachosisitiza na hata jana amesisitiza sana na hili lilikuwa liko wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa hiyo, anachokisisitiza Mheshimiwa Rais ni utawala wa sheria na hata jana amesisitiza sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tekelezeni majukumu yenu kwa ufanisi, Mahakama hivyohivyo, Magereza hivyohivyo, Polisi hivyohivyo, TAKUKURU hivyohivyo. Sasa huyu ndiyo ana mandate, ndiyo Mkuu wa Nchi ana wajibu wa kutusisitizia. Anaposisitiza kauli zake wakati fulani kwa sababu ya uhuru huu wa Kikatiba ya kuwa mtu na fikra na mawazo yake anaweza kuwa ameelewa vibaya akamtafsiri vibaya lakini ukweli ni kwamba Rais bado yuko kwenye Katiba anatekeleza tu wajibu wake kwa ufanisi. Ibara ya tisa inatukumbusha kwamba mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera ya shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa mara nyingine tena nikushukuru na naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.