Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa sababu muda tunagawana, niende moja kwa moja kwenye ripoti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti mbili zimeandikwa vizuri sana na kwa ufasaha na Kamati husika. Hata hivyo, kuna mambo ambayo kwa ujumla tunahitaji sisi kama Bunge kuya-adopt na mengine kutoa ushauri kama Azimio la Bunge kwa Serikali juu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na mambo mengine katika Halmashauri na taasisi zetu huko mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo yanakwamisha miradi mingi sana katika ngazi za Halmashauri kutokukamilika. Jambo la kwanza ni maagizo ya mara kwa mara yanayotoka kwa viongozi wa juu bila kuwekwa katika bajeti za Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa katika Halmashauri zetu kumekuwa na maagizo ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa yaani Mkuu wa Wilaya anaweza kuja katika Halmashauri akatoa agizo ambalo halipo katika bajeti za Halmashauri. Matokeo yake maagizo hayo yamekuwa yakisababisha kuwepo na reallocation. Haya ni matumizi mabovu ya fedha kwani fedha ambazo zilikuwa zimepangwa kufanya kazi nyingine zinaenda kufanya kazi nyingine na matokeo yake anapokuja mkaguzi wa fedha zinaonekana fedha za Halmashauri zimetumika kinyume na vile ambavyo zilikuwa zimepangiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili nilikuwa nashauri ni lazima liingie kama moja ya pendekezo na watu wa Serikali za Mitaa pamoja na taasisi nyingine wajaribu kulichukua na sisi kama Bunge ni lazima sasa tuiambie Serikali, Wakuu wa Wilaya wajue mipaka yao ya kazi, Wakuu wa Mikoa lazima wajue mipaka yao ya kazi na wala siyo kupanga miradi ya maendeleo katika Halmashauri. Infact hata kwa ninyi viongozi wa juu kabisa wakiwemo Mawaziri na Mheshimiwa Rais, tuwashauri vizuri tu kwamba wanapotoa maagizo, kwa mfano unasema tunakwenda kwenye operation ya madawati, ni jambo jema lakini tuseme hiyo operation ya madawati ianze katika mwaka wa fedha ujao siyo katika mwaka wa fedha husika kwa sababu inatuvuruga kabisa katika ngazi ya Halmashauri. Kwa hiyo, hilo naomba tupeleke kama moja ya pendekezo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, moja ya jambo ambalo linakwamisha sana utendaji kazi huku chini katika Halmashauri zetu, huu mfumo wa uteuzi sasa hivi umekuwa ni mbovu sana. Nalisema hili kwa sababu moja, nimeshuhudia mwaka huu tumekuwa na idadi kubwa sana ya Wakurugenzi ambao hawakupitia katika utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yamekuwa yakisemwa na hili ni vizuri tukalisema vizuri. Watu wetu kule chini wanaoanza kazi katika Serikali za Mitaa kwa mfano wanaanza with an intention, anaanza kama Afisa Msaidizi Daraja la II, baadaye anapandishwa Daraja la I, baadaye anakuwa Afisa Mwandamizi, siku inayofuatia anakuwa Mkuu wa Idara, with an intention siku moja nitakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya fulani ama nitapandishwa na nitakuwa RAS. Huu mwenendo wa sasa hivi ambapo watu wamekuwa wakitolewa from no where, mtu alikuwa tu mgombea wa Chama cha Mapinduzi anateuliwa moja kwa moja kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri, imeondoa ile morale na motisha kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii niwaambie kabisa ni moja ya jambo ambao Chama cha Mapinduzi ni lazima mjirekebishe kwenye hili, limeondoa motisha kabisa kule chini. Watu wanalalamika na wananung‟unika sana kwamba yaani sisi huku tuliko tumetumikia zaidi ya miaka 30, 20, 18 nategemea siku moja nitapandishwa cheo kumbe pamoja na utumishi wangu wote uliotukuka katika Serikali za Mitaa lakini leo thamani yangu haionekani. Matokeo yake anakuja mtu from no where na mtu yule ambaye humjui uwezo wake wala utendaji wake wa kazi, ile imeondoa sana morale, hata sasa hivi morale imeshuka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima hili lieleweke kabisa kwamba kwenye masuala ya uteuzi yabaki kama Sheria ya Utumishi inavyosema, lazima mtu atumikie kwa kiwango fulani na akifikia labda miaka saba huyu anaweza kuwa qualified kuwa Mkurugenzi Mtendaji ama kuwa DAS katika Halmashauri husika. Kwa kuendelea na mwenendo huu kitakachotokea ni nini? Wale walioko wanaweza wakawakwamisha hawa wapya ambao wanateuliwa. Wakiwakwamisha hawa wapya wanaoteuliwa zinazoathirika ni Halmashauri na wananchi katika maeneo yetu tunayoongoza. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika Serikali zetu za Mitaa moja ya jambo ambalo linakwamisha sana kutokamilika kwa miradi ni Serikali kuchukua vyanzo vya mapato katika ngazi ya Halmashauri. Kwa sekunde mbili ni kwamba tabia ya hii Serikali kujirundikia, sasa hivi tumekuwa tukiona Serikali ikijisifu kuwa na mapato mengi lakini ukweli mapato yako mengi lakini yanatokana na vile vyanzo vya Halmashauri, haijaanzisha vyanzo vyake vipya. Kwa hiyo, tunachotaka waanzishe vyanzo vipya tofauti na kwenda kunyang‟anya katika ngazi ya Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo dogo la mwisho ni kwamba nimepitia ripoti ya PAC, imeandikwa vizuri lakini watu wa Benki ya TIB walikataa kuleta majina ya wadaiwa sugu ambao wanadaiwa kutokana na kukopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo. Matokeo yake ni nini? Kama wameikatalia Kamati ya PAC maana yake wamelikatalia Bunge na hii ni dharau kubwa sana kwenye Bunge lako Tukufu. Hofu hii inatokana na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kwa sababu Mwenyekiti wa sasa wa Bodi hii ni Profesa Palamagamba Kabudi, ni mtu mwenye heshima lakini inapotokea watu wanakataa kuleta majina ya wadaiwa sugu wakati benki ina madeni chechefu ambayo hayalipiki zaidi ya shilingi bilioni 78, kitakachotokea ni kama kilichotokea kwenye Twiga Bancorp. Kwa hiyo, kwa vile hizi benki ni za Serikali na hizi fedha zinatokana na kodi za wananchi, nashauri Kiti chako lazima kichukue hatua dhidi ya taasisi zozote zinazokataa kutekeleza maagizo ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa hayo machache, nafikiri dakika zangu nyingine atamalizia mwingine. Ahsante sana.