Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda kuwapa pole sana wananchi wangu wa Mji wa Tunduma kwa ajali ya moto ambayo imetokea katika soko kuu la Mji wa Tunduma na kuteketeza maduka mengi ambayo wamepoteza mali zao nyingi sana, nawapeni pole sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze na suala la utawala bora katika nchi hii. Nchi hii utawala bora kwa kipindi cha Awamu ya Tano inaonesha kabisa utawala bora katika nchi hii sasa umetoweka kabisa. Nasema kwamba utawala bora umetoweka, sasa hivi hali ya watumishi katika nchi hii imekuwa ni tete, kila mtumishi amekaa akisubiri matamko, ana wasiwasi na shughuli ambazo anakwenda kuzifanya, haamini kama kesho ataamka akiendelea kuwa mtumishi wa umma katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hali ilivyo katika nchi hii sasa hivi. Jeshi la Polisi sasa wanakamata watu hovyo hovyo, Jeshi la Polisi wanaagizwa, Jeshi la Polisi wanasema wameshindwa kufanya kazi zao bila maagizo kutoka juu, hili jambo tumeliona hata kwenye uchaguzi uliopita. Katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, Madiwani na Wabunge tumeona hali ilivyokuwa tete katika uchaguzi huu. Imeonesha kabisa kwamba katika kituo cha uchaguzi hasa siku ya kupiga kura walikuja Polisi wengi ambao walikuwa wana mbwa na silaha nyingi kabisa, kiasi kwamba waliwatisha wapiga kura lakini pia walizuia hata Mawakala ambao walikuwa wanatakiwa kuhakiki uhesabuji wa kura wasiingie katika vituo vya kupigia kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba kutokana na jambo hili, hata leo Chama cha Mapinduzi wanajinafasi kwamba wamepata kura nyingi na wameshinda lakini tunataka kusema kwamba asilimia kubwa ya matokeo yaliyojitokeza yanaonesha kabisa yalihujumiwa. Tunasema yalihujumiwa na hili tunalizungumza hapa watu wengi watazomea na wataona ni jambo ambalo kama vile tunatania, lakini tunazungumza ukweli na hili lina mwisho. Itafika mahali Watanzania watachukia na watakataa dhuluma pamoja na uonevu unaojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana jambo la uchaguzi na jambo la haki za watu wanapokwenda kupiga kura ni lazima lilindwe. Sheria za nchi sasa hivi hazifuatwi na viongozi wengi wanakaa madarakani kwa sababu eti amesimamia vibaya uchaguzi na kuiba kura kuhakikisha kwamba CCM wanashinda uchaguzi. Jambo hili linasumbua sana na watu sasa hivi wameanza kukata tamaa ya kwenda kupiga kura.
Mheshimiwa Mweyekiti, nikupe mfano mmoja; Kata ya Kijichi wapiga kura walikuwa karibuni 16,800 mwaka 2015 kwenye Uchaguzi Mkuu lakini safari hii wapiga kura waliojitokeza ni 5,000 tu. Hii inaashiria kwamba Watanzania wameanza kukata tamaa na wanaona hawana haja ya kwenda kupiga kura kwa sababu hata wakipiga kura, kura zao na matokeo yao yanahujumiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunataka kusema kwamba ni vizuri pia Serikali hii ikajua kwamba hizi ni haki za watu na watu wanavyokwenda kufanya uchaguzi, waacheni wafanye uchaguzi wamchague kiongozi wanayemtaka atakayeweza kuwaongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine imetokea sasa hivi, kila jambo linalozungumzwa na mtu hata kiongozi akisema kwake kuna njaa wanasema umekuwa mchochezi. Ni vizuri Serikali ikajaribu kutoa ufafanuzi, uchochezi maana yake nini? Jambo la kweli ambalo linazungumzwa nalo limeshakuwa uchochezi. Nchi hii watu watashindwa kuzungumza, watakaa kimya na wakikaa kimya tunakoelekea siyo kuzuri hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa kwenye kampeni maeneo mbalimbali. Ukizungumzia hali halisi ya chakula katika nchi hii nashangaa baadhi ya viongozi ndani ya Serikali hii wamekwenda kutoa matangazo katika mikoa mbalimbali kwamba mtu yoyote atakayesema kwamba kuna njaa anatakiwa kukamatwa. Haya ni mambo ya ajabu kabisa. Njaa haifichiki hata siku moja, njaa iko wazi.