Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye anaendelea kunijaalia afya njema ili na mimi niweze kuendelea kutoa michango yangu katika Bunge lako Tukufu hasa katika Wizara hii ya Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Wizara ya Fedha kwa sababu imekuja na mpango ambao wananchi sasa wanaanza kuwa na imani kwamba kama mpango huu utatekelezwa basi wananchi wote wataenda kufaidika na nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika michango yangu. Kwanza kabisa naomba kuchangia suala zima la Deni la Taifa. Ukiangalia Deni la Taifa, faida zake kubwa sana ni katika kusaidia kuchangia katika maendeleo ya Taifa hususan katika kuendeleza miundombinu kama vile barabara, viwanja vya ndege, reli na hata kwenye afya pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kusikitisha sana ni kwamba Deni la Taifa limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, ninazo data kidogo hapa; mwaka 2005 hadi mwaka 2010 Deni la Taifa lilikuwa yapata trilioni 10; mwaka 2010 hadi mwaka 2012 Deni la Taifa liliongezeka hadi kufikia trilioni 14, lakini mwaka 2015 hadi sasa Deni la Taifa sasa limefikia trilioni 41; hii inasikitisha sana. Kwa sababu gani nasema inasikitisha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa linaongezeka lakini wananchi bado hali inazidi kuwa ni ngumu. Swali langu sasa kwa Waziri, na naomba Waziri atakapokuja anisaidie walau kunipa majibu lakini si mimi peke yangu wala Bunge lako hili Tukufu bali hata wananchi wote wanaonisikiliza sasa hivi, kwamba; ni kwa sababu gani deni hili lime-shoot kutoka trilioni 14 mwaka 2012 hadi kufikia trilioni 41 kwa mwaka 2015. Ninaomba Waziri atakapokuja basi aje na ufafanuzi utakaoweza kuwasaidia wananchi wa Tanzania kuelewa ni kwa nini deni hili linazidi kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia na Wabunge wenzangu deni hili linapokuwa linazidi kuongezeka ni kwamba kila Mtanzania katika nchi yetu anazidi kuwa na ongezeko la kulipa deni hili. Kwa mahesabu, bahati mbaya hesabu nilipata “F” kwa hiyo, sijui namna ya kupiga deni hili kwa kila Mtanzania lakini mtanisaidia pamoja na Waziri, kwamba hivi deni hili ni lini basi litaweza kuwafaidisha wananchi wa Tanzania. Deni linaongezeka, barabara bado ni mbovu, kila Mbunge akisimama hapa wakati wa kipindi cha maswali na majibu hata wakati wa maswali ya nyongeza utasikia kila mtu analalamika kuhusiana na suala zima la barabara lakini hata hivyo, masuala ya maji, kila Mbunge anasimama hapa akiwakilisha wananchi wake kwa kulalamikia suala la maji. Hivi kwa nini Deni la Taifa linazidi kuongezeka? Ninaomba na ninamtaka Waziri atakapokuja anieleze tu ni kwa nini Deni la Tafa linazidi kuongezeka na wakati wananchi bado wana maisha ya chini au la sivyo naomba nitoe taarifa kabisa kwamba nitashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri itakapofika muda wake, kama hatakuja na majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Nampongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu amesaidia. Tunaona kabisa ongezeko la mapato hapa nchini sasa limeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto ambazo zipo. Kwa mfano, baada ya kuongezeka kwa mapato haya, Halmashauri zetu hazifaidiki na ongezeko la Pato la Taifa. Nasema hivyo kwa sababu kwenye Halmashauri zetu kuna kero mbalimbali ambazo zimefutwa ambazo zimekuwa zikiwakera wananchi, na hata Mheshimiwa Rais nae pia amekuwa akiziongelea kero hizi. Baada ya kero hizi kufutwa hakuna mbadala wa mapato ambao umekuwepo katika Halmashauri zetu na ndiyo maana unakuta kwamba hata Halmashauri inapotenga fedha kwa ajili ya kuondoa changamoto za barabara, maji hata afya, hawawezi kufikia malengo yao kwa sababu ongezeko la pato katika Halmashauri zetu – mapato yanapokuwa yanakusanywa malengo ya Halmashauri yanakuwa ni makubwa kiasi cha kwamba Halmashauri zinashindwa hata ku-prioritize kwamba tuanze na lipi na tumalizie na lipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi ninaishauri Serikali walau katika Wizara hii kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara ambayo inakusanya mapato ya Taifa kwa ukubwa kabisa. Wizara hii naweza nikaisema kama ni Wizara nono, Wizara ambayo imeshiba, basi tunaomba kwamba Wizara ya Fedha iweze kupeleka fedha ziwafikie wananchi hasa katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mdogo tu; katika Halmashuri zetu tuna mpango mzuri sana ambao tumeuweka wakuzitenga asilimia10 ambayo asilimia tano inatakiwa kwenda kwa wanawake na asilimia tano iende kwa vijana. Lakini ukiangalia Halmashauri nyingi kwa tathmini ya haraka haraka zimekuwa hazitengi fedha hizi na si kwa sababu wanafanya makusudi kutokutenga fedha hizi iliziweze kuwafikia wananchi, lakini ni kwa sababu ya kulemewa na mzigo wa mipango ambayo wanakuwa nayo kiasi cha kwamba ile fedha hata kama inakuwa imetengwa matokeo yake inakuja kufanya dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; nikiongelea katika Jimbo la Ilemela ambalo ni Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi Mama Angelina Mabula, kule tumekuwa na mipango mizuri sana, kila mwaka wamekuwa wakitenga fedha hizi lakini inapofika wakati kwamba sasa fedha hizi ziweze kugawiwa kwa wananchi hasa wanawake na vijana unakuta fedha hizi zinatumika katika kutengeneza barabara. Ukiangalia katika Wilaya ya Ilemela, ni Wilaya ambayo bado Halmashauri yetu ni changa. Ninaitaka na ninaiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa sana kwamba iweze kuangalia Halmashauri zetu ili basi waweze kuongezewa fedha walau ziweze kuwasaidia wanawake hususan akina mama kama vile mama lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mzunguko wa fedha umekuwa ukionekana kama unaishia huku juu tu, yaani unaishia kwenye sehemu za juu, yaani wananchi wa hali ya juu ndiyo ambao wanafaidika na pesa. Sasa unapoongelea Pato la Taifa limeongezeka wakati mwananchi wa chini bado fedha haijamfikia ni masikitiko makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninamuomba Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake anisaidie tu kuja na mikakati kwamba Serikali imejiwekea mikakati gani ya kuziba mianya ya fedha ambazo imekuwa ikipoteza, kwa sababu inawezekana tukakusanya pesa nyingi lakini wako watu ambao kazi yao wamekaa kuchungulia hizi pesa na kuweza kujinufaisha wao wenyewe matokeo yake wananchi hawafaidiki na fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niongelee suala la shilingi milioni 50 kila kijiji. Tulipokuwa tukizunguka katika kampeni zetu za mwaka huu. Kila mwananchi anakuuliza kuhusiana na suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Swali kwa Waziri ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kila mwananchi ananufaika na pesa. Ukiangalia kwa mfano katika ukurasa wa 24 Maoni ya Kamati au Uchambuzi wa Kamati, unaonesha kwamba Tanzania tunavyo vijiji 19,600, tunahitaji shilingi bilioni 980. Serikali imetenga asilimia sita tu ambayo ni shilingi bilioni 59 na milioni 500. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata nisipoendeea kusoma taarifa hii ya Kamati lakini utaona kabisa kwamba tunayo changamoto ambayo bado ni kubwa sana kwa sababu inaonesha wazi sasa ni vijiji vichache sana, yapata vijiji 1,000 ndiyo ambavyo vitafaidika na hii shilingi milioni 50. Ni masikitiko makubwa sana. Hivi tunaenda kurudi vipi kule kwa wananchi? Tutawaeleza nini wananchi wetu kuhusiana na suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji? Naiomba Serikali ifuate ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti kwamba waongeze pesa walau ifikie asilimia 20 japokuwa na fedha hii bado ni ndogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba Sheria ya Manunuzi iletwe…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.