Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza na mimi nizipongeze Kamati zote kwa uwasilishaji mzuri, lakini ntajikita kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea kidogo suala la asilimia 10 ya vijana na akinamama. Suala hili limekuwa mara nyingi likiongelewa na Waheshimiwa Wabunge wakilalamika kwamba fedha zile hazipatikani katika halmashauri. Kwa hili kidogo nitofautiane na mawazo ya Kamati, kwamba iletwe sheria Bungeni ya kuzilazimisha halmashauri zitenge fedha hii. Halmashauri zetu hazina fedha za kuendesha shughuli zake za kila siku, leo tukipanga kuzitengenezea sheria ya kuzilazimisha zitenge fedha hii maana yake tunataka kuzimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Kamati ingeshauri Serikali ihakikishe Fedha za Matumizi ya Kawaida (OC) zinapatikana katika halmashauri zetu ili fedha za OC zikipatikana zisaidie zile fedha za ndani zinazokusanywa kupangwa katika asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya akinamama, lakini kulazimisha halmashauri kupata maziwa ya kulisha halmashauri zao mpaka ipatikane damu ni vigumu sana. Kwa hiyo, naomba hili kKmati kidogo iliangalie katika sura nyingine pamoja na maoni mazuri ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi halmashauri zina wajibu mwingine mkubwa wa kutenga fedha katika Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017. Yote hiyo ni wajibu wa halmashauri na hizo fedha ni lazima zitengwe, lakini halmashauri hazina uwezo wa kujiendesha. Vyanzo vya halmashauri vingi vimechukuliwa na Serikali Kuu, halmashauri zinajiendesha vipi? Utaratibu wa makusanyo ya halmashauri wenyewe umebadilika mno kutokana na maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa Bunge la Bajeti tulishauri hapa, katika maeneo ya manispaa na majiji yale makusanyo yaliyokuwa yanafanywa na mawakala yaliyofanyiwa tathmini na Benki ya Dunia kwa miaka zaidi ya 10 yasibadilishwe utaratibu wake kwa sababu Halmashauri nyingi zitadhoofika katika makusanyo ya mapato, lakini kwa bahati mbaya, wakati mwingine kwa kiburi cha wakubwa, mlikataa kusikiliza. Leo halmashauri nyingi zimeshindwa kutumia mawakala katika kukusanya fedha katika mpango wenu wa kutumia commission, halmashauri zinajiendesha vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusije tukakaa hapa tukizilaumu halmashauri tukiwalaumu Wakurugenzi bure wakati sisi wenyewe ndio tumewabana tukashindwa kuwafanya waweze kutimiza wajibu wao, Wabunge ni sehemu ya Madiwani, ni vizuri mjue shida ambazo Wakurugenzi na Madiwani wanazo katika Halmashauri zenu ili mkizungumza muwe mnaelekeza, maana wakati mwingine Serikali inavua majukumu yake na lawama zake inataka kuzihamishia kwenye halmashauri peke yake. Kwa hiyo, nadhani kwamba kwa hili Kamati ingeangalia vizuri na Serikali ni vizuri ikaangalia vizuri namna ya kuziboresha na kuimarisha Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mimi naendelea kusisitiza kwamba dhamira ya Serikali Kuu katika kuimarisha Serikali za Mitaa bado haijawa nzuri sana, ni vizuri Serikali Kuu iangalie mtazamo wake na dhamira yake ya kuimarisha Serikali za mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mdororo wa elimu pamoja na dhamira ya Serikali ya kutoa elimu, sijui bure ama bila malipo – maana mpaka sasa sielewi terminology halisi ni ipi, ni elimu bure ama ni elimu bila malipo. Nashauri kwamba miundombinu sio mizuri, lakini hata kama tukiimarisha miundombinu ya elimu ni vizuri tuangalie namna ya kuzisaidia shule za Serikali. Shule za Serikali hazifanyi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro kwa mfano, tulikuwa tuna utaratibu wa kuwalisha watoto chakula wakati wa mchana shuleni, chakula cha kawaida kabisa, lakini wazazi walikuwa wanalazimishwa kutoa michango kwa ajili ya kuhakikisha watoto wao wanakula shuleni. Baada ya tamko la Serikali la elimu bure mindset za wazazi na wananchi zikaamini kwamba sasa hawapaswi tena kuchangia chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri mkaainisha, mkitamka elimu bure mmedhamiria nini? Inawezekana mmedhamiria ada, kwamba wazazi hawatalipa ada ile ya sh. 20,000 katika shule za kutwa na shilingi 70,000 katika shule za mabweni, maana shule za msingi hazikuwa na ada. Ni vizuri mka-specify mnazungumzia nini katika suala la elimu bure ama elimu bila malipo ili wananchi waelewe Serikali hasa ni nini ambacho haichangii na wananchi wanapaswa kuchangia nini ili watimize wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya nchi hii ilikuwa ya ujamaa na kujitegemea, bado mmeandika kwenye Katiba kwamba iko hivyo kwa sasa. Wananchi mindsets zao ni hivyo hivyo kwamba nchi hii ni ya ujamaa na kujitegemea, kwa hiyo huduma zote zinatolewa na Serikali. Wananchi ndio tulikuwa tunawabadilisha kidogo wafahamu kwamba na wao wana wajibu wa kuchangia baadhi ya huduma. Leo mnakuja na propaganda za kisiasa za elimu bure, matokeo yake mnawabadilisha wananchi wanatoka walipokuwa wanakwenda mbele mnawarudisha nyuma bila kuwa na fallback position kwamba mnawasaidiaje katika hatua hizo. Kwa hiyo, ndugu zangu nafikiri Waheshimiwa Wabunge waliangalie hili kwa mapana ili waone namna ya kulisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora. Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, tukiwalaumu tunawaonea bure kwa sababu nimeona hata spirit ya Waziri wa Ofisi ya Rais ,TAMISEMI, ndiyo hiyo hiyo ya udikteta fulani na ndiyo maana anaweza akasema ni halali Wakuu wa Mikoa kufanya wanachoweza kufanya kusumbua viongozi wenzao katika maeneo mbalimbali, sasa inaonekana maelekezo ya nini wafanye Wakuu wa Mikoa yametoka juu, si maamuzi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri sana kwamba ni vizuri ninyi viongozi wa juu mbadilike, badilisheni mwelekeo wenu. Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwepo, ya Awamu ya Tatu ilikuwepo, Wakuu wa Mikoa kweli hawakuwa hivyo, walikuwepo wala Katiba haijabadilika, wajibu wao baina yao na Halmashauri unaeleweka na wanaujua, ni kwa nini Serikali ya Awamu ya Tano Wakuu wa Mikoa ndiyo wabadilike, wamezaliwa upya, wameanguka kutoka mbinguni? Kwa nini waende kukamata watu, wakamate Walimu, wakamate Madaktari, wawaweke ndani kama wanaweka ng‟ombe na mbuzi na ninyi mnaangalia mnaona jambo la kawaida? Kwa nini mnaondoa ule moyo wa wafanyakazi na watumishi kufanya kazi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikaliangalia hili jambo kwa uzito wake ili wafanyakazi wale wafanye kazi kwa moyo. Wafanyakazi na watumishi katika maeneo mbalimbali hawana moyo kwa sababu ya maelekezo mnayowapa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, wamepoteza mwelekeo wa wajibu wao kabisa, sasa hivi wamekwenda kuvuruga kabisa mikoa na wilaya zao na halmashauri, kwa hiyo ni jambo la msingi sana kuliangalia katika uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la rushwa. Rushwa imekuwa ni utamaduni katika nchi hii kwa muda mrefu, lakini inavyoonekana kuna jitihada ambazo inaonekana zinafanyika ambazo huwezi kukwepa kuziona kwamba ni za muhimu, lakini jitihada hizi zinafanywa na mtu mmoja; inakuwa ni one man show kwamba anayeweza kupambana na rushwa ni mtu mmoja, ni Mheshimiwa Rais. Hajaweza kuimarisha mifumo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante na naomba kuwasilisha.