Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutufikisha hatua hii siku ya leo. Ni hatua muhimu sana kwa taifa letu na naamini ni kwa rehema zake tu tumeweza kufika hatua hii siku ya leo na naamini kwa pamoja Waheshimiwa Wabunge hatuna budi kusema Alhamdulillah. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mafundisho ya dini yangu baada ya Mwenyezi Mungu huja wazazi wangu. Naomba niwashukuru sana wazazi wangu kwa kunilea vyema na kunifikisha hapa nilipo. Najua kama mtoto wa kike haikuwa rahisi lakini nimeweza kwa sababu walinisaidia, waliniamini na sasa namshukuru Mungu naweza kuwatumikia Watanzania kwa ujumla. Pamoja na wazazi wangu wapo dada zangu, yupo pacha wangu, nawashukuruni sana kwa kuendelea kunipa support. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwashukuru watoto wangu wapendwa, Samira na Abubakar, nasema ahsanteni sana. Naamini bado ni wadogo mnahitaji kuwa na mimi lakini mmeniruhusu na ninaweza kusimama na kuwatumikia Watanzania. Ahsanteni sana na nawapenda sana watoto wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa sasa naomba nimshukuru mume wangu mpenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru kwa kipekee kabisa. Safari ya ndoa yetu ilianza mbali tukiwa wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, tumekwenda pamoja mpaka tunapata PhD yetu, yeye kapata leo na mimi nimepata kesho. Ahsante sana mume wangu. Nakushukuru sana kwa mapenzi yako kwangu, kwa ushauri wako kwangu kama Mchumi, naamini kwa pamoja tutafika salama na nakuahidi mapenzi yangu ya dhati kwako, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa ujasiri wako kama mwanamke, kwa weledi wako katika utendaji wako wa kazi na umetufikisha leo siku hii ya mwisho ya kujadili bajeti ya Serikali yetu. Hongera sana, endelea kusimama imara. Wewe bado mdogo sana, nafasi yako ni kubwa na utafika pakubwa zaidi ya hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu bunifu kabisa, tumeipokea kwa mikono miwili na tutaifanyia kazi. Naamini haitakuwa rahisi kujibu hoja zote hapa mbele lakini naamini tutazijibu zote kwa maandishi. La muhimu zaidi ni kuyafanyia kazi mawazo yenu yote ambayo mmetupatia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu na taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijibu baadhi ya hoja na hoja ya kwanza ambayo ilisisitizwa na Waheshimiwa Wabunge wengi wakiongozwa na Mheshimiwa Andrew Chenge, namheshimu sana Mheshimiwa Andrew Chenge, nayo ilikuwa ni Serikali itumie mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti ya Chenge One ili kuongeza wigo wa mapato na uendelezaji wa sekta ya viwanda. Naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu ni sikivu sana, ilizingatia sehemu kubwa ya mapendekezo ya ripoti ya Chenge One tangu ilipotolewa hadi kufikia hivi leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema baadhi tu ya mambo ambayo Serikali yetu imeshayatekeleza. Jambo la kwanza kabisa lilikuwa ni TRA kuyafanyia kazi kwa wakati taarifa za Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA). Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu kupitia TRA imekuwa ikitumia ripoti za ukaguzi wa hesabu za TMAA kama nyenzo mojawapo muhimu katika mchakato wa ukaguzi na ugunduzi wa maeneo hatarishi. Tunafahamu Waheshimiwa Wabunge na mmeyasema kwa nguvu zote kwamba katika eneo tunalodanganywa sana ni sekta ya madini. Kwa kushirikiana na TMAA, TRA tumeweza kugundua mambo mengi na tunaendelea kuyafanyia kazi na ndipo mnapoona hata makusanyo ya Serikali yetu yakizidi kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ilikuwa ni kuanzisha kodi katika usafirishaji wa fedha kwa njia ya simu za mkononi. Serikali yetu katika hatua hii ilizingatiwa kwenye mapendekezo ya hatua mpya za kodi kwa mwaka 2013/2014. Waheshimiwa Wabunge mliokuwemo kwenye Bunge hili kipindi hicho mliona na katika mwaka huu wa fedha naamini sote tunakumbuka Serikali imewasilisha maboresho ya hatua hii kwa kupendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa asilimia kumi kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge naomba tuelewane. Asilimia kumi hii ni kwa ada zile zinazotozwa na watoa huduma na si kwenye pesa anayoituma Mtanzania kwenda kwa Mtanzania mwingine. Hivyo, naomba tupeleke ujumbe huu kwa wananchi wetu, Serikali ina dhamira nzuri kabisa kwa Watanzania, kuwawezesha kiuchumi waweze kusimama imara, hivyo ada hii haiendi kuwa ni mzigo kwa wananchi bali sasa tunataka na makampuni yale yalipe kodi stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika ripoti ya Chenge One ilikuwa ni kuanzisha ada ya utumiaji wa kadi za simu (sim card). Kama tutakavyokumbuka, hatua hii tuliichukua kipindi kilichopita lakini pamoja na kuichukua na kuiwasilisha hapa Bungeni ilikumbana na vikwazo vingi kutoka kwa wadau na hivyo Serikali kuamua kuchukua hatua ya kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za simu hadi kufikia kiwango cha sasa cha asilimia 17. Naomba tufahamu kwamba unapokua sokoni kwa sisi Wachumi tunafahamu, kunapokuwa na win-lose situation wewe ndiwe utapoteza zaidi hivyo tuliweza kuihamishia kodi hii upande huu na kuthibitisha kwamba ripoti ya Chenge One tunaendelea kuifanyia kazi hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lilikuwa ni kuimarisha usimamizi wa utozaji wa kodi katika makampuni ya simu. Serikali yetu sikivu kama kawaida imelifanyia kazi suala hili ambapo mtambo wa telecommunication traffic monitoring system tayari umefungwa na umeanza kutumika. Hivi sasa Serikali inaendelea kuweka mfumo wa kutambua aina na kiasi halisi cha miamala na thamani ya miamala inayofanywa na makampuni ya simu. Aidha, Mamlaka yetu ya Mapato wataendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ili kukagua hesabu za makampuni ya simu katika kuhakikisha kuwa kodi stahiki zinalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumelifanyia kazi lilikuwa ni pendekezo la kupunguza kiasi cha misamaha ya kodi hatua kwa hatua hadi kufikia asilimia moja ya GDP ambapo tunafahamu misamaha imeendelea kushuka. Kwa historia tu, katika mwaka 2012/2013 misamaha hiyo ilishuka hadi kufikia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa, asilimia 2.3 ya Pato la Taifa katika mwaka 2013/2014 na asilimia 1.9 ya Pato la Taifa katika mwaka 2014/2015. Serikali inaendelea na juhudi hii ya kupunguza misamaha hasa ile isiyokuwa na tija na hivyo ifikie walau asilimia moja ya Pato la Taifa katika muda wa kati na mfupi ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kwamba hadi kufikia Juni 30, 2016 wiki moja ijayo, ni matarajio ya Serikali kwamba misamaha itakuwa chini ya asilimia moja, tutakuwa ndani ya 0.84 ya Pato la Taifa. Hivyo ripoti cha Chenge One Serikali yetu imeendelea kuifanyia kazi vizuri hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hayo yanatosha katika ripoti ya Chenge One lakini yapo mengi ambayo tumekuwa tukiyafanyia kazi na kwa pamoja tutashirikiana. Kama nilivyosema tutawajibu kwa maandishi na mtaona ni hatua zipi nyingine ambazo zimefikiwa katika kuifanyia kazi ripoti hii ya Chenge One kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu na wananchi wetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania wasimamie na kudhibiti mfumuko wa bei na riba za mikopo. Katika suala la kudhibiti riba za mikopo, Serikali yetu pia inafahamu hili ni tatizo kubwa, linawaumiza wananchi wetu. Pamoja na kuliachia suala hili katika soko lakini pia mkono wa Serikali bado uko pale pale na zifuatazo ni sehemu tu ya hatua tunazochukua kama Serikali kuhakikisha kwamba riba inakuwa si ile inayoumiza wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, tunaendelea na usimamizi imara wa sera za fedha na bajeti (monitory policy and fiscal policy), tunaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba riba hizi haziendi kuwa ni mzigo kwa wananchi. Jambo la pili, Serikali imeendelea kuhamasisha benki za biashara kutumia takwimu za Credit Reference Bureau kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa za historia na uaminifu wa wakopaji. Kupitia njia hii ni imani yetu kwamba kama benki hizo za biashara zitaweza kutumia statistics zilizopo katika kitengo hiki itakuwa ni rahisi kufahamu historia ya wateja wao na hivyo haitakuwa jambo jema kuona tena riba ile inapanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kulifikia jambo hili, Serikali pia inaendelea kukamilisha mradi wa vitambulisho vya taifa kwa sababu tunafahamu moja ya kitu kinachosababisha riba iwe kubwa ni pale benki au mkopeshaji hana taarifa sahihi za mtumiaji wa huduma hii. Kwa hiyo, tunaendelea kukamilisha vitambulisho vya taifa, nina imani kubwa sasa kila Mtanzania atajulikana yuko wapi na benki hizi zitakuwa na uhakika wanamkopesha nani na yuko wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili pia Serikali inaendelea kusimamia uandikishwaji wa hati za umilikishwaji wa viwanja kwa Watanzania ili kuwawezesha wananchi kuwa na dhamana wanapohitaji kukopa. Pia Serikali inaendelea kuboresha soko la dhamana za Serikali na soko la jumla la fedha za kigeni ili kuongeza ushindani katika masoko. Pia Serikali yetu inaendelea kuimarisha benki maalum za maendeleo ambazo ni Benki yetu ya Kilimo na Benki ya Maendeleo ya TIB ili ziweze kutoa huduma kwa wahusika na kwa riba ambayo ni sahihi ambayo Watanzania wengi hawataumia. Huo ulikuwa ni mpango wa kudhibiti riba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti mfumuko wa bei, Serikali imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa muda wa kati umebaki kiwango cha wastani wa tarakimu moja. Aidha, kwa mwaka 2015 kiwango kilikuwa wastani wa asilimia 5.6. Pia katika kudhibiti mfumuko huu wa bei Serikali itaendelea kuhakikisha kwanza ujazi wa fedha kwenye uchumi unakuwa sawia na ukuaji wa shughuli za kiuchumi ili upande mmoja usije ukazidi upande mwingine na hatimaye kupelekea madhara yake kwenye mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Serikali itaendelea kutoa chakula kwa bei nafuu kupitia Hifadhi ya Taifa ya Chakula kwenye maeneo yenye upungufu wa chakula kwa sababu tunafahamu sehemu moja kubwa inayopelekea kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni bei ya chakula. Hivyo, tumejipanga vizuri katika suala hili na tuna imani kubwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki katika tarakimu moja. Pia Serikali itaendelea kudhibiti bei za nishati ya mafuta na pia kuvutia na kuhimiza uongezaji wa tija katika kila nyanja za uzalishaji na utoaji huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ilisema utajiri wa madini bado haujawanufaisha wananchi hivyo Serikali inapoteza mapato mengi katika transfer pricing na mis-invoicing. Serikali ijenge uwezo wa watumishi kuongeza mapato kwenye sekta ya madini. Katika suala hili Serikali yetu pia imeendelea kulifanyia kazi kwa umakini kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na sekta hii ya madini. Kama nilivyosema tuna ushirikiano wa karibu kati ya TMAA na TRA na katika hili TRA tumeendelea kuijengea uwezo ambapo TRA ilianzisha Kitengo cha Kodi za Kimataifa (International Taxation Unit) mwisho wa mwaka 2011. Kitengo hiki kimeendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kiutaalam ndani na nje ya nchi yetu. Mafunzo haya yalidhaminiwa na Serikali ya Norway kupitia Norwegian Tax Agency ambapo walitoa fedha ya mafunzo na Serikali ya Marekani kupitia US Treasury ambao wanaendelea kuleta mtaalam wa transfer pricing. Tunawashukuru watu wa Norway pamoja na Serikali ya Marekani kwa kuendelea kutujengea uwezo katika hatua hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika kuimarisha uwezo wa kiutaalam kwenye kitengo hiki TRA imenunua haki ya kutumia (transfer pricing data base) itakayowezesha kupata taarifa mbalimbali za kulinganisha, that is comparable data kwa ajili ya upatikanaji wa taarifa na kurahisisha ukokotoaji wa kodi. Vilevile TRA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha imetengeneza kanuni za transfer pricing pamoja na transfer pricing guidelines kwa ajili ya kutoa mwongozo wa jinsi ya kukokotoa kodi. Hivyo, tuna imani kubwa kabisa kupitia vitengo hivi na jitihada hizi tatizo hili litaondoka na Watanzania wataweza kunufaika na sekta hii ya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wataalam wetu kupata utaalam huu kwa sasa wataalam wa kitengo hiki wanaendelea na ukaguzi katika makampuni matatu ya madini katika eneo hili la transfer pricing. Kazi hii inatajaria kukamilika katika robo ya kwanza ya 2016/2017 na tutaona wazi mbivu na mbichi ni zipi na Watanzania haki yao iko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia TRA imeshajiunga na Shirika la Kimataifa la OECD Global Forum pamoja na Africa Tax Administration Forum na inaendelea na mchakato wa kusaini makubaliano ya kubadilishana habari za kodi. Hii inaturahisishia kujua ni kiasi gani kimetoka Tanzania bila sisi kujua katika black market na tuweze kuelewa nini cha kufanya na jinsi gani ya kupata kodi yetu stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kuhakikisha kuwa maeneo yanayohitaji weledi maalum yanapata wataalam wa aina hii ya kuyasimamia TRA pia hubadilishana uwezo na mamlaka nyingine za mapato na mamlaka za udhibiti nchini zinazohusika na usimamizi wa mapato na taasisi na idara nyingine za Serikali kama vile TCRA, TMAA, Contractors Registrations Board, TANROADS na kadhalika. Hali kadhalika, Serikali inaendelea na jitihada za kukiimarisha kitengo hili ili kuwa na wataalam wengi zaidi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kikodi zinazoendelea kuibuka katika eneo hili la kodi za kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ilikuwa Serikali itatumia utaratibu gani kuhakikisha kuwa majukumu ya taasisi zilizokuwa zikijiendesha kwa fedha za retention hayaathiriki. Napenda kulithibitia Bunge lako Tukufu kwamba nia ya Serikali ni njema katika eneo hili, imedhamiria kuhakikisha sasa mapato yote ya Serikali yanatumika kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu. Napenda kulihakikishia Bunge lako kwamba taasisi zote zilizokuwa kwenye utaratibu wa retention zitatakiwa sasa kuwasilisha mahitaji ya bajeti kila mwaka kulingana na kalenda ya uandaaji wa bajeti. Serikali itachambua mahitaji ya taasisi husika na kisha kupangiwa ukomo wa Bajeti. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango itahakikisha kwamba bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya taasisi hizi na migao ya fedha kutoka Mfuko Mkuu inatolewa bila kuchelewa ili tusikwamishe utendaji kazi wa taasisi zetu hizi. Tunafahamu umuhimu wa majukumu yao na hivyo, hatutachelewesha fedha kuzipelekea taasisi zetu hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hii italeta usawa katika matumizi ya taasisi zetu na kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwa taasisi zote za taifa letu. Nia ya Serikali yetu ni njema kama nilivyosema mwanzo, naomba Waheshimiwa Wabunge muendelee kutuunga mkono. Hii ni tiba sahihi sana ya lile ambalo tulilisikia huko nyuma kwamba zipo taasisi zilizokwenda kufanyiwa mikutano yao ya bodi nje ya nchi, hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama mchumi ukiwa na pesa ambayo unaiona ni nyingi huna matumizi unaweza kutumia vyovyote vile lakini kwa mfumo huu ni imani yangu sasa tutarejesha nidhamu ya matumizi ya pesa za Serikali na pesa hizi ziweze kuleta tija kwa wananchi wetu hasa wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali ilete Muswada wa Sheria ambapo itaanzisha mamlaka ya kusimamia na kudhibiti taasisi ndogo za fedha nchini. Serikali inakamilisha Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha. Sera hiyo itawezeshwa kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogondogo za Fedha (The Microfinance Act). Sheria hii itaanzisha Mamlaka za Kusimamia na Kudhibiti Taasisi hizo kwa kutumia madaraja kama, moja, tutakuwa na udhibiti wa taasisi ndogo za fedha zinazopokea amana kwa wananchi (deposit taking microfinance institutions) utakaosimamiwa moja kwa moja na Benki Kuu ya Tanzania. Mbili, tutakuwa na udhibiti wa taasisi za huduma ndogo za fedha zisizopokea amana kutoka kwa wananchi (non deposit taking microfinance institutions). Pamoja na programu na mifuko maalum ya Serikali ya kuwezesha wananchi kiuchumi itakuwa chini ya taasisi hizi na chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutakuwepo na udhibiti wa huduma za fedha zinazotolewa na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Mwisho, udhibiti wa huduma za fedha zinazotolewa na vikundi kama vile Village Community Banks (VICOBA), Voluntary Savings Loans Association, Rotating Savings and Credit Association na watu binafsi wanaotoa mikopo na kuweka akiba yaani money lenders and saving collectors chini ya mamlaka ya Serikali za Mitaa. Sheria hii pia itaainisha vigezo na masharti ya ukuaji wa taasisi hizo kutoka daraja moja kwenda daraja lingine ili kuwa na udhibiti imara na ukuaji endelevu wa sekta hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichowaahidi Waheshimiwa Wabunge wakati tunawasilisha bajeti ya Wizara ya Fedha tutamiza ahadi hii ili wananchi wetu waondokane na adha ya usumbufu wa mfumo usio rasmi katika sekta ya fedha. Tunafahamu waathirika wakubwa ni akina mama katika hili na ni imani yangu kubwa tutalisimamia kwa uhakika kabisa ili akina mama waondokane na adha hii ya kukopeshwa bila kuwa mtu yeyote anayeratibu taratibu hizi ili akina mama hawa waondokane na lindi la umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuitolea ufafanuzi ni kwa nini Serikali hailipi madeni inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii takribani shilingi trilioni 8.942? Waheshimiwa Wabunge kama mnakumbuka nimekuwa nikilisemea jambo hili kwa nguvu zangu zote na tumeji-commit kama Serikali. Naomba tufahamu kwamba katika mapitio ya awali yaliyofanyika, yalionesha kwamba madai ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yalifikia jumla ya shilingi trilioni 3.89 hadi Juni, 2015. Madai haya yanajumuisha deni la PSPF la kabla ya mwaka 1999 la shilingi trilioni 2.67 na shilingi trilioni 1.22 kwa ajili ya madai ya mifuko yote yaliyotokana na uwekezaji katika miradi mbalimbali ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia ya dhati ya kulipa madeni haya yote ili kuimarisha Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii mara tu baada ya kukamilisha uhakiki wa madai hayo. Tunafahamu tumekuwa na tatizo la wafanyakazi hewa na tumemsikia Mheshimiwa Rais wetu amesema, unapokuwa na wafanyakazi hewa utakuwa na wastaafu hewa pia. Hivyo, tunaendelea kuhakiki hatua kwa hatua tutafika mwisho mzuri na mifuko yetu ya hifadhi ya jamii itaweza kufanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mmojawapo katika hili hadi kufikia Mei, 2016 uhakiki wa madai ya mfuko wa PSPF ulikuwa umekamilika ambapo kiasi kilichokubalika ni shilingi trilioni 2.04 kutoka madai ya awali ya shilingi trilioni 2.67, kuonyesha kwamba kulikuwa na madai hewa katika wastaafu hawa. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuipatie Serikali yetu muda tukamilishe uhakiki huo ambao umeanza kufanywa na Mkuguzi wetu wa Ndani wa Serikali ili tuweze kuondokana na madeni tata na tuweze kulipa kile tunachostahili kukilipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuhitimisha majibu ya hoja zangu kwa maneno yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika na Bunge lako Tukufu, naomba tufahamu kwamba uchumi wa Tanzania ya viwanda kama alivyosema shemeji yangu Mwijage haupo mikononi mwa vijana wanywa viroba na watafuna mirungi bali mikononi mwa vijana walio tayari kabisa kuingia kwenye uchumi wa kati kiakili na kimwili. Very aggressive to take and tape opportunities that are ahead of us in our country. Kama Wabunge na wawakilishi wa wananchi tuna jukumu la kurejea majimboni mwetu na kuwaandaa vijana wetu wa Tanzania kwa Tanzania ya viwanda iliyo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maisha ya vijana wetu hayapo kwenye bangi na pool table, hapana, bali yapo mikononi mwa mama yao Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli na Serikali yake ambayo imelenga kwenye ubunifu utakaoleta fursa za kiuchumi kwa vijana wetu. Yapo mikononi mwa Serikali makini ambapo ipo tayari kutengeneza ajira kwa ajili ya watu wake. Serikali yetu ipo tayari kwa hayo yote, naomba tuwaandae Watanzania kuingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mratibu na msimamizi wa sera za uchumi mpana (micro-economic policies), Wizara ya Fedha na Mipango tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunakuwa na ufanisi katika soko la fedha (Money market), soko la ajira (labor market) na soko la bidhaa (commodity market).
Masoko haya yote matatu yanategemeana, yanatafsiri pia juhudi zetu za kuelekea uchumi wa kati na yanaathiri au yanaathari za moja kwa moja katika maisha ya Watanzania wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utayari wetu Waheshimiwa Wabunge wa kulipa kodi kwa hiari ni njia pekee ya kutufikisha katika maendeleo endelevu na uchumi wa kati. Hivyo, ni lazima tuangalie kwa umakini rasilimali zetu tulizonazo ndani ya nchi yetu na kuzitumia kwa ufanisi katika kuleta maendeleo ya uchumi jumla (inclusive growth). Hii ni pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo vyetu vya mapato ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa ujasiri, uvumilivu na umakini wake katika utendaji wa kazi zake. Naomba nikuambie Mheshimiwa Waziri, mti wenye matunda ndiyo hupigwa mawe, usikate tamaa endelea kwenda mbele. Najifunza mengi kutoka kwako, endelea kunilea na kunijenga, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.