Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na mimi napenda nikuunge mkono kwa kazi yako unayoifanya ya kusimamia sheria na kanuni zetu za Bunge. Endelea kusimamia sheria na kanuni za Bunge ili kulinda heshima ya Bunge letu. (Makofi)
Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Fedha, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara hii kwa juhudi zao za kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua za maendeleo. Naomba niwatie moyo, endeleeni na kazi, sisi tuko nyuma yenu kuwasaidia pale ambapo panahitajika kutoa msaada wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kutoa mchango wangu kwenye Tume ya Pamoja ya Fedha. Napenda tu kutoa msisitizo kwamba Tume hii ifanye kazi zake na kama kuna upungufu urekebishwe na kama kuna upungufu wa watendaji basi nafasi hizo zijazwe ili Tume hii ifanye kazi yake vizuri na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu mashirika ya Serikali kama NIC na TTCL. Haya ni mashirika yetu ya Serikali lakini hali yake siyo nzuri kiutendaji na katika ukusanyaji wake wa mapato au kupata mapato. Ni vyema sasa taasisi za Serikali ikayatumia mashirika yetu ya Serikali ili kuongeza mtaji na fedha zaidi katika mashirika hayo. Mfano TTCL, taasisi zote za Serikali zikitumia mitandao hii ya TTCL nafikiri tutaweza kuwaongezea mtaji wa kuendesha shughuli zao na litaanza kunyanyuka pamoja na mashirika mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi ambazo zinafanana katika shughuli zake za utendaji mfano TRL na RAHCO, TBS na Weights and Measures Agency. Hebu Serikali sasa iangalie taasisi za namna kama hiyo ambazo kazi zake zinafanana au zinakaribiana iziunganishe ili zifanye kazi kwa pamoja na kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu ukusanyaji wa mapato katika bandari bubu. Ni kweli kabisa fedha nyingi zinapotea katika bandari bubu. Kwanza ni kuziorodhesha bandari zote bubu za Tanzania na baadaye kujua ni mbinu gani ambazo wanatumia katika kupitisha bidhaa. Kwa kufanya hivyo tutaweza kudhibiti upotevu wa mapato na bidhaa za magendo. Kwa kupitia bandari bubu si ukwepaji tu wa kodi uliopo huko bali pia zinatumia kupitisha bidhaa ambazo haziruhusiwi mfano nyara za Serikali zinapitishwa na zinakwenda katika maeneo mengine na zinasafirishwa. Mfano, zinaweza zikapitishwa bandari bubu za Tanga na Zanzibar na kusafirishwa huko zinakokwenda kama China na kwingineko. Kwa hivyo, ulinzi na ukaguzi madhubuti ufanyike katika bandari bubu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi natilia mkazo Sheria ya Manunuzi kama wenzangu walivyoiongelea, iletwe hapa ili ifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitilie mkazo kuongezewa mtaji Benki ya Kilimo kwa sababu benki hii kutokana na mpango kazi wake imejipanga kwenda katika mikoa yote ya Tanzania. Tatizo lao ni mtaji wa kufika na kufungua ofisi katika mikoa yote ya Tanzania. Kama itaongezewa mtaji itaweza kuwafikia wananchi wote huku waliko ili kuwasaidia wananchi katika miradi midogo midogo ya kilimo, uvuvi, ufugaji na mingineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tutilie nguvu ukwepaji wa kodi, najua hili mnalifanyia kazi. Nataka kuuliza, kulikuwa na uwakala wa ukusanyaji wa VAT kati ya Tanzania Bara na Visiwani kila mmoja ni wakala wa mwenzake. Sasa sijui mpango huu mpaka sasa unaendelea au umesimama? Pia naomba tudhibiti mfumko wa bei, kila kukicha mfumko wa bei unakuwa mkubwa na unakuwa mzigo mkubwa kwa wananchi katika kununua bidhaa za kujikimu kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mifuko hii ni vema ikaangalia masharti ya wanachama wake ili kupunguza baadhi ya masharti ili isiwe mzigo kwa wananchama wa mifuko hii. Mfano umri wa kulipwa pensheni wakati wa kustaafu inamlazimisha mwanachama lazima afikishe miaka ile waliyoitaka wao na pengine kungekuwa na nafasi ya kustaafu mapema akalipwa haki zake angeweza kustaafu na nafasi zile zikajazwa na vijana wengine ambao wanataka kuajiriwa. Kwa kipengele hicho kinafanya mtu abakie tu kusubiri kulipwa pensheni kwa sababu kama hukufikisha umri huo huwezi kulipwa pensheni yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize kuhusu ukusanyaji wa mapato kwa jumla. Naomba wafanyabiashara wahamasishwe zaidi kutumia hizi mashine za kieletroniki na mashine hizi zisiwe kwa baadhi tu ya watu, ziwe kwa wafanyabiashara wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja, nawatakia kheri katika ufanisi.