Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa hii, lakini zaidi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuendelea kuishi na kuweza kuchangia katika Bunge hili Tukufu.
Kwanza kabisa niseme naunga mkono hoja, nawashukuru Wizara ya Fedha kwa kuja na Mapendekezo haya ya Mpango. Pia nawashukuru Wabunge wote kwa kuhudhuria na kushiriki kikao hiki, lakini pia na kupata fursa ya kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuzungumza hoja chache zile ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezisema. Moja, nimalizie pale alipoishia Mheshimiwa Mwakyembe kwamba haya ni mapendekezo katika kipindi hiki hatuhitaji Sheria; ile Kanuni ya 94 ipo wazi kabisa, lakini baadaye Mpango ukisoma sasa Kifungu cha 20 cha Sheria ya Bajeti ya Mwaka 2015 na Kifungu cha 26 cha Sheria ya Bajeti, Mpango huu utakapoletwa mahususi wenyewe ndiyo msingi wa kutengenezea Bajeti. Halafu baadae Bajeti inapokuja kutengenezwa ndiyo inatengenezewa Sheria ya Appropriation Act, Sheria ya…
Kwa hiyo, nafikiri niiweke hii wazi kwa baadhi ya Wabunge ambao walikuwa wamefikiri kwamba Serikali imekosea kutokuja hata na Sheria.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Niliona nilitolee ufafanuzi hili kwa sababu baadhi ya Wabunge walikuwa wanajiuliza kwa sababu hawaoni hata Muswada wa Sheria! Nimeona niliweke wazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo naomba kuliongelea ni suala la Zanzibar. Suala hili ni suala nyeti kwa mustakabali wa Taifa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Serikali mbili na hizi Serikali uwepo wake ni Katiba; kuna Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ibara ya (4) ya Katiba hiyo siyo tu inaweka mgawanyo wa madaraka katika mihimili mitatu ya dola, lakini pia, inaweka mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na imeelezwa vizuri na kuna mambo ya Muungano na ambayo siyo ya Muungano. Kwa hiyo, Katiba ya Zanzibar sio ya Muungano, ila Katiba ya Jamhuri ni ya Muungano na Katiba ile ya Zanzibar ndiyo inazaa Tume ya Uchaguzi ambayo inasimamia uchaguzi Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kile ambacho baadhi ya Wabunge wamekisema hapa, ni kama kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano iingilie mamlaka ya Zanzibar! Tafsiri yake ni kwamba kama unataka kuleta hoja ya kujengwa Serikali moja, lakini kwa mujibu wa Katiba ni Serikali mbili. Sasa tukienda kwa namna hiyo tutakuwa tunavunja siyo tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano, lakini pia Katiba ya Zanzibar. Serikali haiwezi ikakifanya hicho na kuwepo kwa Serikali yoyote ni Katiba!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja ya kusema kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano iingilie kule, Rais Magufuli aingilie, ana mamlaka tu yeye kuingilia mambo ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na mpaka sasa kule Zanzibar kuna amani, Rais anafanya kazi yake vizuri, utengamano ni mkubwa kabisa na usalama upo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo nishauri Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapochangia suala la Zanzibar lazima tuheshimu mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tuchangie kwa namna ambayo si ya kuhamasisha uvunjifu wa amani, uhaini au kuvunja umoja na mshikamano! Ikitokea uvunjifu wa amani hapa hakuna yeyote atakayefaidi, wala hatafaidi siasa wala kitu gani! Niliona nilishauri hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa mara nyingine tena nikushukuru na niwashukuru Wabunge wote. Naunga mkono hoja.