Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.

MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Spika naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa kuwa mchangiaji wa siku ya leo kuhusu mkataba wa Ubia wa uchumi baina yetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu ambao mimi nimeushika hapa mkononi ni miongoni mwa mikataba ambayo ni mibovu, ni miongoni mwa mikataba ambayo ni mibaya, ni miongoni mwa mikataba ambayo inanikumbusha enzi za miaka ya zamani. Mikataba kama hii ndiyo ambayo tulisoma kwenye historia ya akina Carl Peters na kwamba Wazee wetu wakiwemo wakina Mangungu waliweza kusaini mikataba mibovu na ya ajabu kama huu.
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Jemedari John Pombe Magufuli ambaye kwa kutumia mkono wake alikataa kabisa mkono wake usitumike katika kusaini mkataba mbovu huu katika Ikulu ya Tanzania, mjini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema mkataba huu ni mbovu? Niliwahi kuja Bungeni hapa nikiwa na semi-trailer ambalo nilishindwa kuliingiza humu ndani nikaliacha pale nje lilikuwa limesheheni bidhaa mbalimbali vikiwemo vijiti vya kutolea nyama kwenye meno, chaki, vikiwemo vitambaa, zikiwemo peremende.
Mheshimiwa Spika, kama nchi yetu imekuwa na bidhaa ambazo zimezagaa na kusababisha sisi tusiweze kuimarisha na kujenga viwanda vyetu, tukisaini mkataba wa namna hii nchi yetu itakuwa ni dampo la bidhaa nyingi za ajabu na matokeo yake dhamira njema ya Mheshimiwa Rais ya kutaka nchi hii sasa iwe ni nchi ya viwanda hakika hatutaweza kufanikiwa kama tutasaini mkataba wa namna hii.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu ambapo katika aya zake 146 zaidi ya vifungu 20 ni vifungu ambavyo vina matatizo, na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi kwa sababu ya muda sina sababu ya kuvipitia tena. Vifungu hivi vina matatizo, vifungu hivi vinatufanya tukisaini mkataba nchi yetu ya Tanzania haitakuwa na nafasi ya kujitanua katika ku-negotiate tutakuwa tumefungwa. Tukisaini mkataba huu kwenye vifungu ambavyo vinahusu masuala ya kilimo, masuala ya mifugo, masuala ya miundombinu tutakuwa tunasaini mkataba ambao kwa kweli nchi yetu itaingia kwenye matatizo makubwa.
Mheshimiwa Spika masuala haya ya nchi za Ulaya kuwinda nchi zetu katika umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanajua kabisa kwamba nchi ya Kenya ambayo wamepiga hatua kiviwanda, sote tunajua viwanda vya nchi ya Kenya viwanda vingi ndivyo hawa hawa ambao wanatoka kwenye Jumuiya ya Ulaya. Kwa hiyo, leo hii tukisaini mkataba kama huu ambapo tunashirikiana na nchi ya Kenya kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa vyovyote vile tutaingia katika matatizo makubwa.
Mheshimiwa Spika, kuna mifano ambayo iko hai. Sisi tulipoanzisha General Tyre wakati ule tulijua kabisa kwamba tutakuwa na soko zuri na tutaweza kuwa na viwanda ambavyo vitatusaidia, lakini Kenya hawa hawa ambao walitumiwa na nchi za Jumuiya ya Ulaya waliweza kuanzisha Kiwanda cha Fire Stone, leo hii kiwanda chetu cha General Tyre kimekufa. Kwa hiyo, tukisaini mikataba kama hii kwa kweli tutaendelea kuwa na matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Spika niseme, wenzetu wa Kenya ndiyo hata miaka ya nyuma wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuwa ni chanzo cha kuua Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo tuliianzisha wakati ule. Leo nina wasiwasi tukiendelea na Mkataba huu tukiwa tunashirikiana na Wakenya kwa vyovyote vile Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki ambayo tumeianzisha kwa nguvu kubwa, kwa nia njema lazima Jumuiya hii matokeo yake itaenda kuvunjika tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo viongozi wetu wa Serikali, Wizara ya Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara na Uwekezaji, hakikisheni kwamba wataalam wetu waendelee kuuchambua mkataba huu ili maeneo yote yale ambayo yana matatizo yaweze kufanyiwa kazi. Na niseme bayana, lazima katika negotiation nchi yetu itakapofanya uchambuzi waweze kuwa na negotiation framework ambayo imetokana na mawazo ya Wabunge waweze kuboresha mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba mkataba huu kuna maeneo ambayo ni mazuri, lakini kwa sababu maeneo makubwa yana matatizo, hatuwezi tukaingia kwenye risk kwa sababu tu kuna mambo ambayo ni mazuri wakati mambo makubwa ndiyo mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo sisi tuna Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye EALA lazima Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika Mashariki iweze pia kushirikisha Wabunge kwa Chapter ya Tanzania na wenyewe wajaribu kuchambua katika Bunge lao, waende kupiga marufuku muswada kama huu kuendelea kusainiwa ukiwa mbovu namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuna Mabunge mawili, Bunge letu hili kwa leo mimi kama Mbunge wa CCM, Mbunge ambaye naamini Serikali yetu inahitaji mkataba wa kufanya biashara na nchi za Ulaya, lakini hatuwezi kukubali Serikali ya CCM ikaingia mkataba ambao ni mbovu, ambao ni fake kama huu.
Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, bila kujali itikadi zetu, lazima nchi hii tuitendee mema, lazima mkataba huu tuukatae, Mkataba huu ni mbovu, urudi uchambuliwe halafu lazima Bunge hili baadaye lishiriki tena kuangalia ile negotiation framework ili tuone kwamba sasa tunaweza tukaenda kusaini mkataba ambao ni mzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mikataba mingine kama hii, humu humu ndani mimi nimesoma vifungu vingine vinajaribu kuwa na mwelekeo pia wa kutuletea mambo mengine ya ushoga kama ambavyo mikataba mingine inaleta mambo ya ushoga. Kwa hiyo, lazima Wabunge tuwahurumie Watanzania na hasa Watanzania ambao ni wanaume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusipokuwa macho, sehemu zao nyeti zinaweza zikaingiliwa kwa sababu ya mikataba mibovu kama hii. Hatuwezi sisi tukakubali. Lazima tulinde haki za binadamu sisi kama Wabunge wa Bunge hili. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mimi ninakushukuru sana. Nitawashangaa Wabunge wenzangu ambao tumepata semina hapa nzuri ya maprofesa na madokta waliobobea halafu matokeo yake Mbunge unasimama, unakuja kuupongeza na kusema tupitishe mkataba wa namna hii. Nitakushangaa sana, na ndiyo maana hii mbingu mnayoiona hii yuko Mwenyezi Mungu anatutazama, analitazama Bunge hili namna gani mlivyo na huruma na uchungu na wananchi ambao ni watu wa Mungu. Mkisaini mkataba huu nawaambieni itakuwa ni vigumu sana hata ninyi kuuona ufalme wa Mungu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. Siungi mkono kupitisha mkataba huo.