Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Naomba nitoe mchango wangu mfupi hasa kuhusiana na suala zima la hali ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa ya tathmini ya MDG kwa nchi yetu kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, taarifa inaonyesha kwamba uchumi wetu umekua kwa asilimia saba kwa kipindi cha miaka 15. Lakini taarifa hiyo inaonesha kwamba kama uchumi utakuwa mfululizo kwa asilimia saba kwa miaka 15 maana yake inategemewa suala la umaskini utapungua kwa kiwango cha asilimia 50. Lakini taarifa hiyo inaonyesha kwa Tanzania imepungua kwa asilimia kumi tu, kwamba bado tuna safari ndefu ya kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema suala la ukuaji wa uchumi lazima pia tuangalie sekta zingine ambazo zinaweza kuchochea suala zima la ukuaji wa uchumi, bado tuna safari ndefu. Ukiangalia kwenye sekta tu ya kilimo uchumi unakua kwa asilimia mbili tu na tunajua kabisa suala la kilimo ni tegemeo kwa Watanzania wengi, wanategemea ili kuondokana na umaskini.
Lakini sekta hiyo imekua kwa asilimia mbili tu kama ambavyo taarifa hiyo inaonyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la ukuaji wa uchumi Serikali mkija hapa na figures na kujigamba mkisema kwa ujumla wake inakuwa kwa asilimia saba bila shaka mtakuwa mna wahadaa wananchi lakini kwa uhalisia ukienda kwenye sekta moja moja ambazo zinachochea uchumi huo bado tupo nyuma na tuna hali ngumu. kwa hiyo, ni vizuri sana mnaposema suala hili la uchumi muangalie uhalisia wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema pia suala la uchumi tukiangalia hali ilivyo sasa kuna mdororo mkubwa wa uchumi, hakuna mzunguko wa fedha, hakuna fedha katika hata bajeti tuliyopitisha ukiangalia sasa tunaingia kwenye quarter ya pili hata asilimia 26 ya utekelezaji wa bajeti bado hamjafikia na kama mmefikia ni hiyo asilimia 26 tu. Kwenye Serikali za Mitaa hakuna fedha, kwenye taasisi za umma hakuna fedha, Wizarani tumeona taarifa mbalimbali Wizara zikiwasilisha kwenye Kamati hakuna fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya, hakuna fedha, nini kipaumbele? Mna mpango gani wa kufikia hiyo bajeti ambayo tumeipitisha kwa shilingi trilioni 29 katika mwaka huu. Lakini mnafanya projection ya bajeti ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo. Napata mashaka sana kama hii tu ya sasa utekelezaji wake tunaingia kwenye quarter ya pili bado hali ni mbaya halafu unafanya projection ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo tafsiri yake ni kwamba mnajifurahisha ninyi kama Serikali kwa namba hizi kubwa kubwa, lakini mnawaongezea wananchi mzigo wa kuendelea kulipa kodi.
Kwa hiyo, unaona kabisa ni bajeti ambayo kwa kweli mwisho wa siku haitaweza kutekelezeka ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeeleza katika mpango huu kumekuwa na changamoto mbalimbali za kuweza kufikia mipango hiyo. Mojawapo mmesema ushiriki mdogo wa sekta binafsi lakini pia kuna suala la upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji. Hivi hizi sekta binafsi kama hazijatengenezewa mazingira rafiki, kama hizi sekta binafsi hazijawa na imani na Serikali iliyopo madarakani kwa sababu tumeona wakati mwingine mna ndimi mbili mbili sekta binafsi ataogopa ku-invest hela zake kwasababu hajui Serikali kesho inatamka nini? Inafanya nini? Kesho inakuja na kodi gani? Kama msipoweka haya mazingira mazuri hakuna sekta binafsi atakayeweza kuja kuwekeza katika nchi hii kama ambavyo nyie wenyewe mmekiri hapa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado tunahitaji kuwepo na sera na mazingira rafiki ya kuweza kuhakikisha hizi sekta binafsi kwa kweli zinakuwa na wao ni sehemu ya uchumi wa nchi hii. Mmeeleza pia changamoto nyingine ni upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji, hili pia ni changamoto kweli kwa sababu kama sasa hivi mabenki hali ni mbaya, mabenki mengine yameshakua chini ya usimamizi wa BOT, mabenki hayana mzunguko wa fedha, fedha ambazo zilikuwa za Serikali kwenye commercial banks zote zimehamishiwa BOT, obviously hakuna uwekezaji unaweza kufanyika. Kwa hiyo, bado tuna changamoto kubwa sana ambayo kwa kweli itakuwa ni ngumu sana kuweza kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hali ilivyo sasa hivi, lakini wakati mwingine unajiuliza hivi kuna haja gani ya kujadili pia mpango au kujiwekea mpango wakati mpango wenyewe ukienda kwenye utekelezaji hauwezi kufanyiwa tathmini na kuona matokeo. Lakini kuna vitu vingine ambavyo vinaenda kutekelezwa ambayo hayapo kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao tunaumalizia 2016/2017 suala la kuhamia Dodoma halikuwepo lakini Rais amelitamka limetekelezeka, halikuwepo kwenye mpango na kuhama Dodoma sio kazi ndogo, inahitaji fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini angalau sasa hivi mmeiweka kwenye mpango unaokuja; sasa unaona wakati mwingine kama tunaendeshwa kwa matamko ya namna hii ambayo hayapo kwenye mipango maana yake unaenda kuharibu bajeti ambayo imepitishwa hapo. Kwa hiyo, pia wakati mwingine ni lazima haya ambayo mnayatamka ni lazima yaendane na bajeti ambayo tumeipitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Waziri wa Fedha na anisaidie majibu atakapohitimisha. TRA wamesema wanakusanya 1.3 trillion kila mwezi, hiyo ni projection. Mishahara inayolipwa nchi hii ni shilingi bilioni 540, madeni ya ndani ama ya nje inalipwa shilingi bilioni 900, ukifanya hapo mahesabu ni kama one point four trillion na makusanyo ni 1.3 trillion kila mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza hizo ndege zilizonunuliwa kwa fedha cash hii hela mliipata wapi? Wakati mnachokikusanya TRA kila mwezi ni 1.3 trillion, ukilipa madeni, ukilipa mishahara ni 1.4 trillion; fedha za kununua ndege kwa hela cash mmeipata wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri unijibu ama ni hizo fedha zilizopo BOT ambazo zimekusanywa na taasisi zikawekwa kule mkaenda mkazichukua mkanunua ndege cash? Naomba nipate majibu ya suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala lingine ni kuhusu suala zima la elimu. Wakati nimechangia kwenye bajeti ya elimu hapa mnajivunia leo suala la elimu bure, lakini elimu bure hii ni bure tu kwa sababu hawalipi kile ambacho kinatakiwa. Ukienda kwenye uhalisia wa shule zetu hali ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi mmesema mwanzoni wakati wa awamu ya JK mliagiza kujengwe maabara nchi nzima; wananchi wakajichanga, mkaita wadau mbalimbali wakachanga maabara ikajengwa, yamebaki majengo yameachwa. Mmeyaacha yale majengo hayana vifaa, maabara hayafanyi kazi ni majengo tu yaliyosimama mkahamia kwenye madawati mmetangaza madawati nchi nzima watu wametengeneza madawati mengine hayana standard, hayana quality inayotakiwa leo mnataka kukimbilia kujenga madarasa kwa mfumo ule ule wa kulipuka. Kule mmeshasahau maabara, madawati mengine hayana kiwango, leo mnakurupuka mnaenda kujenga…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema muache kukurupuka, mkianzisha jambo moja likamilike, liwe na manufaa, lianze kufanya kazi muende kwenye jambo lingine, ahsante sana.