Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na niwaombee Mwenyezi Mungu vilevile awajalie Wabunge wenzangu wapate afya njema tuweze kulitumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia na mazao mchanganyiko hasa katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani. Watu wa Mikoa ya Kusini walikuwa wanategemea mazao mchanganyiko kama ufuta, korosho, kunde na mbaazi. Katika nchi hii ya Tanzania tuligawanyika katika baadhi ya mazao yanayotokana na maeneo fulani, nasikitika sana tuliwaacha wafanyabiashara wachache wanaiyumbisha nchi kwa kununua mazao kwa bei ya chini na kuwafanya wananchi kuwa maskini. Tujiulize wataendelea wao kujitangaza matajiri mpaka lini, wananchi wa Kusini na Watanzania wanaendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, leo katika soko la Euro wanauza ufuta kilo moja euro tatu na wafanyabiashara hawa wanachukua ufuta Lindi, Mtwara, Pwani wanaupeleka Sri Lanka, ina maana ajira inakwenda Sri Lanka. Tunawaona hatuwaoni? Lakini tumenyamaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshindwa kutafuta soko kwa wananchi kuweza kuwakwamua leo ufuta kutoka 3,500 wananunua ufuta kwa shilingi 600 mpaka shilingi 800 na wengine upo majumbani hawana pa kuupeleka kwa ajili ya hawa wafanyabiashara wanaiyumbisha Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa miaka 50 kwa nini tumeachia uchumi wetu unachezewa na kukanyagwa kanyagwa na watu wachache. Ni hali ambayo imetufanya wananchi wamedhoofika, wananchi wamekuwa maskini kwa kuwa wafanyabiashara wanajiona wanakuwa matajiri na kuwaacha wananchi wanaendelea kuwa wanyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaazi zipo majumbani kutoka shilingi 3,800 mpaka shilingi 800 hazitoki, kunde, njugu na choroko zipo majumbani wao wameukamata uchumi na uchumi huo wameukamata kwa vile wana mahali wanapoegemea, wajiulize kwa nini wanaendelea kuikandamiza nchi ya Tanzania na Watanzania wenyewe wenye ngozi nyeusi wakiwa maskini, tujiulize tunajitambua Watanzania? Hatujitambui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka kila Mtanzania humu ndani ajione kuwa yeye ni part and parcel ya kutetea wanyonge wa Tanzania. Watanzania wanadhalilika, mama lishe anakimbizwa Tanzania nzima kwa ajili ya kuambiwa atoe kodi lakini kuna ma-giant hawalipi kodi. Wanatufanya Watanzania kama sleeping giant ambapo wao hawatozwi kodi na wameamua kulindwa, Serikali kama inataka kusema kweli iwashughulikie hawa watu, haina haja ya kuwasema humu ndani mnawatambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi, Mtwara na Pwani tulikuwa na viwanda vya korosho 13 vyote havifanyi kazi. Lindi peke yake haina ajira ya vijana hata moja kwa vile viwanda vyote vimefungwa. Je, tutawapelekaje vijana wale ambao hawana ajira watafanya kazi gani, wamelima ufuta, wamechukua mikopo benki, lakini leo ule ufuta uko majumbani. Hao vijana tunawapeleka wapi?
Tunataka tuhakikishe uchumi wetu utakwenda wapi, watoto watasomaje katika mfumo ambao unaona kabisa ni kandamizi wao wanatangaza mimi nitakuwa tajiri wa dunia, halafu hawa watu wa chini wanakwenda wapi? Ni kitu cha aibu, inabidi Watanzania tujiulize tutaendelea kuwalinda mpaka lini? Mimi na wewe wote tunataka tuangalie wananchi wanyonge wanapata haki yao, haki sawa kwa wote na asiependa haki aelimishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali imesahau uwekezaji hasa katika mabenki, yameingia mabenki mengi utitiri, riba zinatofautiana lakini anayekandamizwa mwalimu, daktari, mbunge, nesi na watu ambao wanachukuwa mikopo katika mabenki. Wao wanategemea taasisi zetu kuenda kuweka fixed deposit katika mabenki yao, mikataba wanayowekeana ni kutoka asilimia nne mpaka nane lakini leo mabenki wanatutoza riba ya asilimia 18.5 na kuendelea. Je, mwalimu wa kawaida ataweza kudumu au ataweza kumudu uchumi wa namna hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa nini wanaweka riba kubwa jibu halipatikani. Leo kila mwezi wanakukata kodi, unakatwa kodi katika mshahara, unakwenda benki unakatwa kodi na bado unaendelea kuweka riba kubwa mara mia tatu mpaka mara mia nne tunasema nini humu ndani kuhusu watu hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki ni mwiba, leo ndani ya benki tunasikia lakini hakuna anayeguswa kwa vile ndani mle hakuna Lugumi wala hamna UDA. Lakini angekuwepo UDA humu ndani mngesikia kelele Bunge zima humu ndani. Wanatuibia vya kutisha, ukiweka pesa benki ukikaa mwaka mmoja haujaigusa akaunti yako hamna pesa mle ndani ya benki, tunafanya nini na riba chafu kama hizi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata katika Qurani wamesema riba ni haramu, lakini tunaona kabisa riba ni kubwa na zinawakandamiza Watanzania hatuangalii ndio maana wanajiuliza kwa nini sasa hivi wanaanza kupata woga, wanapata woga kwa vile walizoea kufanya wizi wa kukithiri ndani ya mabenki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zetu zimekuwa siyo rafiki kwa Watanzania, anakopa Mtanzania anawekewa riba kubwa ambayo anashindwa hata kuimudu, ndiyo maana leo hata akina mama lishe wakikopa pesa benki ananyang„anywa vitanda vyake, magodoro yake maana yake wao wanaweka vitu vya vidogo vidogo kutokana na uwezo wao.
Naiomba Serikali iiangalie hii riba katika mabenki ni wizi wa aina yake. Na kwa nini sasa hivi wanajaribu kukimbiakimbia kusema wanataka kufunga, huu ni uongo! Watu wa benki wamecheza michezo michafu kwa muda mrefu sasa hivi wanajaribu kusimamiwa ndiyo maana wanasema tunafunga benki, lakini hawafungi benki ni kwa ajili ya wizi waliouona ni mkubwa ambao unawakandamiza Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaingia sasa hivi katika mbunga yetu ya wanyama ya Selous Game Reserve sitaki kuangalia sehemu nyingine yoyote. Nimeizungumzia hii mbuga zaidi ya miaka kumi ndani ya Bunge hili. Selous Game Reserve ni mbunga ya kwanza kwa ukubwa duniani, lakini ndani ya Selous sasa hivi watu wanachimba madini. Tunachimba uranium, wanachimba dhahabu, wanachimba almasi sisi wenyewe tupo hapa humu ndani? Nani atatuletea ufafanuzi kuwa ndani ya Selous kunafanyika nini? Hakuna kinachojulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wameifanya Selous kama shamba la bibi, mapato ya Selous tungeweze kuhakikisha yanawasaidia Watanzania wengi na wanyonge wakafaidika hata na ajira. Lakini ndani ya Selous sasa hivi hakuna kinachoendelea zaidi ya kuchimba madini mengi yako mle ndani, kuhakikisha msitu wote unakwisha, wanyama waliokuwa ndani ya Selous wamekwisha. Je, tunakwenda wapi na uchumi wetu? Tufike mahali tujiulize Tanzania, hivi kweli tunaitakia mema nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wachache ambao wanaingalia Tanzania kwa huruma, watu wengi hawataki kuangalia kwa huruma na ndiyo maana mpaka leo meno ya tembo yanauzwa na tunayaacha hivi tunaangaliana. Kila siku tunaangalia meno yanaondoka, kutakuwa na tembo nchi hii, kutakuwa na utalii nchi hii? Na utalii peke yake unatuingizia 27.5 percent, lakini unaona Selous imetupwa haina ajira haina kazi wala kinachofanyika ndani ya Selous; haiwezekani hali imefikia mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuangalia hali tete inayohusu mazao. Tufike mahali tuwaonee huruma wananchi, wakulima wanalima, mpaka leo mazao yao yamekaa ndani hawajui yatayauza wapi? Leo ufuta kutoka shilingi ngapi wamekaa nao ndani mpaka shilingi 800 hakuna soko la ufuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshindwa kutafuta soko la ufuta, tumefika mahali wananchi tumewakandamiza hata pa kupita hawajui, wamekaa wamechanganikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahali, Serikali iangalie kwa makini mabenki na wakulima wanaokopa katika mabenki wanadhurumika vibaya mno. Mabenki yanaweka riba kubwa na ndiyo maana sasa hivi wanajidai ooh tumefilisika, hawajafilisika hawa, wanabadilisha majina tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana.