Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu mdogo. Kwanza nimshukuru Mungu tena kwa kunipa nafasi hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nichangie kama Wabunge wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri kwa speech lakini pia nampongeza kwa kazi ngumu aliyonayo mbele yake. Tunajua yeye ni mtaalam ataweza kutusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie mambo mawili tu, na kama nitakuwa na la tatu basi nitachangia. La kwanza, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 31 kifungu 3.4.10 anasema katika mwaka wa 2015/2016 Wizara imepitia Sheria ya Manunuzi ya Umma namba saba ya mwaka 2011 na kupendekeza marekebisho ya Sheria hiyo. Napenda niseme kati ya vichaka au sehemu ambazo zinatumika kumaliza fedha ya Taifa hili ni Sheria ya Manunuzi. Bei za tender za Serikali huwa ni za ajabu kweli, ni kwa sababu ya sheria hii. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kwa kweli sheria hii iletwe kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma sheria ambazo mmetupa tuangalie za marekebisho miscellaneous, hii sheria siioni, mtaileta nini? Maana yake ndiko huko fedha zinakopotelea. Tunaomba kama mnaweza kuileta hata kwa hati ya dharura tutashukuru kwa sababu matumizi ya Serikali yanatumika vibaya kulingana na sheria hii ya mwaka 2011. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka kusema ni juu ya kazi ya BOT (Benki Kuu ya Tanzania) na hili jambo niliwahi kusema na narudia tena, labda baadaye litaeleweka. Ni vizuri kusema sema hata kama ni jambo la uongo linaweza kuwa la kweli. Sisi tunachimba dhahabu katika nchi yetu, tuna migodi minne sasa inayotoa dhahabu. Kazi ya BOT ni kutunza fedha za kigeni lakini kutunza dhahabu safi na dhahabu ina represent utajiri wa nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati tulijaribu kununua dhahabu tukapata hasara kwa sababu tulinunua dhahabu, tulivyoipeleka kwenye smelting ikaonekana ni makapi lakini sasa tuna nafasi nzuri ya kupata dhahabu safi kwa kuwaambia makampuni watulipe nusu ya mrabaha katika dhahabu safi, hatuna tatizo. Hivi tunashindwa nini kuchukua dhahabu safi tukalipwa, tukaitunza ili baadae watoto wetu tutakapokufa tunawaambia bwana dhahabu hiyo mnaona mashimo hayo, ipo pale tani 200, 300 zimekaa. Uzuri wa kuwa na dhahabu kwenye reserve yetu tunaweza kurekebisaha hata thamani ya shilingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, thamani ya shilingi ikiteremka tuna-release kidogo inakuwa nzuri. Kwa hiyo, tuna wajibu sasa hivi kutunza dhahabu. Najua niliuliza swali mwaka jana, Serikali ikapiga chenga lakini nasema hatuna sababu ya kutokutunza dhahabu kwenye benki yetu. Nchi zingine kama Marekani wana tani 8,000 kwenye reserve yao. Ujerumani wana tani zaidi ya tani 3,000 hata Libya nchi inayopigana ina dhahabu 116 tani. Na nchi nyingi ambazo unaziona ni tajiri zote zina dhahabu kwenye reserve yao. Kwa nini tusifanye hivyo, kwa vile na sisi tunachimba dhahabu. Nchi za Afrika, iko South Africa, ina tani zaidi ya 100 kwenye reserve yao, sisi tuna shida gani? Sisi zero! Kwanini? Kwa hiyo naomba sana Serikali mtafakari jambo hili. Tafuteni wataalam waangalie namna tunavyoweza kufanya jambo hili tukapata dhahabu. (Makofi)
Jambo la tatu, ni matumizi holela ya dola katika nchi yetu. Dola inatumika mahali popote. Ukienda leo mahali popote hata Karikaoo unaweza ukatoa dola ukanunua, hata salon umekwenda kutengeneza nywele ukanunua kwa dola. Dola zetu zinapotea. Haziingii kwenye mfumo halali wa nchi, kwa hiyo dola zinaibiwa, zinapotezwa, zinabebwa kwa sababu tumeruhusu hili jambo. Ukienda South Africa ninyi mashahidi, huwezi kulipa hata hoteli ya kitalii kama huna dola, lazima ukatafute hela yaki-South Africa. Nenda nchi za Ulaya, hivyo hivyo, nenda Thailand, kila mahali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna ruhusu kila mahali dola inatumika, tunapoteza fedha. Serikali tunaomba tena, nilishawahi kuuliza swali mkapiga piga chenga, mimi naomba jamani uchumi wetu unaharibika kwa sababu tuna mifumo ambayo haisimamimii fedha zetu vizuri. Hili ni jambo sio zuri sana. Tunaomba Serikali msimamie jambo hili tungeni sheria. Tungeni sharia tuko tayari sisi Wabunge tutunge sheria ili fedha za kigeni ziweze kubaki kwenye reserve ya Taifa letu vinginevyo tuna kazi kubwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Ubelgiji huwezi ukatumia hela ya nje lazima uibadilishe iwe Euro sasa sisi tuna shida gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne na la mwisho, naomba nisipigiwe kengele, leo niko very smart. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuelimishwa kidogo, la kwanza ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya shilingi milioni 50. Amesema mama yangu pale, kwenye bajeti huko kote nimeangalia sioni, hivi tumeiwekea bajeti wapi?
Inawezekana nimeisoma vibaya, kwenye vitabu vyote nimeangalia hakuna mahali ambapo tumeweka fedha kwa ajili ya kutekeleza ile ahadi ya Rais, basi nielimisheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni MCC. MCC tuliiachia ikaondoka hatuna mradi wa MCC tena, labda kama kuna mazungumzo mapya. Hata hivyo, bado kuna subvote 1007 inasema imeweka hela shilingi milioni 500 kwa ajili ya MCC, ni kitu gani hicho?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.