Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kusimama ndani ya Bunge lako na naanza kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na jambo la msingi lililozungumzwa na Waheshimiwa wachache waliopita juu ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011. Najielekeza kwenye Sheria ya Manunuzi ya Umma kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais kupitia hotuba yake ndani ya Bunge hili lakini kutokana pia na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo asilimia 40 inatarajiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunatambua wakati ule ilipokuwa chini ya asilimia 40, kwenye asilimia 22 na kuendelea tuliona changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, udhaifu wa taasisi mbalimbali katika usimamizi wa matumizi ya pesa za maendeleo na za kawaida. Leo tulipopokea taarifa ya miscellaneous amendment zinazotarajiwa kuwasilishwa Bungeni kutoonekana kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma imetufanya baadhi ya Wabunge tupate mashaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mashaka hayo nikaenda kuchukua taarifa ya PPRA ya mwaka 2014/2015; nikajaribu kupitia kwa kina upungufu uliobainishwa na taarifa hiyo. Pamoja na kwamba taarifa inaonesha masuala ya manunuzi ya umma katika taasisi mbalimbali za kiserikali level of compliance iko juu lakini ukaguzi wa mashirika haya, kwa mfano mwaka 2014/2015 wamekagua jumla ya taasisi za manunuzi 80 kati ya hizo 39 ni za Halmashauri, lakini tunazo Halmashauri 168. Kufanya maamuzi ya kuchelea kuleta marekebisho ya sheria kwa ripoti kwamba labda mambo siyo mabaya si sahihi kwa sababu hata ukaguzi unafanyika kwa taasisi chache.
Kwa hiyo, niombe Serikali iwasilishe Muswada huo tufanye marekebisho kwenye baadhi ya vipengele ili asilimia 40 ya fedha za maendeleo zilete tija na value for money na matumizi hayo yaonekane ili Watanzania wenzetu waweze kufaidika katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naungana na Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa mimi ni Mbunge wa Viti Maalum na kundi kubwa naloliwakilisha hapa ni wanawake na vijana; na wanawake na Watanzania wengi walikipigia kura chetu kwa matumaini ya ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Tunaamini ahadi hii ikitekeleza itakuwa chachu katika uibuaji wa miradi mbalimbali na pia itakuwa chachu ya mzunguko wa fedha katika maeneo yaliyokusudiwa. Naungana na maoni ya Kamati yangu, Serikali pamoja na changamoto iliyopo, lakini dhima ya kuinua uchumi wa watu wachache au kupitia vikundi vya SACCOS ni muhimu kwa sababu mwisho wa siku watalipa kodi kutokana na shughuli watakazozifanya na itaongeza mapato ya Serikali, huu ni mzungunguko tu.
Kwa hiyo, niombe Serikali iongeze kwani asilimia sita haitoshi na wengine tumeshafanya ziara katika maeneo mbalimbali, wanawake wa Kibaha, Mafia, Mkuranga, Rufiji, Bagamoyo na Kisarawe pamoja na vijana na makundi mengine mbalimbali yanayohusiana na masuala haya ya asilimia 20 wako tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijielekeze kwenye suala zima la utekelezaji wa bajeti ya mifuko kwa 2015/2016. Tunaweza tukawa na bajeti nzuri, tunaweza tukatenga pesa nzuri kwa maendeleo na matumizi mengineyo lakini kama mifuko hii kwa mfano Mfuko wa NAOT mpaka mpaka Machi, 2016 una asilimia 45 tu. Ofisi hii Kikatiba imepewa dhima ya kukagua matumizi na mapato ya fedha za Serikali. Kwa dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kupambana na ufisadi, kupambana na ubadhirifu, kupambana na maovu mbalimbali na tumeona kasi yake, mchango mkubwa atasaidiwa na Ofisi ya Ukaguzi wa Serikali (National Audit Office). Kwanza niiombe Wizara ijitahidi kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha iweze kuwawasilishia fedha ambazo hawajasilisha mpaka sasa, asilimia 45 mpaka Machi ni kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna Mifuko ya Mahakama pia asilimia 61, Mfuko wa Bunge asilimia 49 pamoja na interest. Nataka kusema dhima ya mifuko hii ina nafasi kuchangia katika ukuzaji wa uchumi. Kwa hiyo, napenda kusisitiza Serikali ilione hili kwa sababu kama Mfuko wa Ukaguzi utakuwa haufanyi kazi iliyokusudiwa hata uwepo wa Bunge hili katika kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali ambapo msaidizi wetu mkubwa ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inawezekana tukapata tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nizungumzie Wizara zingine, kwa mfano mpaka mwezi Machi Wizara ya Kilimo ilikuwa haijapelekewa fedha ya maendeleo. Kama kweli tunataka kuongeza mapato ambapo tunategemea kilimo ndicho kitachangia katika mchango wa Taifa, Wizara hii mpaka Machi kuwa haijapelekewa fedha za ndani ni tatizo. Pia tunayo Wizara ya Afya asilimia 11 tu, hata Wizara yenyewe ya Fedha naomba niisemee pia asilimia sifuri. Wizara hii ina mchango mkubwa katika kusimamia uchumi wa Taifa letu kama ambavyo Wajumbe wengine wamesema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye masuala ya mishahara hewa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ametoa maelekezo na kwa namna ambavyo kazi imefanyika vizuri na kwa namna ambavyo Serikali imeweza kubaini zaidi ya watumishi hewa 10,000. Hata hivyo, inawezekana kabisa tatizo kubwa ni mfumo. Kwa hiyo, naungana na maoni ya Kamati kwamba Serikali izidi kuangalia mifumo yake hasa LAWSON ambao unatumika katika mishahara, lakini pia EPICA, kuweza kuiunganisha kati ya EPICA9 na LAWSON na isisitize matumizi ya Mkongo wa Taifa. Nadhani kupitia Mkongo wa Taifa masuala ya TEHAMA itaweza kuziunganisha Halmashauri na Serikali Kuu katika mawasiliano ya namna ya kudhibiti watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tungependa kuona hatua za haraka zimechukuliwa kwa watu waliosababisha kuwa na watumishi hewa. Maana kama tumeshapata idadi ya watumishi hewa 10,000, kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa mwaka kilikuwa kinatumika, tunatakiwa tuwajue kinagaubaga na waliohusika wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa niiopongeze Wizara ya Fedha, niendelee kuwaomba…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.